Loading...

Mapya yaibuka mtoto aliyefia bwawani hotelini.

Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Charles Mkumbo.
SAKATA la mtoto wa miaka 12 aliyekufa wakati akiogelea katika bwawa la hoteli ya kitalii ya Mount Meru mjini hapa, limechukua sura mpya baada ya kugundulika kuwa bwawa hilo lilijaa damu baada ya kifo chake.

Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Charles Mkumbo amethibitisha madai ya mashahidi waliokuwa eneo la tukio, waliodai kuwa bwawa la kuogelea la hoteli hiyo liligeuka kuwa dimbwi la damu wakati mwili wa mtoto huyo ukiopolewa kutoka bwawa hilo, siku ya Krismasi.

“Inaaminika kuwa kichwa cha Clifford Alex kilipasukia ndani ya bwawa la kuogelea,” alisema, kamanda huyo wa Polisi wakati akitolea ufafanuzi kifo hicho kilichozua utata mjini Arusha.

Kuna madai kwamba Clifford alijirusha kwenye dimbwi ili aogelee, lakini kichwa chake kilipiga kwenye ukingo wa bwawa hilo la kuogelea na hivyo kusababisha kifo chake, ingawa baadhi ya watu wanadhani kuwa alisukumwa. Uongozi wa hoteli ya Mount Meru pia haujatoa tamko rasmi kuhusu tukio hilo na kwa nini watoto waliruhusiwa kuogelea bila ya kuwa na msimamizi.

“Tunachunguza tukio hilo na ikiwa itabainika kuwa hoteli ilifanya uzembe basi tutaichukulia hatua,” alisema Kamanda Mkumbo.

Tukio hilo lilitokea katika siku ya Krismasi wakati mtoto huyo aliyekuwa anasoma darasa la tano katika shule ya Sekei ya mjini hapa, alipokwenda na wenzake kuogelea katika bwawa la hoteli hiyo mchana wa Jumapili.

Mama wa mtoto, Christina Michael, mkazi wa eneo la Idara ya Maji Sekei, anaeleza kuwa mwanawe huyo alitoka nyumbani majira ya mchana kwenda matembezini na wenzake, lakini ilipofika saa moja usiku, watoto wengine walirejea ila mwanawe hakuwepo.

“Nilipowauliza walisema kuwa Clifford amebaki kwenye maji kule Mount Meru, basi haraka nikaenda pale hotelini lakini wakaniambia kuwa ameshapelekwa Hospitali ya Arusha International Conference Center (AICC) Kijenge kwa matibabu,” alisema.

Hata hivyo, mama huyo alipofika hospitalini alikuta mwili wa mtoto huyo umefunikwa kwa shuka nyeupe na hapo hata yeye akaishiwa nguvu na kuanguka akijua Cliff ameshakufa.

Watoto wenzake walioandamana na Cliff kwenda kuogelea hotelini hapo, Kelvin Celestine na Passon Alex ambao wanasema kuwa walikuwa hawana pesa za kulipia hotelini, hapo ndipo wakamuomba mlinzi awaruhusu kuogelea bure. Mlinzi huyo aliwaruhusu kuogelea kwenye eneo maalumu la watoto.

Lakini inasemekana kuwa baadaye giza lilipoanza kuingia Cliff aliwaacha wenzake na kwenda kuogelea kwenye bwawa la wakubwa na huko ndiko mauti yalimkuta. Hata hivyo, haijulikani kama kweli alijipeleka mwenyewe au alishawishiwa kwenda kwenye bwawa hilo la wakubwa au hata kama kuna mtu asiyejulikana aliyemsukumia humo.

Babu wa marehemu, Emmanuel Magie amesema wanasuburi ripoti ya daktari kuhusu kifo cha Cliff na wameshangazwa kuona uongozi wa hoteli haukuwa na taratibu ya kuwawekea waangalizi watoto wanaokwenda kuogelea.

Ripoti za kifo cha mwanafunzi huyo zilikuwa hazijawafikia polisi wakati tunakwenda mitamboni, lakini Mwenyekiti wa Mtaa wa Sekei, Alphayo Mollel anayesimamia eneo ambalo hoteli hiyo ilipo, anasema bado anawasiliana na uongozi waeleze kwa nini watoto waliruhusiwa kuogelea hadi usiku.

Source: Habari Leo
ZeroDegree.
Mapya yaibuka mtoto aliyefia bwawani hotelini. Mapya yaibuka mtoto aliyefia bwawani hotelini. Reviewed by Zero Degree on 12/28/2016 12:18:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.