Loading...

Hizi ndizo sababu zilizomfanya Rais Magufuli ampe Kenyatta madaktari toka Tanzania

Rais John Magufuli akiwa katika mazungumzo na ujumbe kutoka Kenya ukiongozwa na Waziri wa Afya wa nchi hiyo, Dk Cleopa Mailu Ikulu Dar es Salaam jana.
WAKATI Tanzania imekubali ombi la kuipatia Kenya madaktari 500 watakaoisaidia nchi hiyo kukabiliana na tatizo la uhaba wa madaktari katika vituo vyake vya tiba; hasa baada ya kutokea kwa mgomo wa madaktari nchini humo, gazeti hili limefanya uchambuzi kubaini mazingira ya sekta ya afya baina ya nchi hizo mbili.

Uchambuzi uliofanywa umezingatia data mbalimbali za afya baina ya nchi hizo mbili, zinazobainisha Tanzania kuwa na mazingira yanayoboreka zaidi katika sekta ya afya ukilinganisha na Kenya.

Kutokana na uchambuzi huo, gazeti hili limebaini kuwa hatua ya serikali kukubali kutoa madaktari 500 kwenda kufanya kazi nchini Kenya itainufaisha zaidi Tanzania kupitia Itifaki ya Soko la Pamoja inayotoa mwanya pamoja na mambo mengine wananchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kufanya kazi mahali popote ndani ya jumuiya hiyo kwa kuzingatia sifa.

Data zilizofanyiwa uchambuzi ni zile zilizopo kwenye tovuti za Shirika la Afya Duniani (WHO), tovuti za wizara zinazosimamia sekta ya afya kwa nchi zote mbili na tovuti ya kuonesha uwazi wa uendeshaji wa shughuli za serikali kwa uwazi (www.opendata.go.tz) na ule wa nchini Kenya, ambapo matokeo ya ujumla yanaonesha Tanzania kuwa na mazingira bora zaidi ukilinganisha na Kenya.

Rais Magufuli Jana katika Ikulu ya jijini Dar es Salaam Rais John Magufuli alikubali kutoa madaktari hao, baada ya kufanya mazungumzo na ujumbe wa viongozi wa Wizara ya Afya ya Kenya uliotumwa na Rais wa nchi hiyo, Kenyatta.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu, kiongozi wa ujumbe huo ambaye ni Waziri wa Afya wa Kenya Dk Cleopa Mailu alimueleza Rais Magufuli kuwa baada ya kutokea mgomo wa madaktari pamoja na uamuzi wa nchi hiyo kugatua madaraka katika sekta ya afya, imebainika kuwa nchi hiyo ina upungufu mkubwa wa madaktari ambao hauwezi kumalizwa kwa kutegemea madaktari wanaosomeshwa nchini humo bali kupata madaktari kutoka nje ya nchi.

Dk Mailu aliyeongozana na Gavana wa Kisumu Jack Ranguma alisema Kenya ipo tayari kuwalipa stahili zote madaktari 500 kutoka Tanzania ikiwa ni pamoja na mishahara na nyumba za kuishi.

Kauli ya Waziri Ummy Naye Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu alisema Wizara yake ipo tayari kutoa madaktari hao haraka iwezekanavyo kwa kuwa Tanzania inao madaktari wengi wazuri ambao wamemaliza masomo yao na hawajapata ajira, na wengine wamemaliza mikataba yao ya kazi na bado wana uwezo wa kufanya kazi.

“Kwa hiyo nitoe wito kwa madaktari wote Tanzania ambao hawapo katika utumishi wa umma, hawapo katika hospitali teule na ambao hawapo katika hospitali za mashirika yasiyo ya kiserikali wanaolipwa na Serikali, waombe nafasi hizi. “Vigezo vikubwa ambavyo tutaviangalia ni kwanza awe amemaliza mafunzo ya vitendo na pili awe amesajiliwa na Baraza la Madaktari la Tanganyika, kwa hiyo leo hii tutatoa tangazo na tumefurahi sana kwa sababu tunao madaktari wa kutosha ndani ya nchi na tunaweza kuwapeleka Kenya,” alisema Ummy.

Kwa upande wake Rais Magufuli alisema Tanzania imekubali ombi hilo kwa kuwa Kenya ni ndugu, jirani na rafiki wa kweli wa Tanzania na alimtaka Waziri Ummy kuharakisha mchakato wa kuwapata madaktari hao ili wawahi kwenda Kenya kutekeleza jukumu hilo.

“Matatizo ya Kenya ni matatizo ya Tanzania, tutawapatia madaktari hao 500 ili wakatoe huduma ya matibabu kwa ndugu zetu waliopo Kenya, na kwa kuwa mmenihakikishia kuwa madaktari wangu mtawalipa mishahara inavyotakiwa, mtawapa nyumba za kuishi, na mtahakikisha wanafanya kazi katika mazingira mazuri na salama mimi sina tatizo na naamini mambo yatakwenda vizuri,” alisema Rais Magufuli.

Wizara yatoa tangazo Katika kuonesha uharaka katika utekelezaji wa agizo hilo la Rais Magufuli, Wizara ya Afya baadaye mchana jana ilitoa tangazo la nafasi hizo za kazi kwa madaktari watakaokuwa tayari kwenda nchini Kenya.

Tangazo hilo lililosainiwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dk Mpoki Ulisubisya ilieleza taratibu za uombaji wa nafasi hizo za wakazi ambapo waombaji watalazimika kuambatanisha nyaraka mbalimbali.

Miongoni mwa nyaraka hizo ni wasifu (cv), nakala ya vyeti vya kitaaluma, nakala ya cheti cha kuzaliwa, cheti cha matokeo ya mitihani, cheti cha kuhitimu mafunzo ya udaktari kwa vitendo, nakala ya cheti cha usajili katika Baraza la Madaktari la Tanganyika.

Mahitaji ya madaktari Hadi ilipofika Desemba 31,2015, wakati Tanzania ilikuwa na mahitaji ya madaktari 75,000 ili kumaliza tatizo, huku Kenya ikihitaji madaktari 83,000 ili kumaliza tatizo hilo.

Aidha data za Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto za Desemba mwaka jana zinaonesha kuwa uzalishaji wa madaktari kwa ripoti ya mwaka 2015, umefikia madaktari 1,000 kwa mwaka wakati ripoti ya kipindi kama hicho uliyotolewa na Wizara ya Afya ya Kenya inaonesha nchi hiyo kuzalisha madaktari 600 tu kwa mwaka.

Uwiano wa daktari kwa wagonjwa mijini HabariLeo Jumapili pia ilitupia macho, data zinazoonesha mahitaji ya madaktari baina ya nchi hizo mbili kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa na WHO, vinavyotaka daktari mmoja kuhudumia wagonjwa 1,000 (1:1,000) Katika eneo hilo gazeti hili lilibaini kuwa hadi mwishoni mwaka mwaka 2015, kwa maeneo ya mijini wakati uwiano kwa Tanzania ni daktari mmoja kwa wagonjwa 9,095, Kenya ilikuwa ni daktari mmoja kwa wagonjwa 17,000.

Kutokana na takwimu hizo ni wazi kuwa Tanzania imefanya vizuri zaidi katika miaka ya hivi karibuni katika kuongeza idadi ya madaktari mijini ukilinganisha na Kenya.

Madaktari utumishi wa umma Eneo lingine linaloonesha Tanzania kuendelea kufanya vizuri katika uboreshaji wa sekta ya afya ni takwimu kuhusu ongezeko la madaktari katika utumishi wa umma.

Wakati katika bajeti ya mwaka wa fedha unaokaribia kumalizika Tanzania ilitoa vibali vya kuajiri watumishi wa umma wakiwemo madaktari zaidi ya 10,000, hali ilikuwa ni tofauti kwa Kenya ambapo hakukuwa na ongezeko badala yake katika kipindi cha miaka miwili nchi hiyo imejikuta katika matatizo baada ya madaktari zaidi ya 2,000 kuacha kazi wengi wao wakiwa ni katika utumishi wa umma Katika kuonesha kuwa Tanzania ilikuwa na idadi kubwa ya madaktari wasio na ajira pamoja na kuwa na sifa, Makamu Mkuu wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) Dk Obadia Nyongela anasema hadi mwishoni mwa mwaka jana kulikuwa na madaktari 1,700 mitaani wasio na ajira pamoja na kuwa na sifa.

Dk Nyongela alisema endapo serikali isingetoa vibali vya kuwajiri madaktari hao hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu, basi Tanzania ingejikuta kuwa na madaktari wenye sifa lakini hawana ajira zaidi ya 2,800.

Data hizo zinatoa tafsiri ya wazi kuwa kumekuwa na ongezeko kubwa la madaktari nchini kuliko uwezo wa serikali katika kuwapatia ajira na hivyo kutolewa kwa ajira hizo 500 kwa madaktari nchini Kenya ni hatua muafaka kwa serikali katika kuzalisha ajira kwa watu wake kwa kutumia mtengamano wa EAC.

Source: Habari Leo
Hizi ndizo sababu zilizomfanya Rais Magufuli ampe Kenyatta madaktari toka Tanzania Hizi ndizo sababu zilizomfanya Rais Magufuli ampe Kenyatta madaktari toka Tanzania Reviewed by Zero Degree on 3/20/2017 02:21:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.