Mahakama kuu ya Tanzania yatoa zuio la muda kwa jeshi la polisi kumkamata Mbowe.
Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo [CHADEMA], Mh. Freeman Mbowe |
Mbowe alifungua maombi hayo ya kutokamatwa akipinga kusudio la kamanda Sirro la kumkamata kama hatajisalimisha katika kituo kikuu cha polisi kwa ajili ya mahojiano.
Katika maombi hayo, Mbowe anaiomba mahakama iwazuie wadaiwa kutekeleza azma yake ya kumtia mbaroni pamoja na mambo mengine akidai kuwa kuna kesi ya kikatiba ambayo tayari ameifungua mahakani hapo, hivyo anaiomba mahakama itoe amri ya kuwazuia kumkamata hadi hapo kesi hiyo ya kikatiba itakapomalizika.
Hatua ya Mbowe kufungua maombi hayo inatokana na kauli ya Sirro aliyoitoa februari 18, mwaka huu kwamba anamtaka kiongozi huyo wa upinzani ajisalimishe mwenyewe kituo cha polisi kama hajafanya hivyo basi watamsaka popote alipo na kumtia mbaroni.
Katika mahakama hiyo viongozi wakiwemo wabunge wa chama hicho na wafuasi wa CHADEMA walifika kwa ajili ya kufuatilia mwenendo wa kesi hiyo.
Uamuzi huo umetolewa na jopo la majaji watatu wakiongozwa na Sekieti Kihiyo ambaye ni kiongozi wa jopo hilo,baada ya wakili wa serikali kuieleza mahakama kuwa kesi hiyo imeitishwa kwa ajili ya kutajwa, hata hivyo mahakama hiyo imesema jeshi hilo lina uwezo wa kumuita na kumuhoji Mbowe kama litahitaji katika kipindi cha sasa.
Kutokana na hatua hiyo, jaji Kihiyo alisema kuwa mahakama hiyo inatarajia kuyasikiliza maombi ya Mbowe kama akamatwe na jeshi la polisi au la februari 23, mwaka huu.
Akitolea ufafanuzi baadhi ya mambo juu ya kesi ya msingi namba 1 ya mwaka 2017, ambayo Mbowe aliifungua mahakamani hapo dhidi ya kamanda Saimon Sirro, Paul Makonda na Camilius Wambura ambayo pamoja na mambo mengine anapinga mamlaka ya RC kumtaka afike katika kituo kikuu cha polisi, Dar es Salaam, kwa ajili ya mahojiano na kile anachokiita kudhalilisha watu.
Source: ITV
Mahakama kuu ya Tanzania yatoa zuio la muda kwa jeshi la polisi kumkamata Mbowe.
Reviewed by Zero Degree
on
2/22/2017 03:05:00 PM
Rating: