Loading...

Marufuku waendesha bodaboda kufanya kazi baada ya muda huu

KATIKA kile kinachoelezwa kuwa ni jitihada za kupambana na uhalifu Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, imepiga marufuku waendesha bodaboda kufanya kazi hiyo baada ya saa sita usiku kuanzia sasa.

Amri hiyo ilitolewa jana na Kamanda wa kanda hiyo Simon Sirro, alipozungumza na waandishi wa habari na kusisitiza kuwa baada ya muda huo hakuna pikipiki inayoruhusiwa kuonekana katika vituo ikisubiri abiria.

Alisema kumekuwa na wimbi la uporaji wa pikipiki maeneo tofauti jijini huku Kinyerezi , Kigamboni na Chanika Mwisho zikitajwa kukithiri kwa uhalifu huo.

Aidha, alisema ili kukabiliana na wimbi hilo la wizi, waendesha bodaboda wanatakiwa kufanya shughuli zao mwisho saa sita usiku badala ya kukaa vijiweni hadi asubuhi.

“Haiwezekani baa zifungwe saa sita halafu hawa wakashinda na kulala vijiweni hadi alfajiri, wanafanya nini? Ndiyo maana wanaibiwa pikipiki na wengine kutekwa,”alisema.

Katika hatua nyingine, jeshi hilo limetoa rai kwa mahakama kuangalia uwezekano wa kuwahukumu kwenda jela washtakiwa wanaofanya makosa ya kupita kwenye mradi wa mabasi yaendayo haraka (BRT) kinyume cha sheria.

“Takribani pikipiki 1,280 zilizokamatwa kati yao madereva 30 walipita kwenye barabara ya BRT ya Morogoro, tunawashikilia madereva 27 na wengine watatu walikimbia na kutelekeza pikipiki ,” alisema.
Marufuku waendesha bodaboda kufanya kazi baada ya muda huu Marufuku waendesha bodaboda kufanya kazi baada ya muda huu Reviewed by Zero Degree on 2/25/2017 11:01:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.