Loading...

Kigogo Chadema achezea kichapo, alazwa.

KATIBU wa muda wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Wilaya ya Kyela, Mponjoli Mwaikimba, amenusurika kufa baada ya kuvamiwa na kundi la wanachama walioingia kwenye ofisi za chama na kumpiga na kumsababishia maumivu makali.


Patashika hiyo ilitokea jana saa tano asubuhi wakati katibu huyo akiwa ofisini kwake makao makuu ya Chadema wilaya, mjini hapa. Wanachama hao waliingia ndani na kuanza kumcharaza makofi na baadaye kumwacha akiwa hoi.

Mwenyekiti wa muda wa chama hicho wilayani hapa, Philemon Mahenge, alisema alipata taarifa za uvamizi huo na alipofika ofisini, wavamizi walikuwa wametokomea ndipo alipochukua jukumu la kwenda kumpeleka polisi kutoa maelezo na baadaye kupewa fomu ya matibabu na kumpeleka hospitalini.

Alisema kitendo kilichofanywa na watu hao, hakivumiliki na kuwa walipotoa ripoti polisi na kuwataja baadhi ya wanachama waliohusika, wanachama wawili walikamatwa huku wengine wakiendelea kutafutwa.


Mahenge aliwataja waliokamatwa kwa tuhuma za kumpiga katibu huyo ni Jackson Mwaipasi ambaye ni Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mwaikambo na Davis Denis mwanachama kutoka Kata ya Bondeni na wanashikiliwa na polisi.

Alisema chama kwa sasa kiko kwenye mgogoro mzito toka kumalizika kwa uchaguzi mkuu Oktoba, mwaka jana, uliosababisha mwenyekiti wa chama wilaya, Saadat Mwambungu na kamati yote ya tendaji kuvunjwa na kuunda uongozi wa muda.

Mahenge alisema kuhusu masuala ya uvamizi wanawaachia polisi wafanye kazi yao na kama kuna masuala ya kichama ndani yake watakaa kwenye vikao kujadili na kuchukua hatua.

Hata hivyo, Mwaikimba hakuweza kusema lolote kwa waandishi wa habari kutokana na maumivu aliyokuwa nayo huku akilalamika kuumizwa sehemu za nyuma ya kichwa na shavuni kutokana na kipigo.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Kyela, Dk. Francis Mhagama, alikiri kumpokea kiongozi huyo na kusema kuwa wanaendelea kumpatia matibabu kutokana na kulalamika kuumia katika baadhi ya sehemu za mwili.

Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Dhahiri Kidavashari, alikiri kuwapo kwa tukio hilo na kusema licha ya kuwashikilia watu wawili, pia wanaendelea kuwasaka watu wengine waliohusika na uvamizi huo.

Source: Nipashe
ZeroDegree.
Kigogo Chadema achezea kichapo, alazwa.  Kigogo Chadema achezea kichapo, alazwa. Reviewed by Zero Degree on 12/16/2016 10:08:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.