Loading...

Jinsi Jermain Defoe anvyompa faraja Bradley Lowery

KAMA furaha ni njia moja wapo ya kuongeza siku za kuishi, basi mshambuliaji wa klabu ya Sunderland na timu ya Taifa ya England, Jermain Defoe, anazifanya siku za Bradley Lowery zizidi kuongezeka.

Bradley Lowery ni mtoto wa miaka mitano ambaye ni shabiki mkubwa wa klabu hiyo ya Sunderland ya nchini England, amekuwa akisumbuliwa na tatizo la saratani.



Mwishoni mwa mwaka jana wataalamu wa ugonjwa huo ambao walikuwa wanamfanyia matibabu mtoto huyo, waliweka wazi kuwa hana muda mrefu wa kuendelea kuishi duniani kutokana na hatua aliyofikia.

Desemba mwaka jana walisema mtoto huyo amebakisha miezi miwili kuweza kupoteza maisha yake, hivyo mashabiki mbalimbali wa Sunderland na wadau wa soka walikuwa wanamwombea mtoto huyo lakini wengi waliamini atapoteza maisha kutokana na kauli ya madaktari.



Mapema Februari, mashabiki wengi wa Sunderland waliamini ndio mwezi ambao watampoteza mtoto huyo ambaye ni shabiki mwenzao, lakini siku zote Mungu ndio anayepanga, mwezi wa pili ulimalizika na kuingia wa tatu na bado yupo hai hadi sasa.

Wapo mashabiki ambao waliwatupia lawama madaktari ambao walitoa taarifa hizo ambazo zinaonekana kuwa si sahihi.

Mtoto huyo amekuwa shabiki wa Sunderland kutokana na kuwa na mapenzi na mshambuliaji wao, Jermain Defoe.

Amekuwa na wakati mgumu akiwa anafuatilia mchezo wa Sunderland halafu Defoe akawa yupo nje ya uwanja, anajikuta anatoa chozi.

Wakati yupo hospitalini anapewa matibabu alikuwa pia anaiombea Sunderland ipate ushindi katika michezo yake, hivyo viongozi wa klabu hiyo baada ya kusikia kuwa mtoto huyo anampenda Defoe basi walifanya matembezi ya kushtukiza hadi hospitalini wakiwa na Defoe, mtoto huyo alionekana kuwa na furaha kubwa na kuwashangaza wote ambao walikuwa kwenye msafara huo.

Hiyo ilikuwa ni siku moja kabla ya kumaliza miezi miwili ambayo madaktari walisema anatarajia kupoteza maisha.

Defoe alipewa nafasi ya kulala na mtoto huyo huku wakiamini atakuwa ni mtu wa mwisho kuona uhai wa mtoto huyo ambaye amekuwa ni shabiki wake mkubwa.

Asubuhi ilipofika inasemekana mtoto huyo alikuwa wa kwanza kuamka na kumwamsha Defoe na kumwambia kuwa ‘kumekucha’.

Hadi Defoe anatoka hospitalini hapo mtoto huyo alikuwa anazidi kuwa katika hali nzuri na hadi sasa anazidi kuleta matumaini kwa familia yake na mashabiki kwa ujumla.

Wiki iliyopita kocha wa timu ya Taifa ya England, Gareth Southgate, alikiita kikosi cha timu hiyo kuelekea mchezo wa kirafiki dhidi ya Germany na mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Lithuania.

Katika kikosi hicho mshambuliaji huyo wa Sunderland, Defoe, aliitwa kujiunga na timu hiyo ya Taifa. Kuitwa kwa mchezaji huyo kulizidi kuinua furaha ya mtoto huyo baada ya kupewa taarifa.

Kupitia akaunti ya Twitter ya mtoto huyo iliwekwa video yake ikimwonesha akiruka ruka baada ya kupewa taarifa kuwa Defoe amechaguliwa katika kikosi cha timu ya Taifa.

Mama wa mtoto huyo Gemma, alisema furaha aliyonayo mwanaye baada ya kumpa taarifa kuwa Defoe ameitwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa ni kama yupo kwenye mwezi.



Gemma: Unaweza kutabiri ninachotaka kukwambia? Tabiri ni nani ameitwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa England kwa ajili ya mchezo ujao?

Bradley: Ni nani?

Gemma: Jermain Defoe

Bradley: Yeaaaaah

Mtoto huyo alikuwa na furaha kubwa huku akionekana akiruka ruka kufurahia taarifa hiyo ambayo ilikuwa mpya kwake. Defoe mara ya mwisho kuitwa kwenye kikosi cha timu hiyo ya Taifa ilikuwa 2013 baada ya kucheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Chile.

Kikubwa ni kwamba, Defoe anatakiwa kuendelea kujituma uwanjani ndani ya klabu yake na timu ya Taifa ili kuweza kumpa furaha mtoto huyo ambayo itamfanya aongeze siku zake za kuishi kama kweli furaha inaongeza siku za kuishi.
Jinsi Jermain Defoe anvyompa faraja Bradley Lowery Jinsi Jermain Defoe anvyompa faraja Bradley Lowery Reviewed by Zero Degree on 3/20/2017 02:28:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.