Loading...

Askari wawili mbaroni wakituhumiwa kujihusisha na wizi wa mafuta ya ndege

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu, Simon Sirro
JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linawashikilia askari wawili wa Kikosi cha Anga pamoja na mlinzi wa Kampuni ya Ulinzi ya Moku kwa tuhuma za kujihusisha na wizi wa mafuta ya ndege.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu, Simon Sirro alisema tukio hilo lilitokea Machi 17, mwaka huu kwenye hanga la Kampuni ya Ndege ya Tanzania (ATCL) kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius (JNIA).

Kamanda Sirro alisema Polisi kwa kushirikiana na maofisa wa usalama uwanjani hapo, walimkamata Iddy Nyangasa (42) mkazi wa Vingunguti kwa Mnyamani ambaye ni mlinzi wa Moku baada ya kuiba lita 38 za mafuta ya ndege kutoka kwenye ndege yenye namba za usajili 5H-MWF aina ya DASH 8-Q 300 mali ya ATCL iliyokuwa kwenye hanga hilo kwa ajili ya matengenezo.

Aliongeza kuwa baada ya ukaguzi wa kina na wahandisi wa ATCL, ilibainika jumla ya lita 220 ndizo zilizoibwa kutoka ndege hiyo.

Sirro alisema baada ya tukio hilo, uchunguzi wa kina ulifanyika na kubaini mtandao huo wa wizi wa mafuta ya ndege pia unahusisha askari polisi wa Kikosi cha Anga ambao ni Koplo Bahati Msilimini na Konstebo Benaus Mkama.

Alisema askari hao wamekamatwa kwa uchunguzi zaidi na mara tu uchunguzi utakapokamilika, watuhumiwa wote watafikishwa kwenye vyombo vya sheria.

“Wizi wa mafuta kwenye ndege ni hatari sana kwani unaweza kusababisha janga kubwa kama moto au ajali kwa ndege kukosa mafuta. Imebainika kuwa katika jamii zetu mafuta haya yamekuwa yakiuzwa kama mafuta ya taa,” alisema Kamanda Sirro.

Alitoa rai kwa wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam na maeneo mengine ya nchi wasijihusishe na ununuzi wa mafuta wa aina hii, kwani watakapokutwa nayo watachukuliwa kama washiriki wa makosa haya.

Pia aliwaomba kutoa taarifa polisi mara wanapoona mafuta hayo yakiuzwa mitaani ili kuepusha madhara yanayoweza kutokea.
Askari wawili mbaroni wakituhumiwa kujihusisha na wizi wa mafuta ya ndege Askari wawili mbaroni wakituhumiwa kujihusisha na wizi wa mafuta ya ndege Reviewed by Zero Degree on 3/23/2017 05:55:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.