Loading...

Nape kupeleka Ligi Kuu makao makuu ya nchi, Dodoma

WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye ameahidi kusimamia na kuhakikisha maeneo ya wazi au viwanja vya michezo vilivyoporwa au kubadilishwa matumizi vinarudishwa ili kutumika katika kuimarisha michezo makao makuu ya nchi, Dodoma.

Mbali na hilo, Nape pia ameahidi kushirikiana na wahusika kuhakikisha Dodoma inatoa timu za Ligi Kuu ya soka Bara.

“Madiwani wamekuwa wakibadilisha matumizi ya viwanja vya michezo au maeneo ya wazi kwa kuwapa watu kujenga, jambo ambalo wizara yangu itaanza nalo na kuhakikisha vinarudishwa na kutumika kwa ajili ya michezo,” alisema.

Waziri Nape alitoa kauli hiyo mjini hapa jana baada ya wizara yake kuhamia Dodoma na kujitambulisha kwa wakazi wa mji huo kwa kushiriki katika mazoezi ya kukimbia (jogging) pamoja na vikundi mbalimbali vya mjini hapa kuanzia eneo la Nyarere Square hadi Uwanja wa Jamhuri.

Awali, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, anayeshughulikia Kazi, Ajira na Vijana, Antony Mavunde alimwomba waziri awasaidie wakazi wa mkoa huo kuhakikisha kwamba timu zao zinapanda na kucheza Ligi Kuu Bara.

Waziri Nape alikubali ombi hilo akaahidi kwamba atafanya kila analoweza kuhakikisha timu moja au mbili za kutoka hapo makao makuu ya nchi zinapanda daraja na kucheza Ligi Kuu, ili kuwapa burudani viongozi na wakazi wa mji huo na vitongoji vyake.

“Nitafanya kila ninaloweza kutokana na ukweli kwamba mji huu utajengwa uwanja mkubwa kuliko Uwanja wa Taifa Dar es Salaam, hivyo ni vema uwanja huo pia ukatumika na timu za mkoa huu zilizopo katika Ligi Kuu,” alisema.

Nape alisisitiza kwamba, wizara au watumishi wa serikali hawawezi kukaa makao makuu ya nchi bila kuwa na mahali ambapo wanaweza kuona michezo, hivyo ni wajibu wake kuhakikisha kunakuwa na timu Ligi Kuu ambayo itasaidia kuwapa burudani viongozi waliohamia mjini hapa.

Waziri Nape alikubali ombi la kushirikiana na Naibu Waziri, Mavunde ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini (CCM) la kuwa mlezi wa vikundi vya mazoezi (jogging) mjini Dodoma akatoa ahadi kwamba atahakikisha kila mtaa unaanzisha klabu hizo kwa ajili ya kufanya mazoezi na kuondoa vitambi na hivyo kujenga afya zao.

Waziri Nape pia alikubali ombi la Naibu Waziri Mavunde la kuhamasisha mawaziri na watendaji wengine kutoka wizara mbalimbali kushiriki katika michezo mbalimbali ikiwamo hiyo ya kufanya mazoezi.

Waziri Nape alisema, huo utakuwa utaratibu wa wizara hiyo yenye makao makuu yake katika jengo la Mfuko wa Serikali za Mitaa (LAPF) mjini hapa kila wakati kushiriki katika michezo mbalimbali ikiwamo kufanya mazoezi na kuhamasisha wizara nyingine kushiriki katika mazoezi hayo.

Katibu Mkuu, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Elisante Ole Gabriel alisema amefurahishwa na mapokezi ya wakazi wa Dodoma kwa kuwashirikisha katika jogging na michezo mingine katika kujenga afya.

Dodoma ulikuwa maarufu kimichezo kwa nyakati tofauti hasa wakati timu ya Waziri Mkuu na CDA zilipokuwa zikicheza Ligi Kuu kwa miaka kadhaa sasa uwanja wa Jamhuri wa mjini hapa umekuwa hauna timu inayoutumia. Kwa sasa CDA inacheza ligi ya mkoa na Waziri Mkuu ilifutika.

Katika jogging hiyo pia alishiriki Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde (CCM) ambaye aliwataka wakazi wa Dodoma kushirikiana kikamilifu katika kampeni hiyo ya kufanya mazoezi kama kweli wana azma ya kufanikisha dhamira yao ya kujenga afya zao.

Source: Habari Leo
Nape kupeleka Ligi Kuu makao makuu ya nchi, Dodoma Nape kupeleka Ligi Kuu makao makuu ya nchi, Dodoma Reviewed by Zero Degree on 3/03/2017 11:59:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.