Loading...

Bunge la Marekani kufanya uchunguzi juu ya tuhuma za Rais Donald Trump dhidi ya Obama

MWENYEKITI wa Kamati Teule ya Bunge ya Ujasusi anayetoka Chama cha Republican, Devin Nunes, amesema kamati yake itayashughulikia madai ya Rais Donald Trump, hasa baada ya Ikulu kuliomba Bunge kuyachunguza.

Awali Mkurugenzi wa Shirika la Upelelezi Marekani (FBI), James Comey, aliitaka Idara ya Uchunguzi kuyakana hadharani madai hayo kuwa rais aliyemaliza muda wake, Barack Obama, alidukua mawasiliano yake ya simu kabla ya uchaguzi mkuu mwaka uliopita.

Likiwanukuu maofisa wakuu wa Marekani, gazeti la New York Times la hapa limeripoti kuwa Comey anaamini madai ya Trump dhidi ya Obama hayana msingi wowote na ni ya uongo.

Hadi sasa FBI haijatoa tamko rasmi kuhusu madai ya Trump.

Kulingana na gazeti hilo, Comey alitoa ombi hilo kwa sababu hakuna ushahidi wa kuyathibitisha madai hayo.

Akihojiwa na runinga ya NBC, Mkurugenzi wa Idara ya Ujasusi nchini Marekani, James Clapper aliyesimamia mambo ya ujasusi wakati Obama alipokuwa madarakani, amekanusha kudukuliwa kwa mawasiliano ya simu ya Trump.

Alisema hakukuwako agizo la mahakama ambalo lingeruhusu jambo kama hilo kufanyika.

“Ninafikiria ni kwa manufaa ya kila mmoja, manufaa ya rais wa sasa, manufaa kwa Wademocratic, Warepublican na kwa manufaa ya taifa uchunguzi wa kina ufanywe dhidi ya madai haya.

“Ni kwa vile yanakanganya, na labda Warusi wanafurahia juhudi zao zinapozua mgawanyiko humu nchini,” alisema.

Trump alikuwa amewasilisha madai yake kupitia ukurasa wake wa twitter siku ya Jumamosi bila ya uthibitisho akiishia kusema ‘ni hali ya kusikitisha kuwa Rais Obama alinasa mawasiliano yangu ya simu wakati wa uchaguzi.’

Obama kupitia msemaji wake alikanusha madai hayo.

Madai hayo yamezua cheche za ukosoaji, huku wengi wakisema lengo la Trump ni kuyabadilisha mawazo ya watu dhidi ya mlolongo wa ufichuzi kuhusu mikutano au uhusiano wa washirika wake na Urusi.
Bunge la Marekani kufanya uchunguzi juu ya tuhuma za Rais Donald Trump dhidi ya Obama Bunge la Marekani kufanya uchunguzi juu ya tuhuma za Rais Donald Trump dhidi ya Obama Reviewed by Zero Degree on 3/07/2017 12:10:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.