Loading...

Lissu akamatwa kwa mara ya 5, asafirishwa chini ya ulinzi kutoka Dodoma hadi Dar

JESHI la Polisi limemtia mbaroni kwa mara ya tano Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), ikiwa imebaki siku moja kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).

Mkutano huo wa uchaguzi unatarajiwa kufanyika kesho jijini Arusha, huku joto likizidi kupanda baada ya mwanasheria huyo machachari kujitosa kuwania nafasi ya urais, hatua ambayo inapingwa na Serikali na hata kutishia kuifuta TLS kwa madai ya wanachama wake kuingiza siasa.

Lissu alikamatwa jana saa 5 asubuhi nyumbani kwake Area C mjini hapa wakati akijiandaa kuelekea Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma kusikiliza uamuzi wa kesi ya kupinga uchaguzi wa TLS ambayo ilifunguliwa na Wakili Godfrey Wasonga.

Saa chache baada ya askari kuzingira nyumba yake, Lissu aliandika ujumbe ambao ulisambaa katika mitandao ya kijamii, akieleza namna polisi walivyokwenda kumtia mbaroni.

“Wandugu wapendwa. Ninaandika haya nikiwa nyumbani kwangu Dodoma. Najiandaa kwenda mahakamani kwa ajili ya uamuzi wa Mahakama Kuu juu ya kesi ya kutaka kuzuia Uchaguzi wa TLS.

“Ninawapa taarifa kwamba nimefuatwa nyumbani na askari wawili kutoka ofisi ya RPC Dodoma, sijazungumza nao bado, lakini ni wazi wana maagizo ya kunikamata na kunizuia kuja Arusha kwenye Uchaguzi wa TLS.

“Wameshindwa kuzuia uchaguzi wetu mahakamani, sasa kama kawaida ya Serikali za kidikteta kila mahali, wanatumia mabavu ya kijeshi.

“Wito wangu kwenu mawakili wa Tanzania, nendeni Arusha mkachague viongozi wa TLS watakaopigania haki za binadamu, utawala wa sheria na demokrasia. Msipofanya hivyo, hakuna mtu yeyote, hata ninyi mawakili, atakayepona kwenye utawala wa aina hii.

“Kumbuka, kama Nimrod Mkono anaweza kufungiwa ofisi na TRA, ni wakili gani mwingine aliye salama?” alisema na kuhoji Lissu katika andiko lake hilo.

Kutokana na hali hiyo, alisema anakwenda mahabusu na gerezani huku akiwaomba kura ili aweze kuwaongoza katika kipindi hiki ambacho alikiita kigumu.

“Hiki sio kipindi cha kuwa na viongozi wanaojipendekeza kwa wanaokandamiza haki za watu wetu na haki za mawakili wetu.

“Hiki ni kipindi cha kuwa na viongozi watakaopigania haki zenu na haki za watu wetu, mnanifahamu, nipeni jukumu hili la kuwaongoza kwenye giza hili nene na msikubali kuyumbishwa,” alisema Lissu.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa, alithibisha kukamatwa kwa mbunge huyo akiwa nyumbani kwake Area C kutokana na agizo walilopokea kutoka Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.

Lissu alisafirishwa kupelekwa Dar es Salaam jana mchana kwa gari ya polisi aina ya Land Cruiser nyeupe yenye namba CY75XTGP.

Alipoulizwa sababu za kukamatwa kwa mbunge huyo, Kamanda Mambosasa alisema hafahamu zaidi ya kudai inawezekana aliruka dhamana katika kesi mojawapo kati ya zinazomkabili.

Baada ya kuwasili jijini Dar es Salaam jana 11:45 jioni akiwa chini ya ulinzi, aliingizwa katika chumba cha mahabusu kabla ya kupata fursa ya kuzungumza na wakili wake Nashon Nkhungu.

Wakili Nkhungu alisema kuwa pamoja na kuzungumza na mteja wake, lakini bado hakuwa ameelezwa sababu ya kukamatwa kwake.

“Hadi sasa (saa moja usiku) nimezungumza na mteja wangu na hajahojiwa na hajaelezwa sababu ya kukamatwa kwake. Na pia wamemnyima dhamana,” alisema Wakili Nkhungu.

MATUKIO YA LISSU KUKAMATWA
Desemba 15, mwaka jana Lissu alikamatwa na Jeshi la Polisi na kupelekwa katika Kituo Kikuu, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwa madai ya uchochezi kutokana na kauli aliyoitoa katika moja ya mikutano yake kuhusu kupotea kwa msaidizi wa Mwenyekiti wa Chadema, Ben Saanane.

Februari 6, mwaka huu, alikamtwa tena na Polisi Mkoa wa Dodoma kwa maagizo kutoka makao makuu ya jeshi hilo Dar es Salaam.

Lissu alikamatwa saa 11 jioni akiwa katika viwanja vya Bunge alipokuwa akihudhuria vikao.

Machi 6, alikamtwa tena katika maeneo ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.

Source: Mtanzania
Lissu akamatwa kwa mara ya 5, asafirishwa chini ya ulinzi kutoka Dodoma hadi Dar Lissu akamatwa kwa mara ya 5, asafirishwa chini ya ulinzi kutoka Dodoma hadi Dar Reviewed by Zero Degree on 3/17/2017 11:30:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.