Loading...

Sababu 3 zilizosababisha kifo cha straika wa Mbao Fc zatajwa.

MWILI wa mshambuliaji wa Mbao, Ismail Mrisho Khalfan, unatarajiwa kuzikwa leo kwenye makaburi ya Mabatini Wilaya ya Nyamagana jijini Mwanza, baada ya kufikwa na umauti wakati wa mchezo wa ligi ya vijana chini ya umri wa miaka 20.

Ismail alifariki dunia juzi jioni mjini Bukoba baada ya kuanguka uwanjani dakika ya 74 Uwanja wa Kaitaba, Bukoba dakika chache baada ya kuifungia bao timu yake katika ushindi wa 2-0.

Kufuatia kifo hicho, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) liliunda Kamati ya Tiba ili kufanya uchunguzi wa kifo cha mchezaji huyo ambapo Katibu Msaidizi wa Chama cha Wataalamu wa Tiba ya Michezo Tanzania (TASMA), Shecky Mngazija, alisema zipo sababu nyingi zinazopelekea vifo vya wachezaji uwanjani.

Alizitaja sababu ambazo huenda zimechangia kifo hicho ambazo ni pamoja na mchezaji kugongwa sehemu ambayo si sahihi na kuleta athari huku pia inategemea amegongwa sehemu gani ya mwili wake.

“Kitaalamu inaitwa ‘sudden deaths’, vifo vya ghafla vinatokea michezoni kwa sababu nyingi ila sababu ya kubwa ni huenda aligongwa sehemu ambayo kiwango cha kumgonga kimekuwa kikubwa, wengine wanagongwa sehemu ya kichwani, tumboni na baadhi ya viungo vya tumbo huenda viliumia kwa kiasi kikubwa,” alisema.

Mganzija aliitaja sababu nyingine ni furaha au huzuni ikizidi sana huenda ikasababisha kifo, kitaalamu kila kitu kinatakiwa kiwe kwa kiasi.

“Kila kitu kinatakiwa kiwe kwenye kiasi kama furaha ikizidi sana ule mwili unashindwa kustahimili ile furaha na inapelekea kuzidi katika kiwango na unaweza upate tatizo hilo la kifo au huzuni imezidi sana mwilini ambapo mara nyingi vifo vya namna hii vipo sana michezoni.

“Kwenye mechi mfano ya Simba na Yanga mtu anashindwa kustahimili huzuni ya kiasi au furaha iliyopitiliza ndio maana unasikia shabiki afa uwanjani, vifo hivi hutokea mara nyingi.”

Katibu huyo msaidizi wa TASMA aliendelea kusema kuwa jamii inapaswa kuelewesha mashabiki kwanza wasiende uwanjani wakiwa na matokeo ili kuepuka vifo vya namna hiyo.

“Ukienda na matokeo lazima timu yangu ishinde ile timu ikafungwa basi utakuwa na huzuni ya kupitiliza, mwili unashindwa kuhimili ile huzuni na huweza kusababisha kifo na pia ukiwa na furaha labda utafunga na baadaye ikashinda utakuwa na furaha ya kupitiliza na baadaye mwili utashindwa kuhimili baadhi ya ‘hormone’ ambapo kuna vitu mwilini vikizidi sana vinaweza kuleta athari kila kitu kinatakiwa kiwe kwa wastani kama ni furaha isizidi sana ikasababisha vitu vingine,” alisema.

Alisema kitu kingine kinachosababisha vifo hivyo vya ghafla ni maradhi ya muda mrefu ambayo hayajajulikana kama tatizo la ini, figo au moyo.

“Sheria ya Fifa, CAF na TFF inashauriwa uchunguzi wa afya ya wachezaji kabla ya mashindano ambapo husaidia kutambua maradhi na utimamu wa mwili na akili ambapo kama mchezaji atakuwa na maradhi ambayo hayajagundulika basi huenda ikasababisha kifo cha ghafla.

“Kupima afya ni kitu cha msingi sana na wanaangalia utimamu wa mwili na akili kwa sababu inawezekana mchezaji ana shida ya mapafu, figo au hata ini sasa anapofanya mazoezi katika kiwango fulani inaweza kuzidisha au kupunguza,” alisema.

Alimaliza kwa kusema kwa sasa wanasubiri ripoti ya madaktari wenzao mkoani Mwanza ambao ndio wataeleza kwa kina sababu hasa za kifo hicho.

“Hatuwezi kujua kama alikuwa na shida ya ini au moyo, ila kwa kuwa madaktari watafanya uchunguzi wa kina itagundulika tu kama lilikuwa na tatizo la muda mrefu au limempata pale pale uwanjani,” alisema.

Katika hatua nyingine, Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Deodatus Kinawilo, amesema wamepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha straika huyo tegemeo wa kikosi hicho cha Mbao.

Kinawilo aliyasema hayo jana wakati wa kuaga mwili wa mchezaji huyo katika Hospitali ya Rufaa Mkoa ya Kagera.

“Serikali inaungana na ndugu na jamaa wa marehemu kwa kipindi hiki, tumetoa usafiri ili uweze kusafirisha mwili wa marehemu hadi jijini Mwanza kwa ajili ya maziko,” alisema Kinawilo.

Ismail alifariki dunia juzi jioni mjini Bukoba baada ya kuanguka dakika ya 74 katika Uwanja wa Kaitaba, dakika chache baada ya kuifungia bao timu yake katika ushindi wa 2-0.

Source: Bingwa
ZeroDegree.
Sababu 3 zilizosababisha kifo cha straika wa Mbao Fc zatajwa. Sababu 3 zilizosababisha kifo cha straika wa Mbao Fc zatajwa. Reviewed by Zero Degree on 12/06/2016 11:09:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.