Loading...

Huu ndio mwonekano wa sasa wa Uwanja wa Maracana [Brazil] miezi 6 baada ya Olimpiki

UNAWEZA usiamini lakini ndivyo hali ilivyo hivi sasa katika Uwanja wa Maracana, nchini Brazil.

Miezi sita baada ya kumalizika kwa fainali za mashindano ya Olimpiki zilizofanyika kwenye Jiji la Rio de Janeiro, hali ya uchumi wa taifa la Brazil imeyumba na kupelekea baadhi ya mambo kuvurugika kwa kukosa huduma.



Na miongoni mwa mambo yaliyoathirika ni uwanja wa kihistoria wa taifa hilo unaotumika kwa ufunguzi na kufunga michezo mikubwa, dimba la Maracana.

Mpaka wakati huu Serikali ya Jiji la Rio na waandaaji wa michezo ya Olimpiki wanatupiana mipira juu ya nani wakulipa deni la umeme la zaidi ya pauni 800,000.



Ukubwa wa deni hili umepelekea Mamlaka ya umeme ndani ya Taifa la Brazil kukata umeme katika maeneo mengine, hali inayoleta kero kwa wananchi.

Janga hili si kwa Maracana tu, uwanja wa pili kwa ukubwa uliotumika kwa michezo ya Olimpiki, dimba la Deodoro, umefungwa mpaka Serikali itakapopata mdhamini wa kuuendesha.

Serikali ya Jiji la Rio de Janeiro pia imeshindwa kulipa mishahara ya walimu kwa wakati, wahudumu wa hospitali na huduma nyingine za kijamii huku ikiripotiwa kuongezeka kwa kasi kwa matukio ya kihalifu.

“Wakati wa michezo ya Olimpiki, viongozi walikuwa wakijitahidi mno kuweka mambo sawa,” alisema Oliver Stuenkel, raia wa Brazil anayefundisha chuo kikuu nchini humo. “Lakini punde tu baada ya Olimpiki kumalizika, kila kitu kimevurugika.”

Inatajwa kuwa michezo ya Olimpiki na matumizi mengine yaliyofanywa wakati wa fainali za Kombe la Dunia mwaka 2014, ndio yamelirudisha nyuma Jiji hilo linalosifika kwa starehe nyingi.

Baadhi ya majengo yaliyojengwa kwa ajili ya michezo hiyo mikubwa ya kidunia yamezua mijadala mikubwa miongoni mwa wanasiasa huku viongozi wa Serikali wakituhumiwa kwa rushwa.

Mpaka sasa viongozi watatu waliohusika na mpango wa ujenzi wa majengo hayo, Rais wa zamani, Luiz Inacio Lula da Silva, Gavana wa zamani wa Jiji la Rio, Sergio Cabral na Meya wa Jiji, Eduardo, wako kwenye uchunguzi huku baadhi ya waandaaji wengine wakifungwa jela baada ya kunaswa na hatia.

“Michezo ya Olimpiki ilitoa mwanga wa ugumu wa maisha ya Wabrazil,” alisema Stuenkel. “Huenda tusione kama hali ni mbaya, lakini mazingira ya kuishi hapa ni magumu mno kwa sasa.”
Huu ndio mwonekano wa sasa wa Uwanja wa Maracana [Brazil] miezi 6 baada ya Olimpiki Huu ndio mwonekano wa sasa wa Uwanja wa Maracana [Brazil] miezi 6 baada ya Olimpiki Reviewed by Zero Degree on 2/12/2017 04:55:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.