Loading...

Mbunge aliyejitabiria kifo afariki dunia.

Mbunge wa Jimbo la Dimani Mhe. Hafidh Ali Tahir ( katikati ) akisisitiza jambo enzi za uhai wake.
Mbunge wa Dimani (CCM), Hafidh Ali Tahir, ambaye siku kumi zilizopita aliuliza swali bungeni kuhusu mrithi wa nafasi inayoachwa na mbunge anayefariki, ameaga dunia usiku wa kuamkia jana.

Mbunge huyo amefariki kutokana na shinikizo la damu usiku wa siku ambayo Bunge lilikuwa linaahirishwa baada ya kuuliza swali hilo siku ya kwanza ya Mkutano wa Tano wa Bunge la Kumi na Moja.

Swali lake la mwisho bungeni lilihoji sababu za Serikali kutoona umuhimu wa kumpa ubunge mtu aliyeshika nafasi ya pili katika kura za maoni za chama chake pindi inapotokea kifo cha mbunge aliyeshinda kwenye uchaguzi.

Tahir aliuliza swali hilo Novemba Mosi. Swali hilo, licha ya kuzua mjadala mkali, mbunge huyo alionekana kusimamia kile alichoamini.

“Mheshimiwa mwenyekiti, ni kwanini Serikali isifikiri namna bora ya kufanya mabadiliko katika sheria ya uchaguzi ili mshindi wa kiti cha ubunge akifariki, usiitishwe uchaguzi na badala yake aliyekuwa mtu wa pili ndiye achukue nafasi hiyo?” alihoji Tahir.

Mbunge huyo alisema uchaguzi hutumia fedha za ziada na pia kusababisha migogoro. Pia alipendekeza katika uchaguzi, iwapo mgombea mwenza akifariki uchaguzi usiahirishwe.

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Vijana, Ajira na Walemavu), Dk Abdallah Possi alijibu swali hilo akisema mpango huo unaweza kuwa mzuri ikiwa utapitia hatua zote hadi ufikishwe bungeni kwa ajili ya kutungwa sheria.

Majibu hayo yalimridhisha mbunge huyo ambaye alifariki dunia akiwa Hospitali ya Rufaa ya Dodoma. Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk James Kilogwe alisema alikwenda mwenyewe hospitali hapo kutibiwa shinikizo la damu.

“Alifika hospitali saa 8:00 usiku (kuamkia jana) akiwa anasumbuliwa na blood pressure (shinikizo la damu). Lakini wakati anaendelea na matibabu alipata stroke (kiharusi) na muda mfupi baadaye alifariki dunia,” alisema Dk Kilogwe.

Spika wa Bunge, Job Ndugai alisema walikuwa na mbunge huyo hadi juzi usiku kwenye kikao cha Bunge Sports Club kilichoketi kuandaa mashindano ya mabunge ya Afrika Mashariki na hakuwa na dalili za kuugua.

Alisema mbunge huyo alishiriki semina na wabunge wenzake kwenye Hoteli ya New Dodoma na kikao cha Bunge cha juzi jioni.

“Alikuwa miongoni mwa wabunge walioomba kwenda Urambo kwenye mazishi ya spika mstaafu (Samuel Sitta). Tumeondokewa na mbunge mchapakazi, mcheshi, mwanamichezo na aliyewajali sana wapigakura wake,” alisema.

Ndugai alisema kwa mujibu wa Kanuni ya Bunge 152, inapotokea mbunge amefariki wakati Bunge likiwa katika shughuli zake, Spika ataahirisha shughuli kwa siku hiyo kwa ajili ya maombolezo.

Alimtaka Waziri Mhagama kutengua kanuni ili wabunge waweze kuomboleza msiba huo na pia kufanyika kikao maalumu cha kuaga mwili wa Sitta.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Sheria Ndogo, Andrew Chenge pia alitakiwa na Spika Ndugai kuhitimisha hoja yake ya taarifa ya utendaji kazi wa kamati hiyo iliyowasilishwa juzi ili ikafanyiwe kazi na Serikali. Chenge alihitimisha kwa muda mfupi hoja hiyo bila kuchangiwa na wabunge, tofauti na utaratibu wa Bunge. Baada ya kikao kuahirishwa, wabunge waliuaga mwili wa Tahir.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema ni jambo la kushtua kwa kuwa juzi walikuwa na Hafidh na alishiriki mambo mbalimbali ya Bunge.

“Leo (jana) tunazungumza akiwa katika hali nyingine, ni jambo la huzuni kwetu na ni funzo pia. Serikali kupitia Rais John Magufuli inatoa pole kwa Spika na wafiwa wote,” alisema.

Kiongozi wa Kambi ya Upinzani bungeni, Freeman Mbowe alisema msiba huo uwe somo kwa wabunge kwa kuwa unawakumbusha kupendana na kuheshimiana. Alisema Tahir alikuwa mcheshi na mstarabu.

“Safari ya Tahir ni yetu sote, katika maisha haya tumepewa na Mungu na ana mamlaka ya kuchukua wakati wowote. Ni vyema tukaishi na kutambua tofauti zetu hapa duniani ni za muda mfupi. Alikuwa mwana-Yanga mwenzangu, alikuwa ni mtu wa kuunganisha wabunge pamoja na hajawahi kukwazana na mbunge,” alisema Mbowe.

Almas Maige, mwakilishi wa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ambayo Tahir alikuwa mjumbe, alisema marehemu atakumbukwa katika kusimamia ukweli wakati wote kwenye kamati hiyo.

Naghenjwa Kaboyoka, mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) ambayo Tahir pia alikuwa mjumbe, alisema wamepata pigo kubwa kwa kuwa “alikuwa mcheshi, alipenda kutuchekesha pale tunapokuwa tumechoka, tunapofanya kazi hadi usiku. Alikuwa mchangiaji mzuri”.

Mbunge wa Buhigwe (Chadema), Kasuku Bilago alisema Tahir alikuwa na upendo na utani. “Nilikuwa nakaa katika kiti cha kulia, Tahir kushoto kwangu na jana (juzi) nilipokuja bungeni alinitania kuwa nilikuwa nimekosa kuuliza swali la nyongeza. Tukacheka kweli. Nimepoteza jirani wa kukaa naye na kila nikitazama kiti chake nitakuwa nakumbuka mengi,” alisema.

Vilio na simanzi

Mwili wa Tahir uliwasili viwanja vya Bunge saa 3:27 asubuhi na Spika Ndugai aliongoza viongozi na wabunge kuupokea, huku baadhi wakiangua vilio. Mbunge wa Viti Maalumu (CUF), Miza Bakar Haji alianguka hivyo kumlazimu Naibu Waziri wa Afya, Dk Hamisi Kigwangalla kusaidiana na wauuguzi na daktari wa zahanati ya Bunge kutoa huduma ya kwanza.

Baadaye walimchukua mbunge huyo kwa kutumia kiti maalumu cha kubebea wagonjwa kumpeleka zahanati ya Bunge.

Kabla ya kwenda uwanja wa ndege, Ndugai aliwatangazia wabunge kuwa posho yao ya kikao cha jana itagawanywa mara mbili kwa ajili ya rambirambi kwa familia ya Tahir na Mbunge wa Urambo, Margaret Sitta ambaye ni mke wa marehemu Samuel Sitta.

ZeroDegree.
Mbunge aliyejitabiria kifo afariki dunia. Mbunge aliyejitabiria kifo afariki dunia. Reviewed by Zero Degree on 11/12/2016 12:01:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.