Loading...

Simbu afunguka waliombeza Olimpiki

BAADA ya kumaliza katika nafasi ya tano katika Michezo ya Olimpiki ya Rio, Brazil 2016 na kupokewa kwa shamshamra, baadhi ya wadau wa michezo waliMbeza na kusema hakustahili mapokezi hayo.

Simbu alimaliza katika nafasi ya tano kwa kutumia muda wa saa 2:11:15 ikiwa ni nafasi ya juu zaidi kuwahi kufikiwa na wanariadha wa Tanzania licha ya kutofikia ule muda uliowekwa na Juma Ikangaa wa saa 2:11:10 alioweka katika Olimpiki ya Los Angeles, Marekani 1984 alipomaliza wa sita.

Kudhaminiwa na DStv Simbu baada ya kumaliza wa tano Kampuni ya MultiChoice-Tanzania ilijitokeza kumdhamini mwanariadha huyo ili aweze kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali ya kimataifa.

Mwanariadha huyo anakiri kuwa udhamini wa MultiChoice umemsaidia sana kwani umemuwezesha kuelekeza nguvu zake katika mazoezi tu badala ya kufikiria jinsi ya kuendesha familia.

“Kwa kweli udhamini wa Multi Choice umenisaidia sana, kwani sasa akili yangu yote naielekeza katika mazoezi badala ya kufikiria fedha za kuihudumia familia yangu", anasema Simbu mwenye mke na mtoto mmoja.

Kujiunga na Jeshi Awali, Simbu alikuwa raia lakini baada ya kufanya vizuri katika riadha, sasa amepata 'shavu' lingine baada ya kulamba ajira katika Jeshi la Kujenga Taifa, JKT.

Simbu pia anamshukuru sana mkuu wa jeshi hilo pamoja na mkuu wa michezo wa jeshi hilo kwa kumpa ruhusa ya kufanya mazoezi kujiandaa na Marathon za Mumbai. Kushinda nchini India Simbu wiki iliyopita alishinda marathon za Mumbai baada ya kumaliza wa kwanza kwa kutumia saa 2:11:15.

Mwanariadha huyo katika mahojiano maalumu na mwandishi wa makala haya anasema kuwa mbio hizo zilikuwa ngumu, lakini maandalizi yake mazuri ndio yamemfanya kushinda.

Mipango ya baadaye Mwanariadha huyo baada ya kushinda Mumbai Marathon, amepata zawadi ya dola za Marekani 42,000 (ambayo ni zaidi ya Sh milioni 90).

Akizungumzia mipango yake ya baadaye, Simbu anasema kuwa baada ya kushinda kwa mara ya kwanza marathon, sasa anaangalia mashindano makubwa yajayo zikiwemo mbio za London Marathon.

London Marathon zitafanyika Aprili 23 pamoja na mashindano ya dunia ya riadha na mengine kibao.

Anasema huo ni mwanzo tu lakini amepania kufanya mambo makubwa zaidi katika mchezo huo na kamwe hatabweteka na mafanikio hayo ya sasa. Siri ya mafanikio yake Simbu anasema kuwa siri kubwa ya mafanikio yake ni juhudi kubwa katika mazoezi, kutokata tamaa na kutobweteka.

Anasema kuwa yeye ametokea katika maisha magumu sana, hivyo riadha ndio kazi yake, ambayo itamkomboa kutoka katika umaskini mkubwa huko kwao.

Anasema vijana wengi wamekuwa wakiangushwa na kubweteka mara wanapopata mafanikio kidogo, ambayo inamwezesha kupata fedha kidogo.

Anasema kuwa mafanikio hayapatikani bila ya kugangamala katika mchezo huo, lakini vijana wengi wanataka njia ya mkatano wakifanya mazoezi leo kesho washinde, “lakini riadha hiyo haiku hivyo.”

“Kwa kweli hakuna kitu kizuri kama kujiandaa vizuri, kwani maandalizi yale ya kila hali ndio yamenifanya kufanya vizuri na kuwashinda hata Wakenya na Waethiopia, “anasema Simbu katika mahojiano hayo.

Wadau wampongeza Simbu Wadau mbalimbali wamempongeza Simbu akiwemo Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Filbert Bayi anasema kuwa ushindi wa mwanariadha huyo ni salamu tosha kwa wale waliokuwa wakimbeza baada ya kushika nafasi ya tano katika Olimpiki ya Rio 2016.

Bayi anasema kuwa mwanariadha huyi kutokana na nidhamu aliyonayo hakuna ubishi kuwa ataendelea kufanya vizuri na siku moja kuandika historia ya aina yake katika riadha duniani.

“Ni salamu tosha kwa waliokuwa wakimbeza na hakuna ubishi kuwa Simbu ataendelea kufanya vizuri kwani ana nidhamu kubwa ya mchezo,” anasema. Mkurugenzi wa MultiChoice-Tanzania, Maharage Chande anasema kuwa, wataendelea kumdhamini Simbu ili kuhakikisha anaendelea kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali ya kimataifa.

ZeroDegree.
Simbu afunguka waliombeza Olimpiki Simbu afunguka waliombeza Olimpiki Reviewed by Zero Degree on 1/22/2017 01:59:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.