Loading...

Askofu Valentino Mokiwa ajibu tuhuma zinazomuandama

Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam, Dk Valentino Mokiwa
Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam, Dk Valentino Mokiwa amejibu tuhuma mbalimbali zikiwamo za wizi wa fedha zilizoelekezwa kwake, akidai ni uzushi wenye lengo la kumchafua ili aondolewe kwenye nafasi hiyo.

Mbali ya kujibu tuhuma hizo, Dk Mokiwa amedai mgogoro huo umezushwa kutokana na hofu ya uchaguzi wa askofu mkuu mpya mwakani na uongozi wa kutojiamini wa Askofu Mkuu, Dk Jacob Chimeledya.
Akizungumza na waandishi wa habari waliofika ofisini kwake kujua kiini cha mgogoro katika kanisa hilo ambao umesababisha Dk Chimeledya kumwandikia barua akimtaka ajiuzulu, Dk Mokiwa alisema mzozo uliopo katika kanisa hilo umetengenezwa na ‘wakubwa’ kwa kuwatumia mapadri wawili waliofukuzwa utumishi katika dayosisi ambao waliandaa mashtaka ili aonekane kuwa hafai na aondolewe.

“Ili niondoke, wakatengeneza mashtaka 10 wakitumia mapadri wawili ambao bahati mbaya nimewaondoa kwa utovu wa nidhamu,” alisema. “Kila shtaka lililotengenezwa dhidi yangu linafurahisha, linasikitisha, linachekesha kwa sababu malengo yake ni hatimaye Mokiwa aondolewe. Haya Askofu Mkuu wangu, Dk Chimeledya ameyaamini, ameyafanyia kazi, anaamini kabisa kwamba Mungu, Roho Mtakatifu amemtuma na huduma yake ya uaskofu mkuu itakuwa nzuri ikiwa mimi nitaondolewa kwa mashtaka hayo.”

Akijibu tuhuma moja baada ya nyingine kadri ilivyoandikwa katika mashtaka aliyopelekewa na Dk Chimeledya, Dk Mokiwa alisema: “Kuna shtaka eti nimezuia michango isiende jimboni. Hii ina sababu yake, kuna sheria katika katiba yetu inazuia dayosisi moja isivuke mipaka kwenda kufanya kazi katika dayosisi nyingine. Hapa kuna mwenzetu ametoka huko kwake anakuja kufungua makanisa hapa. Ni ukiukwaji wa katiba tu.”

Alitaja shtaka la pili kuwa ni madai ya kuitoa Dayosisi ya Dar es Salaam katika udhamini wa Kanisa la Anglikana Tanzania. Shtaka hilo linatokana na hoja ya dayosisi kutaka kutumia viwanja vyake katika uwekezaji na kwamba kiwepo kifungu cha kuwa na majadiliano katika uwekezaji huo.

“Hapa wanamaanisha kwamba nilitaka kujitenga niwe mwenyewe. Hata kama ningekuwa nimekula dawa fulani haiwezekani kwa sababu hii siyo taasisi yangu, kama ni kweli nataka kufanya hivyo basi nianzishe kanisa langu na mke wangu anifanye kuwa askofu,” alijibu.

Kuhusu ufujaji wa mali na kuingia mikataba mibovu, alisema havipo na kama ni mikataba iliamuliwa na sinodi na kamati ya dayosisi na kwamba, chombo hicho kina uwezo wa kurekebisha kama kuna makosa na tayari kimetengeneza kamati ya kupitia mikataba hiyo.

Ingawa mashtaka yalionyesha kuwa Dk Mokiwa alifuja mali za dayosisi, ushahidi wa nyaraka na taarifa za fedha za benki aliouweka wazi unaonyesha mapadri wawili walihusika katika akaunti zilizopo kwenye Benki ya Maendeleo, ACB (Benki ya Biashara ya Akiba) pamoja na DCB (Dar es Salaam Commercial Bank) iliyopanga katika jengo la dayosisi hiyo lililopo Magomeni.

Dk Mokiwa alisema kuna miamala inayoonyesha fedha zilikuwa zinaingizwa ACB tawi la Buguruni na kuna nakala za hundi zinazoonyesha fedha zikichotwa na kuingizwa kwenye akaunti binafsi za mapadri hao.

Alisema tangu aanze kazi kwenye dayosisi hiyo ameboresha taasisi alizozikuta na kuanzisha nyingine mpya ili kuinua mapato.

“Sipigi vita mafanikio, nataka maendeleo. Sijisifu ila kanisa hili nimelitoa kimasomaso. Sema tu nabii haheshimiki kwao,” alisema.

Dk Mokiwa alisema ushahidi kwamba mgogoro huo unapaliliwa na wakubwa ni baruapepe aliyodai kiongozi mmoja wa ngazi za juu alimwandikia mmoja wa mapadri waliofukuzwa Desemba 16, 2016 akimjulisha kuhusu tume iliyotumwa kumhoji Dk Mokiwa na kwamba timu nyingine inatumwa kwa ajili ya kazi hiyo.

Mwezi uliopita, Dk Chimeledya alisambaza waraka kwa makanisa ya Anglikana Dar es Salaam uliomtaka Dk Mokiwa kujiuzulu kutokana na tuhuma mbalimbali. Hata hivyo, askofu Mokiwa ameutaka uongozi wa Anglikana Taifa kufuata Katiba.

Source: Mwananchi
Askofu Valentino Mokiwa ajibu tuhuma zinazomuandama Askofu Valentino Mokiwa ajibu tuhuma zinazomuandama Reviewed by Zero Degree on 2/02/2017 12:17:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.