Loading...

Rais Magufuli kukagua Gwaride la kwanza la maadhimisho ya miaka 55 ya Uhuru wa Tanganyika.

Rais John Magufuli, anatarajiwa kukagua gwaride la kwanza la maadhimisho ya miaka 55 ya Uhuru wa Tanganyika.

Gwaride hilo litapambwa na vikosi mbalimbali vya majeshi ya ulinzi na usalama. 
Aidha, makomandoo wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), watafanya maonyesho yao na yanatarajiwa kuwa kivutio kwa wengi.

Maadhimisho ya mwaka huu, yatakuwa ya kwanza kwa Rais Magufuli ambaye ana mwaka mmoja na mwezi mmoja ofisini baada ya mwaka jana kufuta shamrashamra za miaka 54 ya maadhimisho kama hayo.

Baada ya kufuta shamrashamra hizo, aliagiza siku hiyo itumike kufanya usafi nchi nzima ili kupambana na ugonjwa wa kipindupindu uliokuwa umepamba na kuagiza Sh. bilioni nne zilizotarajiwa kutumika kwa shughuli hiyo, zitumike kupanua barabara ya Bagamoyo, kutoka Mwenge mpaka Morocco.

Jana, vikosi vya Jeshi la Majini, Nchi Kavu na Anga, vilifanya maandalizi katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam saa 4:00 asubuhi.

Katika maandalizi hayo, kikosi cha makomandoo wa JWTZ, kilionekana kuwa kivutio kwa wengi baada ya kuonyesha baadhi ya mafunzo ya kujihami na adui na kupambana naye.

Mbali na Kikosi hicho cha Makomandoo, pia Kikosi cha Bendera kilionyesha kujiandaa vizuri katika sherehe hizo ambazo zinatarajiwa kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka ndani na nje ya Tanzania.

Kadhalika, vikosi vya Jeshi la Magereza, Kutuliza Ghasia (FFU), Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Polisi na JWTZ, vilionyesha ukakamavu wa kupiga gwaride, hali iliyoashiria vikosi hivyo vimejiandaa vizuri.

Akizungumza baada ya kumalizika kwa maandalizi hayo, Msimamizi Mkuu wa Gwaride, Brigedia Jenerali Dominic Mrope, alisema askari hao wamefanya mazoezi kwa mwezi mzima na watafikia tamati kesho.

Alisema maandalizi yao yamekwenda vizuri na tayari wamekamilika kwa asilimia 99.

Brigedia Jenerali Mrope alisema jambo jipya litakalokuwapo na kubainika kwa wananchi, ni kikundi cha kwata ya kimya kimya, lakini kwa askari wenyewe wamefanya mabadiliko ambayo kwa wananchi ni vigumu kuyabaini.

Aliwataka wananchi kwenda kushuhudia maonyesho hayo kwani majeshi yanafanya maadhimisho kwa niaba ya wananchi, lakini sherehe za Uhuru ni kwa wananchi wote.

ZeroDegree.
Rais Magufuli kukagua Gwaride la kwanza la maadhimisho ya miaka 55 ya Uhuru wa Tanganyika. Rais Magufuli kukagua Gwaride la kwanza la maadhimisho ya miaka 55 ya Uhuru wa Tanganyika. Reviewed by Zero Degree on 12/08/2016 10:07:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.