Loading...

Isipokuwa mtahiniwa mmoja katika darasa zima, wengine wote wapata 'ziro'

Uchache wa wanafunzi katika shule zenye wanafunzi chini ya 40, si kigezo pekee cha ufaulu baada ya baadhi zilizomo kwenye kundi hilo kufanya vibaya matokeo ya kidato cha nne yaliyotangazwa Jumanne na Baraza la Mitihani la Taifa (Necta).

Katika kundi hilo lenye jumla ya shule 1,439, Sekondari ya Dodeani Technical ya Kaskazini Pemba iliyokuwa na watahiniwa sita, ni mmoja tu aliyepata daraja la nne huku wengine wakipata sifuri.
Makoongwe ya Kusini Pemba iliyokuwa na watahiniwa 16 ni mmoja tu aliyepata daraja la nne na wengine wamepata sifuri.

Tangu Serikali ilipoanza kutenga matokeo katika makundi mawili, lenye wanafunzi zaidi ya 40 na chini ya 40 shule hizo zimekuwa hazitajwi sana.

Mbali ya Dodeani, Sekondari ya Mkotokuyana ya Lindi iliyokuwa na watahiniwa 21 ni wanne tu waliopata daraja la nne, huku wengine wakipata sifuri.

Nyingine ni Sekondari ya Sakami ya Dodoma iliyokuwa na watahiniwa 34 na kati yao ni sita tu waliopata daraja la nne. Sekondari ya Kweulasi ya mkoani Tanga iliyokuwa na watahiniwa 10 ni wawili tu walioambulia daraja la nne.

Zilizofanya vyema


Shule ya Sekondari ya Ahmes ya Pwani ndiyo kinara katika matokeo ya kidato cha nne kwa shule hizo zenye watahiniwa chini ya 40.

Ahmes ilikuwa na watahiniwa 29 ambao 23 walipata daraja la kwanza huku sita wakipata daraja la pili. Haikupata daraja la tatu, nne wala sifuri. Katika matokeo ya mwaka 2015, shule hiyo ilikuwa ya saba katika kundi hilo.

Shule ya pili ni seminari ya Mafinga, Iringa ambayo ilikuwa na watahiniwa 28, kati yao 26 wakiwa na daraja la kwanza, na wawili la pili. Mwaka 2015 ilikuwa imeshika nafasi ya sita.

Seminari ya Rubya ya Kagera ambayo ilikuwa na watahiniwa 26 ilishika nafasi ya tatu, kwa wanafunzi 22 kupata daraja la kwanza na wawili daraja la pili. Mwaka 2015, ilishika nafasi ya nne katika kundi hilo.

Shule zilizofuata ni Bethel Sabs Girls ya Iringa yenye watanihiwa 36 iliyoshika nafasi ya nne ikifuatiwa na Twibhoki ya Mara yenye watahiniwa 16, Musabe Boys ya Mwanza yenye watahiniwa 22 na Mugini ya Mwanza iliyokuwa na watahiniwa 15.

Sekondari ya Rising Star ya Dar es Salam iliyokuwa na watahiniwa 33 imeshika nafasi ya nane, ikifuatiwa na Seminari ya St Joseph Kilocha ya Njombe iliyokuwa na watahiniwa 38 na ya 10 ni St Marcus ya Mbeya iliyokuwa na watahiniwa 30.

Source: Mwananchi
Isipokuwa mtahiniwa mmoja katika darasa zima, wengine wote wapata 'ziro' Isipokuwa mtahiniwa mmoja katika darasa zima, wengine wote wapata 'ziro' Reviewed by Zero Degree on 2/03/2017 11:30:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.