Loading...

Hizi hapa wizara zilizokamilisha mchakato wa kuhamia Dodoma

AWAMU ya kwanza ya serikali kuhamia Dodoma imehitimishwa jana wakati wizara 16 kati ya 19 tayari zimehamishia ofisi zake katika Makao Makuu ya Serikali.

Serikali ilitangaza Februari 28, mwaka huu kuwa mwisho wa awamu ya kwanza kuhamia makao makuu Dodoma, yaliyotangazwa mwaka 1973, lakini yakapata msukumo wa Rais John Magufuli mwaka jana alipotangaza kuwa ifikapo mwisho wa muhula wake wa kwanza wa uongozi, serikali yake yote itakuwa imehamia Dodoma.

Miongoni mwa wizara ambazo tayari ziko Dodoma ni Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki; Maji na Umwagiliaji; Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Fedha na Mipango; Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo; Katiba na Sheria; Nishati na Madini na Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Nyingine ni Kilimo, Mifugo na Uvuvi; Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Maliasili na Utalii, Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Mambo ya Ndani ya Nchi, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

Wizara ambazo taarifa zake za kuhamia Dodoma hazijapatikana ni Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na Muungano na Mazingira.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari jana, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dk Augustine Mahiga alisema alisema wizara yake imeshahamia Dodoma tangu Februari 17, mwaka huu na kuhusisha awamu mbili; ya kwanza imetekelezwa Januari 28 na awamu ya pili Februari 17, mwaka huu.

Balozi Mahiga alisema katika uhamisho wa mara ya kwanza jumla ya watumishi 43 walihamia Dodoma; wakati wafanyakazi wa wizara hiyo kwa jumla yake ni 355 wakiwemo wale wanaofanya kazi kwenye balozi zilizo nje ya nchi.

Alisema mpaka sasa kuna balozi zaidi ya 50 na kila ubalozi una wastani wa watumishi katika ya 15 na 30. Aidha, alisema wiki ijayo atakuwa na kikao na mabalozi wote na kuwatangazia rasmi uamuzi wa wizara hiyo kuhamia Dodoma.

“Nataka niwaeleze na tujue mipango yao kuna balozi zimeonesha dhamira ya kuhamia Dodoma nataka kusikiliza pia kutoka kwao lazima tuwaeleze wakija Dodoma watoto wao watasoma wapi, wakiumwa watatibiwa hospitali gani na hata wajue hospitali zetu zina viwango gani,” alibainisha Balozi Mahiga.

Alisema miongoni mwa ubalozi ulioonesha dhamira ya kuhamia Dodoma ni Ubalozi wa Brazil.

“Tunataka tupate pia uzoefu wa mabalozi ambapo kwenye nchi zao makao makuu ya nchi yalihamishwa ili tupate uzoefu wao na kuweza kubadilishana nao mawazo,” alifafanua. Nigeria ni miongoni mwa nchi zilizobadili makao makuu yao.

Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Gerson Lwenge alisema awamu ya kwanza ya watumishi kuhamia Dodoma imekamilika na shughuli zote za wizara kuanzia sasa zitafanyika mkoani Dodoma.

Lwenge alisema watumishi waliohamia ni Idara ya Utawala, Kitengo cha Mipango na Sera, Kurugenzi ya Maji Mijini, Kurugenzi ya Maji Vijijini, Kitengo cha Uratibu wa Programu, Ofisi ya Mwanasheria, Tehama, Uhasibu, Raslimali za Maji, Ubora wa Maji, Ukaguzi wa Ndani na Kitengo cha Habari.

Alisema watumishi wa wizara hiyo watahamia kwa awamu nne; ya kwanza watumishi 102, ya pili watumishi 99, ya tatu watumishi 100 na ya nne watumishi 121.

“Safari ya wizara kuhamia Dodoma imekamilika na kuanzia leo (jana) kazi zote za wizara zitafanyika kutoka Dodoma na tunafanya utaratibu wa kuwa na jengo letu la kudumu ili watumishi wote wakae pamoja tofauti na sasa ambapo watumishi watafanya kazi katika ofisi tofauti,” alibainisha Lwenge.

Wizara ya Maliasili na Utalii ilisema katika taarifa yake jana kwamba watumishi 52 wakiongozwa na Waziri Profesa Jumanne Maghembe, Naibu Waziri Ramo Makani, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu imeshamia rasmi Dodoma kuanzia jana na ofisi zake zitakuwa Mtaa wa Kilimani (Barabara ya Askari) na Chuo Kikuu cha Dodoma, Kitivo cha Sayansi ya Jamii “Block 12.”

Hivi karibuni, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama alisema Ofisi ya Waziri Mkuu ilishatoa mwongozo wa lini mawaziri, manaibu, makatibu wakuu na manaibu wao wanatakiwa kuwa Dodoma.

Alisema mwisho wa viongozi hao na watumishi kuhamia Dodoma ni leo Februari 28. Septemba 30, mwaka jana, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliandika historia mpya baada ya kuhamia rasmi mjini Dodoma; na kutangaza kuwa watakaomfuata ni mawaziri wote manaibu na makatibu wakuu mpaka Februari wote watakuwa Dodoma na Rais Magufuli alisema asiyehamia atakuwa amejiondoa kazini.

Akihitimisha Mkutano wa Nne wa Bunge la 11, Majaliwa alisema serikali itahamia Dodoma kwa awamu sita; ya kwanza itakuwa Septemba 2016 hadi Februari 2017 ikiwahusisha makatibu wakuu, naibu makatibu na walau idara mbili za kila wizara. Awamu ya sita ni Machi 2020 hadi Juni 2020 ambayo Rais na ofisi yake watahamia Dodoma.
Hizi hapa wizara zilizokamilisha mchakato wa kuhamia Dodoma Hizi hapa wizara zilizokamilisha mchakato wa kuhamia Dodoma Reviewed by Zero Degree on 3/01/2017 09:37:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.