Loading...

Bidhaa bandia zenye thamani ya milioni 800/= zateketezwa jijini Dar

Tingatinga likiharibu bidhaa bandia zenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 800 zikiwamo wino bandia wa printa katika dampo la Pugu Kinyamwezi, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam jana.
KATIKA kuhakikisha inawalinda walaji, Tume ya Ushindani nchini (FCC) imeteketeza bidhaa mbalimbali bandia ikiwemo wino wa printa zenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 800.

Uteketezaji wa bidhaa hizo umefanyika jana kuanzia asubuhi katika dampo la Pugu Kinyamwezi, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa kuteketeza bidhaa hizo, Ofisa Mwandamizi wa Mawasiliano na mahusiano ya Umma wa FCC, Frank Mdimi alisema, bidhaa hizo zilikamatwa katika operesheni mbalimbali za kuondoa bidhaa bandia sokoni.

Alisema walipokea malalamiko kutoka kwa watu mbalimbali kuhusu tona bandia za printa hatua ambayo ilisababisha kubainika kwa bidhaa hizo kupitia opereheni mbalimbali ambazo hufanyika mara kwa mara.

“Bidhaa hizi zilikamatwa katika mazoezi mbalimbali jijini Dar es Salaam, kwa kiasi kikubwa bidhaa hizi zinahusisha vifaa vya tona za printa maofisi ambazo zimekuwa zikisababisha hasara pamoja na kuharibu mashine zao,” alisema Mdimi.

Alisema bidhaa hizo zinakadiriwa kuwa na uzito wa tani 24 na thamani ya Sh 854,400,000.

Alitaja baadhi ya bidhaa zilizoteketezwa ni pamoja na makasha matupu ya kufungia tona za printa, makasha ya wino, visikilizio vya simu mbalimbali pamoja na bidhaa nyingine.

Kufuatia tukio hilo, Mdimi amewataka wafanyabiashara na wananchi kwa jumla, kujiepusha na ununuzi holela wa bidhaa kwani kufanya hivyo kunawaweka katika hatari ya kununua zilizoghushiwa kinyume cha sheria za nchi.

Alisema kumekuwa na matatizo kwa baadhi ya watu wanaoenda kutoa malalamiko kuwa na risti ambayo imeandikwa kituo tofauti na alichonunua, hivyo kupata wakati mgumu wa kuwasaidia.

“Naomba niwaambie wafanyabiashara na wananchi wote kwa ujumla vita ya bidhaa bandia inaimarishwa, hatua dhidi ya wale watakaokutwa na bidhaa bandia zitachukuliwa,” alisema.

Kwa mujibu wa Sheria, adhabu ya mtu anayeuza bidhaa bandia ni kutozwa faini, kupokonywa bidhaa husika na kugharamia uteketezaji wa bidhaa hizo.
Bidhaa bandia zenye thamani ya milioni 800/= zateketezwa jijini Dar Bidhaa bandia zenye thamani ya milioni 800/= zateketezwa jijini Dar Reviewed by Zero Degree on 3/20/2017 11:06:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.