Loading...

Kinachowafanya watu wengi kukimbilia kwenye tiba asilia

Daktari wa tiba asilia, Longino Kente (kushoto), akiwaonyesha washiriki wa mafunzo ya tiba asili mti wa mlongelonge ambao unatibu magonjwa 240.
Ongezeko la magonjwa, imani, uhaba wa dawa, kukwepa gharama za matibabu ya hospitali na propaganda zinazofanywa kupitia kwenye matangazo, vinadaiwa kuwa chanzo cha watu wengi kuvutiwa na kukimbilia tiba za asili.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), tiba asili inatoa huduma kwa asilimia 80 ya wanaohitaji huduma za afya katika nchi zinazoendelea.

Hapa nchini, inakisiwa kuwa asilimia 60 ya Watanzania wanatumia tiba asilia katika kutibu magonjwa yao na kwamba kila kijiji kina watoa huduma wa tiba asilia.

Pia, takwimu kutoka Wizara ya Afya zinaonyesha kuwa takriban asilimia 60 ya wananchi huanza kutumia tiba asilia wanapopatwa na maradhi kabla ya kwenda kwenye vituo vya afya.

Mtaalamu wa tiba asilia kutoka taasisi ya Pharm Mazua, Ally Mazu alisema tiba asilia ilianza kuaminiwa tangu enzi za mababu na kwamba wengi wanaendelea kuitumia, hasa katika magonjwa sugu yaliyokuwa yakiiandama jamii.

Alisema hadi sasa watu wengi wanakabiliwa na magonjwa sugu yakiwamo ya kurithi, ambayo si rahisi kutibiwa hospitalini kama ilivyo kwa magonjwa ya kuambukiza.

“Mfano, mama mwenye tatizo la hedhi akienda hospitali atapewa dawa ya kupunguza maumivu tu, lakini huku kwenye tiba asilia zipo dawa zitakazomponya kabisa kutokana na imani ya mgonjwa. Imani ndiyo ambayo huwafanya watu wengi waje kwenye tiba asilia,” alisema Mazu.

Hata hivyo, aliishauri Serikali kuweka vitengo maalumu vya kutoa huduma za masuala ya lishe katika hospitali kwa madai kuwa magonjwa mengi yanayoiandama jamii hivi sasa yanatokana na lishe duni.

Alisema licha ya kuwa matangazo ya tiba hizo huwa yanashawishi zaidi, bado wengi huchagua tiba asilia kutokana na urahisi wake katika kuipata sambamba na gharama nafuu ikilinganishwa na tiba ya kisasa hospitali. “Imani ya mitishamba ni kubwa kwenye jamii, hiyo ndiyo inachangia watoa huduma wa tiba asilia kupokea watu wengi zaidi wanaohitaji matibabu,” alisema Mazu.

Wauzaji wa dawa za mitishamba za kimasai, katika eneo la Ubungo walisema hupata wateja wengi hasa wanaohitaji tiba ya magonjwa ya asili.

Muuzaji Solomini Meng’anataki alisema kwa siku hupata kati ya wateja 10 hadi 20 wanaohitaji dawa za kuongeza nguvu za kiume, shinikizo la damu, pumu, figo na vidonda vya tumbo.

“Dawa zangu zinatokana na miti ya porini na nashukuru kila siku ninapata wateja wengi,” alisema.

Mtaalamu wa masuala ya asili na utalii katika Chuo Kikuu cha Iringa (UoI), Jimson Sanga alisema kiasili Waafrika hawakuwa wakitumia dawa za kisasa katika kutibu magonjwa mbalimbali yaliyokuwa yakijitokeza kwenye jamii.

Alisema asili hiyo haiwezi kufutika kiurahisi na ndiyo maana bado watu wengi hupendelea kupata tiba ya asilia.

Alisema imani iliyojengeka tangu enzi za mababu kuwa dawa za asili zina nguvu kubwa ya kuponya maradhi mengi, bado inafanya kazi kubwa na hiyo ndiyo sababu iliyoifanya Serikali kukubali na kutunga Sera ya Tiba Asilia.

“Kila mtu ana asili na asili huanzia kwenye koo kwa hiyo ni rahisi watu kuendelea kutunza asili zao na ndiyo maana imani ya dawa za asili haiwezi kufutika kamwe, bado tunaishi kwenye koo na makabila na huko ndiko liliko chimbuko la asili la dawa hizi,” alisema.

Alisema kwa asili Waafrika wanazo mila zao na desturi ambazo huwa zinawaongoza katika kutekeleza masuala mbalimbali yakiwamo ya tiba.

Alishauri zifanyike tafiti za kujua dawa zinazotumika kutibu magonjwa hasa ya asili, ikibainika ukweli wa tiba hizo ziweze kutumiwa hospitalini.

“Mfano, pumu katika hospitali inasemwa kuwa hakuna tiba yake zaidi ya ile ya kutuliza, lakini mtaani unasikia kuna mtu anatibu pumu na pia kuna watu wengi katika maeneo tofauti ambao wanatibu magonjwa mbalimbali, lakini mwendelezo hakuna kwa kuwa hakuna mafungu ya utafiti,” alisema Sanga.

Mtaalamu wa Dawa na Tiba wa Hospitali ya Sanitas, Dk Sajjad Fazel alisema watu wa tiba asilia wanajitangaza zaidi ndiyo maana watu wengi wamekuwa wakivutiwa na kwenda kutibiwa.

“Mgonjwa anapoumwa huhitaji matokeo ya haraka, sasa akishaambiwa atapona ni wazi kwamba atakimbilia huko, wenzetu wa tiba asilia wanajitangaza sana,” alisema.

Dk Sajjad alisema ukweli utabaki palepale kwamba ili mgonjwa apate tiba sahihi ni lazima apate vipimo vya uhakika vya maabara vitakavyosaidia kujulikana kwa ugonjwa wake.

Alisema vinginevyo, mgonjwa anaweza kupata tiba isiyo sahihi na kupoteza maisha yake. “Mara nyingi huwa tunapokea wagonjwa wakiwa kwenye hatua za mwisho, hata kama watatumia miti shamba basi iwe ni kwa ajili ya magonjwa yanayowasumbua baada ya vipimo kubainisha. Vinginevyo bado ni hatari. Kumpa mtu dawa bila kupima si sawa.”

Alisema yaliyotokea kwa Babu wa Loliondo hayakuwa sawa kwa sababu watu walikunywa dawa ya aina moja wakiamini itatibu magonjwa yote jambo ambalo kitaalamu haliwezekani.

“Huwezi kutibu magonjwa mengi kwa dawa moja, hili halipo sawa,” alisema.

Imani inavyoponya


Dk Sajjad anasema imani inaweza kumponya mtu hata kama dawa atakayotumia haiwezi kutibu ugonjwa husika.

“Ndiyo maana ninapowatibu wagonjwa huwa nawaambia wazi, waamini kama dawa hizo zinaponya. Imani tu ukiwa nayo inasaidia kuongeza baadhi ya virutubisho kwenye mwili wako. Ikiwa mtu ana imani na dawa husika, uhakika wa kupona huwa ni mkubwa zaidi,” alisema.

Wagonjwa wasimulia
Baadhi ya wagonjwa wanaopata matibabu kwenye tiba asilia walisema imani waliyonayo kwenye tiba hiyo ndiyo iliyowasukuma kuitumia.

Mgonjwa Pelonimo Aron, mkazi wa Ubungo alisema anatumia dawa za asili zinazouzwa na wamasai, kujitibu maradhi ya figo yanayomsumbua baada ya kukosa fedha za matibabu.

“Nina tatizo la figo, siwezi kutibiwa hospitali kwa sababu gharama yake ni kubwa, nimeamua kutumia mitishamba na ninaamini nitapona,” alisema.
Msimamo wa Serikali kuhusu Tiba Asili
Katika tamko la Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Ummy Mwalimu alilolitoa mwishoni mwa mwaka jana wakati wa uzinduzi wa fomu ya usajili wa dawa za tiba asilia nchini, Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala lililoanzishwa kisheria nchini limesajili waganga zaidi ya 14,000 na vituo 180 vya tiba asilia.

Kwa mujibu wa tamko hilo, Serikali inatambua umuhimu wa tiba asilia kutokana na ukongwe wake na Serikali imerasimisha tiba asilia kwa kujumuisha na tiba mbadala kwenye Sera ya Afya pamoja na kuitungia sheria.



Source: Mwananchi
Kinachowafanya watu wengi kukimbilia kwenye tiba asilia Kinachowafanya watu wengi kukimbilia kwenye tiba asilia Reviewed by Zero Degree on 2/27/2017 01:01:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.