Loading...

Masaa matatu ya RC Makonda kwenye kitimoto mbele ya kamati nzito ya Bunge

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, akihojiwa na Kamati ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge iliyomtaka kufika mbele yake tangu mwezi uliopita kufuatia matamshi aliyoyatoa kudaiwa kuwa yenye kudharau chombo hicho cha kutunga sheria. PICHA: BUNGE
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda jana alihojiwa kwa saa tatu mfululizo na Kamati ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge kwa tuhuma za kuingilia haki, uhuru na madaraka ya chombo hicho cha kutunga sheria.

Makonda aliwasili Bungeni Dodoma majira ya saa nne asubuhi kuitikia wito wa Kamati hiyo uliotokana na Azimio la Bunge lililotolewa Februari 8 na kuhojiwa na kamati hiyo kwa muda wa saa tatu kuhusu tuhuma zinazomkabili.

Katika kikao hicho, Bunge liliamua Makonda aitwe kujieleza kwenye Kamati ya Bunge ya Haki, Kinga na Madaraka kwa tuhuma za kukashfu chombo hicho.

Sambamba na uamuzi huo, pia Bunge liliagiza mbunge yeyote ambaye kwa namna yoyote anadhani amekashfiwa na Makonda, awasilishe malalamiko yake kwa Spika ili hatua zaidi zichukuliwe.

Hatua ya kutaka Makonda aitwe mbele ya kamati hiyo, ilitokana na mwongozo uliotolewa na Mbunge wa Mkuranga(CCM), Abdallah Ulega, kwa Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge, aliyedai mkuu huyo wa mkoa ameudharau mhimili huo wa dola na wabunge.

Akizungumza mara baada ya kumaliza kazi yao, Mwenyekiti wa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, George Mkuchika alisema Makonda alidaiwa kutoa kauli kupitia televisheni ya Clouds akidai kwamba wabunge wanasinzia bungeni jambo lililoonekana kwamba ni kudharau mhimili huo wa dola.

“Napenda kutoa taarifa kwamba mheshimiwa Makonda leo amekuja mbele ya Kamati na ametupa ushirikiano mzuri," alisema Mkuchika ambaye ni mbunge wa Newala Mjini (CCM).

"Tumepokea maelezo yake na Kamati imemaliza kazi yake.”

Alisema Kamati yake itakabidhi taarifa yake kwa Spika Job Ndugai kwa mujibu wa kanuni, ambaye ndiye atakayeamua namna ya kutoa taarifa kuhusu kazi ya kamati hiyo.

Katika mwongozo wake kwa Spika, Ulega kwa kutumia Kanuni ya 68 (7), alisema kupitia vyombo vya habari, kuna taarifa kwamba Makonda ametoa kauli ambazo zinaashiria na kuonyesha dharau kwa Bunge.

“Sisi wabunge tuko mstari wa mbele katika kuhakikisha tunapambana na kumsaidia Rais (John Magufuli) kwenye vita dhidi ya dawa za kulevya. Ikumbukwe kwamba sheria inayosimamia vita dhidi ya dawa hizo imeundwa kwenye Bunge hili," alisema Ulega.

“Kama haitoshi wabunge bado tunayo kumbukumbu siku alipokuja kipenzi chetu, Rais Dk. John Magufuli na kuhutubia, tulimshangilia sana alipotangaza rasmi kwa nguvu zake zote juu ya vita dhidi ya dawa za kulevya.

"Leo wabunge wameambiwa kwamba hawana jambo isipokuwa wanakuja kufanya kazi ya kulala kwenye Bunge hili.”

KIJANA MZALENDO:

Mbunge huyo alisema akiwa kijana mzalendo na Makonda kuwa mdogo wake na rafiki yake pia, ni lazima Bunge kama chombo huru kiendelee kuheshimika.

“Sisi tunadhani ya kwamba mawili... ama kijana mwenzangu huyu hakuwa anajua anachokisema au amefanya dharau ya makusudi.

"Ninaomba kutoa hoja zifuatazo ili unipe mwongozo tuone tunaendaje kutoka hapa tulipo, hasa ukizingatiwa sisi ndio ‘number one’ wa kumsaidia Rais katika vita hii.”

Katika hoja hizo, Ulega aliomba Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwa kiongozi mkuu wa serikali, achukue hatua za makusudi ili kuwalindia heshima wabunge.

“Au kwa kutumia kanuni za Bunge na sisi tunayo kanuni ya haki, kinga na madaraka ya Bunge, kanuni na sheria basi hatua zichukuliwe kupitia muhimili huu, au atumie tena vyombo vya habari vile vile kusema kwamba amekosea na anaomba radhi, naomba mwongozo,” alisema Ulega.

Mbali na Ulega, Mchungaji Peter Msigwa wa Iringa Mjini (Chadema), alimpongeza Ulega kuomba mwongozo huo wa msingi kwa hadhi ya Bunge.

“Naomba kwenda kwenye kanuni ya 51 ya Bunge ili wabunge tujadili kuhusu tabia ya Mkuu wa Mkoa huyu anayedhalilisha chombo hiki ambacho ni muhimili muhimu ambacho kinaweza ku-‘balance’

(kuweka mambo sawa) ili serikali ifanye kazi," alisema Msigwa.

"Naomba tujadili hadhi ya Bunge iweze kulindwa. Naomba kutoa hoja.”

Akijibu mwongozo huo, Chenge alisema: “Nimepokea ombi la mwongozo wa Ulega na Msigwa ametaka kuchombeza kama hoja ijadiliwe. Mimi nitajielekeza kwenye ombi la muongozo. Nimemuelewa Mheshimiwa Ulega maelezo yake mazuri tu."

Chenge alisema Bunge kama taasisi na wajumbe wake na ni moja ya mihimili mitatu ya dola (ikiwamo serikali na mahakama) lazima liheshimiwe na mtu yeyote.

“Kwa vile tumejiwekea utaratibu wetu kupitia Kamati ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge, ili sasa ikathibitike kama ameyasema hayo (ya sisi kulala tu ndani ya Bunge) na wapi, lini na kama yanaangukia ndani ya sheria yetu ya kinga, huko ndiko ukweli wote utakapodhihirika.

“Kwa hiyo mimi kwa suala hili naagiza ofisi ya Katibu wa Bunge, kwa taratibu zilizopo, wamtake Makonda atoe maelezo yake na kama kweli amesema au la na watayapokea na kupelekwa kwenye Kamati ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge.

"Tutakuwa tupo ndani ya taratibu zetu za kikanuni na ndani ya sheria kwa kuwa lazima ithibitike kama inaangukia kwa haki za Bunge zinazopaswa kuheshimika.”

Source: Nipashe
Masaa matatu ya RC Makonda kwenye kitimoto mbele ya kamati nzito ya Bunge Masaa matatu ya RC Makonda kwenye kitimoto mbele ya kamati nzito ya Bunge Reviewed by Zero Degree on 3/30/2017 11:30:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.