Loading...

Mkuu wa wilaya ya Kasulu, Kanali Martin Mkisi aondolewa na kurejeshwa jeshini

Kulia ni Mbunge wa Kasulu, Daniel Nsanzugwanko na kulia kwa Waziri ni Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Kanali Martin Mkisi (Aliyeshika 'maiki').
MKUU wa Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, Kanali Martin Mkisi ameondolewa katika wadhifa huo na kurejeshwa jeshini.

Akithibitisha habari hizo, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kasulu, Titus Mughuha amebainisha kuwa Kanali Mkisi alitoa taarifa za uhamisho huo katika kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama na kueleza kuwa anarejea Makao Makuu ya Jeshi alikokuwa mwanzo.

“Ni kweli Kanali Martin Mkisi amepata barua ya kurudi Makao Makuu ya Jeshi. Uhamisho huu ni wa kawaida na haustahili kuhusishwa na uzushi ama sababu zozote,” alieleza Mughuha, kwa mujibu wa taarifa ya Ofisa Habari wa Wilaya ya Kasulu, Respice Swetu.

Mghuha aliongeza pia kuwa kutokana na mabadiliko hayo, nafasi ya Mkuu wa Wilaya ya Kasulu inakaimiwa na Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe, Kanali Marko Gaguti, kusubiri uteuzi wa Rais John Magufuli kwa Mkuu wa Wilaya atakayejaza nafasi hiyo.

Kanali Mkisi amedumu katika nafasi hiyo kwa kipindi cha miezi tisa, akitokea Makao Makuu ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kutokana na uteuzi wa Rais Magufuli kwa wakuu wa wilaya 139 alioufanya Juni, mwaka jana.

Kanali Mkisi anakuwa mkuu wa wilaya wa pili kuondoka katika nafasi ya ukuu wa wilaya katika siku za karibuni baada ya aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Uyui mkoani Tabora, Gabriel Mnyele kuomba kujiondoa katika wadhifa huo, hatua ambayo iliridhiwa na Rais Magufuli na alisema atatangaza mrithi wake baadaye.

Kanali Mkisi amewahi kuwa Kamanda wa Kikosi cha Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Mafinga wilayani Mufindi mkoani Iringa.
Mkuu wa wilaya ya Kasulu, Kanali Martin Mkisi aondolewa na kurejeshwa jeshini Mkuu wa wilaya ya Kasulu, Kanali Martin Mkisi aondolewa na kurejeshwa jeshini Reviewed by Zero Degree on 3/14/2017 06:21:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.