Loading...

Wachezaji Simba kukatwa mishahara.

Kocha wa Simba Joseph Omog.
OMOG ametishia kumkata mshahara mchezaji yeyote atakayechelewa kuripoti kwenye mazoezi ya timu hiyo kwa ajili ya kujiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, ambao umepangwa kuanza Desemba 17 mwaka huu.

Simba ndiyo vinara wa ligi hiyo wakiwa na pointi 35, wamepanga kuanza mazoezi leo Jumatatu, kujiandaa na ligi hiyo ambayo imeonesha kuwa na ushindani mkubwa msimu huu.

Akizungumza na gazeti hili Omog, raia wa Cameroon, alisema amezungumza na wachezaji wote wakati akiagana nao kwenda kwenye mapumziko hayo mafupi hivyo hatokuwa na msamaha kwa yeyote ambaye atachelewa kufika mazoezini pasipo sababu za msingi.

“Simba ni timu kubwa na ina malengo yake iliyojiwekea malengo yetu msimu huu ni ubingwa na ili tuchukue ubingwa lazima tufanye kila kitu kwa pamoja na kwa wakati haiwezekani wengine waje siku ya kwanza wengine wachelewe wote ni kitu kimoja ndiyo maana nimesisitiza kukata mshahara kwa kila atakayechelewa,”alisema Omog.

Kocha huyo alisema wachezaji wote wa Simba ni profeshno, wanatambua majukumu yao na mikataba yao inavyoelekeza hivyo haoni sababu ya kupigizana kilele kwa sababu kila mtu anatambua wajibu wake kutokana na kanuni za klabu zinavyoelekeza.

Alisema kwa kutambua hilo ndiyo maana yeye kama kiongozi mkuu tayari, amewasili kwenye kituo cha kazi tayari kwa maandalizi hayo ambayo wanalazimika kuyafanya kwa umakini ili kutimiza kile ambacho wamekusudia kukifanya msimu huu nacho ni ubingwa.

“Ligi imekuwa ngumu na yenye ushindani hivyo bila kujipanga mapema tunaweza kupoteza nafasi yetu ya kuongoza ligi ifahamike kwamba tupo mbele kwa tofauti ya pointi mbili kati yetu na Yanga, kwa hiyo ni lazima tufanye jitihada kwa kuongeza bidii ya kupambana ili kupate kile tunachokihitaji,” alisema Omog.

Simba inalazimika kupambana kufa au kupona ili kutwaa ubingwa msimu huu baada ya kupita katika kipindi kigumu cha misimu mitatu bila kutwaa taji lolote katika michuano yote iliyoshiriki ndani ya nchi.

Source: Habari Leo
ZeroDegree.
Wachezaji Simba kukatwa mishahara. Wachezaji Simba kukatwa mishahara. Reviewed by Zero Degree on 11/28/2016 10:14:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.