Loading...

Jinsi Mtoto wa miaka 14 alivyobakwa na watu watano

Mratibu wa Kituo cha Usuluhishi kutoka Chama cha Waandishi wa Habari Tanzania (TAMWA), Gladness Hemedi Munuo(kushoto) [Picha ya Mtandao]
WAKAZI wa Kibaha mkoani Pwani, wamebubujikwa machozi baada ya mtoto wa miaka 14 (jina linahifadhiwa), kueleza jinsi alivyobakwa na watu watano, huku kukiwa hakuna hatua madhubuti zilizochukuliwa kwa wabakaji hao.

Hayo yalijitokeza mjini Kibaha wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, ambayo iliandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake mkoani Pwani (PWMO).

Wananchi waliohudhuria maadhimisho hayo, ambayo yalifanyika kwenye Uwanja wa Bwawani Maili Moja, walionekana wakilia wakati akitoa ushuhuda wa jinsi alivyobakwa. Akisimulia, mtoto huyo alisema alibakwa na watu watano. Tukio hilo lilitokea mwaka jana.

Mtoto huyo alikuwa akisoma darasa la saba. Tukio hilo lilimuathiri kisaikolojia. Alisema siku ya tukio alikuwa ametumwa dukani na njiani akakutana na kijana, akamshika kwa nguvu na kumvutia vichakani, ambaye alianza kumwingilia na ghafla wakatokea wengine wanne.

Yule wa kwanza alipomaliza, akaanza wa pili na wakati huo wote alikuwa akipiga kelele. Kelele hizo zilisababisha vijana hao kukimbia na kumwachia majeraha na maumivu makali. Alieleza kuwa kesi hiyo ilipelekwa mahakamani, lakini imekuwa ikisuasua, hivyo kuleta hofu kuwa haki inaweza isipatikane.

Awali, akiibua suala hilo la ubakaji, Diwani wa Viti Maalumu, Elina Mgonja alisema vitendo vya ukatili kwa wanawake ikiwemo ubakaji, vimekithiri huku wanawake na watoto wakikosa haki zao na kunyanyaswa. Mgonja alisema baadhi ya watu, wamekuwa wakifumbia macho vitendo hivyo vya unyanyasaji na ukatili wa kijinsia.

“Hawa ni wachache tu wanaofanyiwa vitendo hivyo vya ukatili, hivyo tunaomba vyombo vinavyohusika na utoaji wa haki, kuzingatia sheria ili wale wanaohusika waweze kupata adhabu inayostahiki,” alisema Mgonja.

Kwa upande wake, Mwakilishi kutoka Mahakama ya Mkoa wa Pwani, Herieth Mwailolo alisema kama kesi hiyo ina matatizo, zinaweza zikachukuliwa hatua zaidi kwa kupeleka suala hilo mahakama za juu.

Mwailolo alisema kuwa familia husika, inatakiwa iende kwa mwanasheria mkuu wa serikali ili kumuomba afuatilie kesi hiyo na kama kuna makosa basi yaangaliwe ili haki ipatikane, kwani kesi kwa sasa zinachukua muda mfupi kama ushahidi umekamilika.

Mgeni rasmi kwenye maadhimisho hayo, Gladys Munuo ambaye ni Mratibu wa Kituo cha Usuluhishi kutoka Chama cha Waandishi wa Habari Tanzania (TAMWA), alisema waandishi wa habari wana uwezo wa kupaza sauti na kufichua vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia ndani ya jamii.

Munuo alisema kuwa licha ya kwamba kumekuwa na uelewa kidogo juu ya masuala ya jinsia, lakini bado kuna watu ambao hawajaona umuhimu wa kuacha vitendo hivyo vya ukatili, ambavyo havifai ndani ya jamii.

Aliwataka waandishi wa habari kufuatilia fursa, ambazo zinapaswa kupewa wanawake, ikiwa ni pamoja na asilimia tano inayotolewa na halmashauri nchini. Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari mkoani Pwani, Mwamvua Mwinyi alisema kuwa bado fursa kwa upande wa wanawake hazijatolewa kikamilifu, kwani wamekuwa wakipewa uongozi wa chini.

Mwinyi alisema kwa kuwa nchi kwa sasa mkakati wa kuwa na viwanda, waajiri wazingatie usawa wa kijinsia, badala ya kupendelea wanaume, kwani hata wanawake wana elimu kubwa kama wenzao.

Alisema changamoto kubwa inayowakabili ni ukosefu wa fedha au usafiri, kuweza kufika maeneo ya vijijini kwa ajili ya kufichua maovu yanayofanywa maeneo ya pembezoni mwa miji. Chama hicho kilianzishwa mwaka 2013 kikiwa na wanachama 15.

Source: Habari Leo
Jinsi Mtoto wa miaka 14 alivyobakwa na watu watano Jinsi Mtoto wa miaka 14 alivyobakwa na watu watano Reviewed by Zero Degree on 3/09/2017 01:34:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.