Loading...

Lissu pigo jingine kwa Waziri Mwakyembe

TUNDU Lissu ameongeza pigo lingine katika wiki iliyoonekana kuwa na upepo mbaya kisiasa kwa Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe!

Hivyo ndivyo inavyoweza kuelezewa na baadhi ya wafuatiliaji wa masuala ya siasa nchini, baada ya Lissu ambaye ni Mbunge wa Singida Mashariki na Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kuibuka na ushindi wa kishindo wa zaidi ya asilimia 84 ya kura zilizopigwa katika uchaguzi wa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) jijini Arusha, jana.

Katika uchaguzi huo uliokuwa na misukosuko kadhaa kabla ya kufanikishwa kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC), Lissu alitangazwa mshindi na kuibua shangwe na nderemo jana jioni.

Kwa mujibu wa mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi huo, Kabuta Ongwamuhana, Lissu alifuatiwa kwa mbali na Victoria Mandari aliyepata kura 176, Francis Stola kura 64 na Godwin Mwapongo kura 23.

Ongwamuhana aliwataja washindi wa nafasi nyingine kuwa ni Godwin Ngwilimi aliyepata kura 1,269 na kuwa Makamu wa Rais; Sadock Magai alishinda nafasi ya kuwa Mweka Hazina (kura 1,103) huku wajumbe wakiwa ni Stephen Axwesso, Aisha Sinda, Jeremiah Mtebesya, Hussein Mtembwa , Lambaji Madai, Madeline Kimei na Godluck.

Baadhi ya mawakili waliozungumza baada ya kutangazwa kwa mtokeo hayo yaliyoibua shangwe kubwa ukumbini, walisema ushindi wa Lissu ni mwendelezo wa wiki mbaya kwa wakili mwenzao, Dk. Mwakyembe kwa sababu alionekana wazi kuwa hakutaka Lissu ashiriki uchaguzi huo na pia uamuzi wa Rais John Magufuli kufuta agizo lake kuhusu zuio la ufungishwaji ndoa kwa watu wasiokuwa na vyeti vya kuzaliwa.

“Ushindi wa Lissu umehitimisha wiki mbaya kwa Mwakyembe.

Ni kwa sababu alionekana wazi akipinga Lissu agombee na hivyo hatafurahi hata kidogo kuona kuwa amekabiliana na vikwazo vyote na mwishowe kushinda,” alisema wakili huyo kabla ya kuongeza:

“Ushindi huu wa kishindo wa Lissu ni pigo lingine kwake bada ya Rais Magufuli kufuta agizo lake lililokuwa na utata mwingi kuhusiana na amri ya kuzuia kuwafungisha ndoa watu wasiokuwa na vyeti vya kuzaliwa. Bila shaka hii itabaki kwenye kumbukumbu kuwa ni moja ya wiki mbaya kwake katika masuala ya uongozi.”

Juzi, Rais Magufuli alitangaza kufuta agizo la Mwakyembe la kutaka kuanzia Mei Mosi, mwaka huu kusiwe na ruhusa ya kuwafungisha ndoa watu wasio na vyeti vya kuzaliwa.

Miongoni mwa viunzi alivyokumbana navyo Lissu na wenzake katika safari ya kuelekea uchaguzi wao jana ni pamoja na kesi kuzuia kufanyika kwake ili kuhakikisha uchaguzi huo unasimamishwa na pia Dk. Mwakyembe kuwahi kukaririwa akitishia kukifuta chama hicho iwapo kitakuwa na mwelekeo wa kisiasa.

Kauli ya Dk. Mwakyembe ilionekana kumlenga moja kwa moja Lissu, kwa madai kuwa kama TLS itaongozwa na mwanasiasa, kuna hatari TLS ikaacha majukumu yake ya msingi.

KAZI YA KWANZA YA LISSU TLS

Baada ya ushindi wake jana, Lissu anatarajiwa kuanza na kazi nzito ya kufanikisha uchunguzi wa sakata la ubadhirifu wa fedha za chama hicho.

Kabla ya kutangazwa kwa matokeo, wanachama wa chama hicho, kwa kauli moja walikubaliana kuunda kamati ya watu watano kuchunguza ubadhirifu wa fedha za mwaka 2015/2016.

Wakati mawakili hao wakijadili ripoti fedha ya chama hicho, waligeuka mbogo na kuikataa, wakisema ina ishara za ubadhirifu mkubwa.

Rais aliyemaliza muda wake, John Seka, alisema iwapo uchunguzi utabaini kuna viongozi walihusika, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Mabishano makali kati yao kuhusu ripoti hiyo, yalitokea wakati wakijadili kifungu kwa kifungu baada ya kila mjumbe kuonyesha shaka kuhusu matumizi ya fedha.

Katika mchango wake, Wakili Lawrence Masha aliutaka uongozi wa TLS kubwaga manyanga ili uchunguzi wa ripoti hiyo ufanyike dhidi yao. Masha alikuwa mmoja wa wagombea wa urais wa TLS lakini alitangaza juzi kujitoa na kumuunga mkono Lissu.

“Mwaka jana mlishindwa kujieleza na mwaka huu mmeshindwa tena. Hili haliwezi kuvumilika. Lazima mbwage manyanga ili kupisha uchunguzi,” alisema Masha, huku akiungwa mkono na Edmund Ngemela, aliyewataka wajumbe wenzake kukubali kuunda kamati itakayofanya uchunguzi wa ripoti hiyo.

Baada ya mabishano hayo, ndipo wajumbe waliafiki kuundwa kwa kamati ambayo wajumbe wake wengine ni pamoja na Rweikama Rweikiza, Lawrence Masha, Anna Juilia, Magdalena Sylvester na Dulia Nicolas.

Mwenyekiti wa kikao hicho, Seka, alisema, kamati hiyo itatakiwa kushirikiana na uongozi mpya kuchunguza na kutoa mapendekezo ya nini kifanyike kama itabainika kuna ubadhirifu wa fedha.

Awali, Profesa Josephat Kanywanyi, aliwataka wajumbe kuunga mkono hoja ya kuunda kamati ili kushughulikia suala hilo.

Wakili Andrew Kaisari alishangaa wajumbe kushindwa kupata nakala za ripoti hiyo huku wengine wakiwa wameipata kuelekea mwishoni wakati Exavery Makwi akisema chama hicho kimepata hasara nyingi iliyochangiwa na uongozi dhaifu.

Alisema wanachama wanaongezeka lakini taarifa ya michango ya fedha inaonekana kushuka na matumizi kuongezeka.

Kwa upande wake, Wakili Andrew Kasaiz alihoji kuhusu risiti zilizopo akilitilia shaka kuwa huenda ziko ambazo ni bandia au zimechakachuliwa.

Wakili Amin Mshana, alitaka maelezo kuhusu Sh. milioni 50 zilizotolewa na Foundation for Civil Society (FCS) kwenye taarifa inasomeka Sh. milioni 25.

Source: Nipashe
Lissu pigo jingine kwa Waziri Mwakyembe Lissu pigo jingine kwa Waziri Mwakyembe Reviewed by Zero Degree on 3/19/2017 12:19:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.