Loading...

Mkuu wa mkoa wa Mwanza apiga marufuku wanafunzi wa mkoani mwake kutumia simu

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela
MKUU wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela amepiga marufuku matumizi ya simu za kiganjani kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari mkoani hapa.

Mongela alitoa agizo hilo jijini Mwanza alipokuwa akizungumza kwenye mkutano wa wadau wa elimu ambao pia ulihudhuriwa na wakuu wa wilaya, wakurugenzi watendaji, maofisa elimu, wakurugenzi watendaji wa halmashauri zote za mkoa, wadau wa elimu na viongozi wa madhehebu ya dini.

Alisema wanafunzi wengi hivi sasa wameachwa na walezi na wazazi wao wakitumia simu za mkononi kwa ajili ya kuangalia picha za ngono na zile za utupu ambazo kimsingi haziwajengi kwenye misingi ya maadili mema na kuzingatia masomo shuleni.

“Wanafunzi wengi walio na simu hizi wanazitumia vibaya kwa kuangalia video na picha za utupu ambazo hazilengi katika kuwapa maadili na mafunzo bora ya kitaaluma kuanzia leo napiga marufuku matumizi ya simu za mkononi kwa wanafunzi wote kwa mkoa wangu”, alifafanua.

Alisema serikali kwa kushirikiana na uongozi wa shule hizo utaweka utaratibu mzuri utakaowezesha wanafunzi kuwasiliana na wazazi au walezi wao wakati wa shule kwa mambo muhimu zikiwemo taarifa za ugonjwa, ukosefu wa ada na nyingine muhimu zitakazokuwa zikiratibiwa na wakuu wa shule.

Mongela aliwataka wakuu wa shule za msingi na sekondari kuhakikisha kuwa wanatekeleza agizo hilo na kwamba mwanafunzi atakayebainika akiwa na simu ya mkononi akiwa darasani au bwenini au kwenye mazingira ya shule hatua za kinidhamu zichukuliwe dhidi yake mara moja.

“Ni matarajio yangu baada ya agizo hili Wakuu wa shule watapanga utaratibu mzuri wa utekelezaji wa agizo na Wadhibiti ubora wa shule fuatilieni suala hili kwa ajili ya utekelezaji”, alisema.

Kwa upande wao, viongozi wa madhehebu ya dini waliohudhuria mkutano huo, waliiomba serikali ikiwa inataka kuboresha na kuinua kiwango cha taaluma katika mkoa wa Mwanza, wahakikishe madai yote ya walimu yanalipwa kwa wakati.

Kwa upande wake, Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Amani ya Mkoa wa Mwanza, Shehe Hassan Kabeke, alisema suala la madai ya walimu limekuwa ni tatizo sugu karibu kwa maeneo mengi nchini ambapo aliiomba serikali kuchukua hatua mara moja kumaliza tatizo hilo.

Mjumbe wa Kamati hiyo ya Amani ya viongozi wa madhehebu ya dini mkoa wa Mwanza, Askofu Alexander Rwakisumbwa alisema ili kuboresha kiwango cha elimu lazima uwepo ushirikiano wa pamoja.
Mkuu wa mkoa wa Mwanza apiga marufuku wanafunzi wa mkoani mwake kutumia simu Mkuu wa mkoa wa Mwanza apiga marufuku wanafunzi wa mkoani mwake kutumia simu Reviewed by Zero Degree on 3/10/2017 12:45:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.