Loading...

Mahakama yawahukumu wawili kifungo cha miaka 30 jela kwa wizi wa pikipiki mkoani Tabora

MAHAKAMA ya Wilaya ya Igunga mkoani Tabora imewahukumu vijana wawili kutumikia kifungo cha miaka 30 jela kila mmoja kwa wizi wa kutumia silaha.

Waliohukumiwa na mahakama hapo ni Michael Machiya (25) mkazi wa kitongoji cha Itagata Kijiji cha Migandu mkoani Singida na Sanyiwa Mbalu (25) kutoka Kijiji cha Mgoroka Wilaya ya Mpanda mkoa wa Katavi.

Awali Mwendesha Mashtaka wa Polisi WIlaya ya Igunga, Elimajid Kweyamba alidai mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Wilaya, Ajali Milanzi kuwa watuhumiwa hao walikamatwa Februari 6 mwaka huu usiku katika mtaa wa Mwayunge barabara ya Mwanzugi Igunga mjini.

Washtakiwa wote wawili kwa pamoja walikuwa wakituhumiwa kuiba pikipiki ya SANLG yenye thamani ya Sh milioni 2.2 mali ya Mazinge Jumanne ambaye ni dereva wa bodaboda mkazi wa mtaa wa Mwayunge ambaye walimkata na kitu chenye ncha kali shingoni.

Washtakiwa walikana kutenda kosa hilo lakini mashahidi watano akiwamo muathirika wa tukio hilo waliwatambua washtakiwa.

Kabla ya kutoa hukumu, Hakimu Ajali Milanzi alisema mahakama imewaona wana hatia hivyo  walihukumiwa kwenda jela miaka 30 kila mmoja huku pikipiki ikikabidhiwa kwa mwenye mali.
Mahakama yawahukumu wawili kifungo cha miaka 30 jela kwa wizi wa pikipiki mkoani Tabora Mahakama yawahukumu wawili kifungo cha miaka 30 jela kwa wizi wa pikipiki mkoani Tabora Reviewed by Zero Degree on 3/30/2017 11:20:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.