Loading...

SADC yaandaa hati moja ya kusafiria [Paspoti] ya kimataifa kwa wanachama wake

JUMUIYA ya Maendeleo kusini mwa Afrika (SADC) inaandaa hati moja ya kusafiria ya kimataifa kwa nchi wanachama wake kwa lengo la kurahisisha usafiri na kukuza uchumi wao.

Mpango huo wa kuandaa pasi moja ya kusafiria utakapokamilika, nchi 15 wanachama wa SADC watakuwa na hati moja ya kusafiria yenye nguvu barani Afrika zaidi ya ile ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambayo awali ilikuwa na nguvu zaidi.

Taarifa ya Jukwaa la Uchumi la Dunia (WEF) ya mwaka 2017 inaonesha kwamba, pasi hiyo ya kusafiria itakuwa na nguvu zaidi kutokana na nchi wanachama 15 kuitumia badala ya utaratibu sasa ambao katika baadhi ya nchi, watu wanatakiwa kuingia wakiwa na viza na hati ya kusafiria.

Taarifa hiyo inaonesha kwamba nchi ya Seychelles inaongoza kwa watu wake kuingia bila viza katika nchi 126, Mauritius (118), Afrika Kusini (90) na Tanzania ni ya 12 ambapo watu wake wanaruhusiwa kuingia katika nchi 62 bila kuulizwa viza.

Muungano wa Afrika (AU) ulizindua pasi ya kusafiria Afrika Julai mwaka jana, miezi minne baada ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuzindua pasi ya kimtandao jijini Arusha. Pasi ya kusafiria katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ilianza kutumika Januari mwaka huu, wakati ile ya Muungano wa Afrika (AU) itaanza kutumika mapema mwakani.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dk Augustine Mahiga aliliambia gazeti hili kwamba hati hiyo ya kusafiria itakuza uchumi wa nchi wanachama, Tanzania ikiwamo kama mwanachama wa AEC na SADC.

Nchi wanachama wengine wa SADC ni Angola, Botswana, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Madagascar, Malawi, Mauritius, Msumbiji, Namibia, Seychelles, Afrika Kusini, Swaziland, Zambia na Zimbabwe.

“Hati hiyo ya kusafiria itaondoa kama sio kumaliza kabisa changamoto ambazo zilizokuwa zikiwakumba wanachama wa nchi hizo za kudaiwa viza na hati za kusafiri wanapoingia katika nchi nyingine,” Waziri Mahiga alisema. Pia, alisema zitasaidia kuondoa vizuizi vilivyokuwapo kwenye mipaka baina ya nchi na kwenye Bara kwa ujumla.” alisema.

Maendeleo hayo mapya ya kuanzisha pasi moja ya kusafiria yanakuja wakati ambapo nchi nyingi duniani zinapambana kuhusu wahamiaji wasio na hati za kusafiria ambao wahamiaji wanasumbuliwa kwa kutokuwa na nyaraka za kusafiria.

Mtandao wa SADC unaonesha kwamba malengo ya mkataba wa Umoja wa Nchi hizo wa kuhamasisha sera na kuondoa vikwazo mipakani, ni pamoja na kuruhusu watu kusafiri kutoka nchi moja hadi nyingine bila kusumbuliwa.

Naibu Katibu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ramadhani Mwinyi alilieleza gazeti hili kwamba, nchi za SADC zinarekebisha mfumo wa hati ya kusafiria na katika muda mfupi ujao, zitakuwa na pasi moja ya kusafiria.

Mwinyi alisema mkakati nchi za SADC ni kuhakikisha zinakuwa na mfumo mmoja wa hati ya kusafiria ili kuhakikisha nchi za EAC ambazo pia ni wanachama wa SADC, zinakuwa na hati moja ya kusafiria.

Hivi karibuni serikali ya Msumbiji iliwatimua wahamiaji 4,000 kutoka Tanzania wasio na pasi za kusafiria waliokuwa wakiishi na kufanya kazi katika nchi hiyo iliyo Kusini mwa nchi hii.
SADC yaandaa hati moja ya kusafiria [Paspoti] ya kimataifa kwa wanachama wake SADC yaandaa hati moja ya kusafiria [Paspoti] ya kimataifa kwa wanachama wake Reviewed by Zero Degree on 3/07/2017 12:37:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.