Loading...

Sababu za Rais Magufuli kufumua muundo wa Chama Cha Mapinduzi [CCM].

WAKATI mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk John Magufuli alipokuwa akipiga push up katika mikutano ya kampeni za urais mwaka jana na kuibuka na falsafa yake ya ‘Hapa Kazi Tu,’ baadhi ya wanasiasa na hata wananchi wa kawaida, waliona kwamba hiyo ilikuwa ni sehemu au janja ya kujipatia kura kwa wananchi.

Dk Magufuli alivutia watu wengi wakati alipoanza kupiga push up kusisitiza falsafa yake hiyo ya ‘Hapa Kazi Tu’ ambayo alianza nayo tu baada ya Mkutano Mkuu wa CCM, Julai mwaka jana kumteua kuwa mpeperushaji wa bendera ya chama hicho kikongwe na tawala nchini.

Akajizolea maelfu ya wananchi kwenye mikutano yake ya hadhara, na kila alipopanda jukwaani, yeye alikuwa akisisitiza kwamba anakusudia kuingia Ikulu ya Magogoni, Dar es Salaam, akiwa na dhamira moja tu ya kuwatumikia Watanzania kwa kufanya kazi.

Mwaka mmoja sasa madarakani, Watanzania wameisoma namba. Hakuna anayebisha kwamba Rais Magufuli ametembea katika maneno yake. Utawala wake umejikita katika kusisitiza kufanya kazi kwa kila mmoja kuanzia yeye mwenyewe, serikali yake na Watanzania wote kwa ujumla.

Kwake msamiati mkubwa ni kufanya kazi. Hataki maneno maneno mengi. Hana muda huo, ndio maana alianza kwa kuhakikisha kila mmoja anafanya kazi na anafaidika na matunda ya jasho lake.

Hivyo akawashughulikia kuanzia watumishi hewa hadi wanafunzi hewa kuhakikisha wanaofaidika na jasho hilo ni walengwa na si vinginevyo. Katika kuthibitisha kwamba amepania kila mahali pawe ni mahali pa kazi, sasa amehamishia falsafa hiyo kwenye chama chake, CCM.

Amekifumua chama hicho tawala akitembea katika maneno yake aliyoyaahidi Julai mwaka huu alipochaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Taifa wa CCM mjini Dodoma.

Aliwaahidi wanaCCM kwamba anataka kuijenga CCM mpya ikiwamo kuondokana na vyeo visivyokuwa na tija na pia kupunguza idadi ya wajumbe wakiwamo wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ambao walichaguliwa hata katika ngazi ya wilaya.

Katika kikao chake cha kwanza kuongoza NEC tangu ashike wadhifa wa uenyekiti, Dk Magufuli alipeleka hoja na mapendekezo makubwa ya kukifumua chama hicho, ambayo pengine kwa kuelewa falsafa ya mwenyekiti wao, wajumbe wa NEC hawakuwa na jinsi nyingine zaidi ya kukubaliana naye.

Kwa hiyo, kuanzia mwakani wakati CCM itakapokuwa inafanya uchaguzi wake wa ndani, tutaona muundo mpya wa chama hicho kikongwe ambao utapungua wajumbe wa kuanzia Kamati Kuu, NEC hadi katika ngazi za wilaya ambako vikao vya maamuzi navyo vimeguswa.

Msingi mkubwa wa mabadiliko hayo ya muundo wa CCM ni kwenda na falsafa ya ‘Hapa Kazi Tu’ ambayo imejikita sasa katika utendaji wa serikali na sasa Dk Magufuli anaipeleka CCM ambako amepunguza idadi ya wajumbe wa vikao na idadi ya vikao katika ngazi mbalimbali ili viongozi watumie muda mwingi kufanya kazi za chama.

Kwa mujibu wa CCM, uamuzi huo una lengo la kuongeza ufanisi wa utendaji wa chama na kuongeza muda wa viongozi kufanya kazi za chama kwa umma, badala ya kutumia muda mwingi vikaoni. Dk Magufuli hapendi maneno mengi anataka vitendo.

Hivyo, unapoyatazama mabadiliko hayo makubwa kufanywa na CCM ya Dk Magufuli katika miezi michache tu tangu achaguliwe kuongoza chama hicho, unaona kabisa yaanakisi yale masuala muhimu aliyoyapa kipaumbele katika Serikali ya Awamu ya Tano.

Hapa unazungumzia kubana matumizi, kukabiliana na rushwa, kuondokana na watumishi (wanachama) hewa, kuondokana na watumishi wasio na kazi (kufuta vyeo visivyo vya lazima), kudhibiti ubadhirifu na matumizi ya rasilimali za umma na kuondokana na tabia ya mtu mmoja kulundikiwa vyeo vingi.

Kwa kupunguza idadi ya wajumbe katika vikao, CCM ya Dk Magufuli si tu imeokoa rasilimali fedha na muda, lakini pia itaongeza ufanisi wa vikao hivyo na kuwa vyenye msingi wa kujenga zaidi kuliko kuwa vikao vya kulumbana, vyenye kujenga makundi, visivyo na tija na wakati mwingine kutumiwa na baadhi ya wanasiasa kwa ajili ya malengo yao. Piga picha ya kilichotokea katika NEC ya mwisho ya kupitisha majina ya uteuzi wa wagombea wa urais wa CCM mwaka jana.

Jinsi baaadhi ya wajumbe walivyoamua kukiuka utamaduni wao wa kumsifu mwenyekiti anapoingia kuendesha vikao, na badala yake kuimba jina la mmoja wa wagombea ambaye alikwisha kuenguliwa katika kinyang’anyiro. Ulikuwa ni usaliti kwa chama. Ndio maana Dk Magufuli anasema anataka kuwa na chama kinachoongoza badala ya mwanachama/wanachama kuongoza chama.

“Tunataka kuwa na chama ambacho kinaongoza, sio mwanachama kuongoza chama. Tunataka chama kuwa mali ya wanachama, badala ya mwanachama kuwa mali ya chama,” Dk Magufuli aliwaeleza wajumbe wa NEC katika kikao cha wiki iliyopita katika Ikulu ya Dar es Salaam.

Lakini pia msingi mwingine muhimu katika muundo huo mpya ni kwamba utasaidia kulinda siri za chama katika vikao hivyo. Hakuna ubishi kuwa siri za vikao vingi vya CCM vilikuwa vikivuja sana katika mikutano yake, na wakati mwingine wanaovujisha wanafanya hivyo kwa maslahi binafsi. Hilo linathibitishwa na kauli ya mwanasiasa mkongwe aliyewahi kuwa Mjumbe wa NEC, Dk Christant Mzindakaya ambaye anasema,

“Kawaida maamuzi makubwa ya chama yanayofanyika ni siri, lakini hali ilikuwa tofauti kwani kila siri ilikuwa ikitoka nje; huku kuwa na utitiri wa viongozi kulisababisha chama kupata gharama kwa kuwalipa pale inapoitishwa mikutano ya Halmashauri Kuu.”

Lakini pia uamuzi wa muundo mpya pia unafuta kujilimbikizia vyeo kwa wanachama wa CCM kwani kama alivyokusudia katika serikali, mtu mmoja cheo kimoja, sasa hali hiyo Dk Magufuli ameipeleka CCM.

Hakutakuwa tena na Mbunge huyo huyo M-NEC, huyo huyo Mwenyekiti wa CCM Mkoa nk, hasa kwa wale wenye nafasi za uongozi kwa kazi za muda wote kama zilivyoainishwa na Kanuni za Uchaguzi za CCM Toleo la 2012 Kifungu cha 22 na 23.

Nafasi hizo ni Mwenyekiti wa Tawi/Kijiji/Mtaa, Mwenyekiti wa Kata/Wadi, Mwenyekiti wa Jimbo, Wilaya na Mkoa, Makatibu wa Halmashauri Kuu kwa ngazi zote zinazohusika, na Mbunge, Mwakilishi na Diwani.

Kwa sasa, ndani ya CCM kulikuwa na tabia ya baadhi ya watu kujilimbikizia vyeo kwani ilikuwa si jambo la ajabu kumuona mbunge akiwa pia ni Mjumbe wa NEC na wakati mwingine ni mwenyekiti wa chama hicho mkoa. Hali ilisababisha wanachama wengine kukosa fursa kutokana na wajumbe hao kulinda maslahi yao binafsi ya kisiasa na kiuchumi.

Ndio maana Dk Magufuli anasema anataka kukirejesha chama kwa wananchi wa chini (wanachama wanyonge) kama anavyoeleza katika serikali yake kwamba atasimamia kutetea wananchi wanyonge.

Lakini pia mabadiliko haya ya CCM ya Dk Magufuli yanaonesha dhahiri anataka kukirejesha chama kwa wanachama na kukipa uhai mpya na nguvu ya kukabiliana na mazingira ya kisiasa ya leo, kama anavyothibitisha Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na mchambuzi wa masuala ya kisiasa na kijamii nchini, Dk Benson Bana.

“Hiki ni chama cha wanachama kwa ajili ya wanachama na alichokifanya Magufuli ni kuonesha nia ya kufanya,” alisema Bana.

Kuthibitisha kwamba Dk Magufuli anataka CCM yake iakisi kile anachokifanya ndani ya serikali, suala la rushwa na uhakiki wa wanachama wa chama hicho ni miongoni mwa mambo ambayo amesema yatapewa kipaumbele kikubwa katika uenyekiti wake.

Katika rushwa, amewahakikishia kwamba katika utawala wake ndani ya CCM, hatawasamehe viongozi wala rushwa na wanaotoa rushwa.

“Kamwe msichague walarushwa. Hatutawasamehe viongozi wala rushwa. Wametuumiza sana, lazima tufike mahali tuseme basi,” alisema Dk Magufuli, huku akibainisha kuwa kwa kutumia vyombo vya uchunguzi watahakikisha wanaondoa viongozi pandikizi pamoja na kufuta chaguzi zote zitakazohusisha rushwa.

Aidha, suala la uhakiki ni muhimu hasa kwa kufahamu idadi halisi na ya kweli ya wanachama wake, lakini zaidi litasaidia katika kushughulikia wanachama waliosaliti katika chaguzi hasa Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.

Je, walikuwa wanachama kweli au pandikizi? Hapa jibu linaweza kupatikana. Kwa ujumla, muundo na mabadiliko haya makubwa ya kwanza, tena katika muda mfupi wa uongozi wake ndani ya CCM, yanadhihirisha kuwa Dk Magufuli ameamua kuifanya CCM iendane na mazingira ya sasa ya kubana matumizi, kukabiliana na rushwa kwa vitendo, kuondokana na kazi zisizo na lazima, lakini kubwa zaidi kuwatumikia wananchi (wanachama) walioweka viongozi madarakani.

Hakuna shaka haya yatakuwa mabadiliko chanja katika chama tawala, hasa ikizingatiwa hali ya kisiasa ilivyo nchini na uelewa mkubwa wa wananchi katika masuala ya kisiasa hivyo kuhitaji chama kinachoakisi hisia za wanachama wake na kuzipa kile inachotaka.

Source: Habari Leo
ZeroDegree.
Sababu za Rais Magufuli kufumua muundo wa Chama Cha Mapinduzi [CCM]. Sababu za Rais Magufuli kufumua muundo wa Chama Cha Mapinduzi [CCM]. Reviewed by Zero Degree on 12/20/2016 10:45:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.