Loading...

Watatu wafikishwa kizimbani kwa kosa la kuhujumu uchumi na kuisababishia hasara serikali

WAFANYABIASHARA watatu akiwemo raia wa Zambia wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakikabiliwa na mashitaka ya uhujumu uchumi ya kusafirisha mali iliyofichwa na kuisababishia serikali hasara ya Sh milioni 478.7.

Washitakiwa hao ni Sultan Ibrahim (36) mkazi wa Usalama Temeke, Augustino Kalumba (39) raia wa Zambia walifikishwa mahakamani hapo na kusomewa mashitaka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.

Aidha, mshitakiwa Ibrahim alipandishwa tena kizimbani na Ramadhan Hamisi (48) ambaye pia ni dalali mbele ya Hakimu Mkazi, Respicious Mwijage.

Wakili Mwandamizi wa Serikali, Nassoro Katuga alidai mbele ya Hakimu Simba kuwa washitakiwa Ibrahim na Kalumba wanakabiliwa na mashitaka matatu ya uhujumu uchumi.

Katuga alidai kuwa washitakiwa wote kwa pamoja kati ya Desemba Mosi mwaka jana na Machi Mosi mwaka huu, maeneo yasiyofahamika walikula njama kinyume na kifungu namba 193 cha Sheria ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Kudhibiti Ushuru ya Mwaka 2004. Alidai washitakiwa hao walikula njama kusafirisha mali iliyofichwa kinyume na sheria hiyo.

Katika mashitaka ya pili ilidaiwa kati ya Desemba mosi na 31 mwaka jana, maeneo ya Mamlaka ya Usimamizi Bandari Tanzania (TPA), waliingiza magari matatu aina ya Range Rover Sports yenye chesisi namba SALW 2KE 9EA 388884 ya rangi nyeusi, chesisi namba SALVA 2CE 4EH 948974 nyeupe na SALGA 2JEODA 115580 yakiwa yamechanganywa na mitumba ya viatu, mabegi na nguo kwenye kontena namba MSKU 9914162.

Pia inadaiwa kati ya Desemba mosi mwaka jana na Machi mosi mwaka huu maeneo ya Bandari wilayani Temeke washitakiwa hao waliingiza mali iliyofichwa na kusababisha serikali kukosa mapato ya Sh milioni 287.8.

Pia Ibrahim na Hamisi walipandishwa kizimbani katika mahakama hiyo mbele ya Hakimu Mwijage ambapo walidaiwa kusababisha hasara ya Sh milioni 190.9.

Katuga akishirikiana na Wakili wa Serikali, Batilda Mushi alidai washitakiwa hao walikula njama kutenda kosa hilo kinyume na sheria ya ushuru kwa kuingiza mali iliyofichwa.
Watatu wafikishwa kizimbani kwa kosa la kuhujumu uchumi na kuisababishia hasara serikali Watatu wafikishwa kizimbani kwa kosa la kuhujumu uchumi na kuisababishia hasara serikali Reviewed by Zero Degree on 3/30/2017 11:42:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.