Loading...

Siri ya Simba SC kuifunga Yanga yafichuka

KAMA kuna mtu anadhani bado Simba wanaendelea na sherehe za kuwafunga Yanga, atakuwa anajidanganya, kwani Wekundu hao wa Msimbazi ni kama wamesahau yaliyopita na siri iliyopo ni kuweka mikakati ya kuhakikisha kila timu itakayokuja mbele yao haibaki salama.

Jumamosi iliyopita, Simba waliwafunga Yanga ambao ni wapinzani wao wa jadi kwa mabao 2-1 na kufikisha jumla ya pointi 54 katika michezo 23 na kujichimbia kileleni mwa msimamo wa ligi, huku Wanajangwani wao wakibakia nafasi ya pili na pointi zao 49.

Kutokana na matokeo hayo, wengi walidhani kuwa uongozi, wachezaji pamoja na benchi la ufundi, watakuwa wanaendelea kula bata kwa furaha, lakini hali ni tofauti kabisa, kwani mikakati iliyowekwa na Wana Msimbazi hao, ni kuhakikisha wanatwaa ubingwa msimu huu.

Moja ya siri ambazo zimebainika ni kwamba, baada ya ushindi dhidi ya Yanga, viongozi waliwaita wachezaji wote pamoja na benchi la ufundi wakakaa kikao kizito ambapo pamoja na mambo mengine, walijadiliana namna ya kushinda michezo yao saba iliyobakia.

Katika suala hilo waliafikiana kuwa watapambana kila mmoja kwa nafasi yake ili wasije wakapoteza pointi yoyote katika michezo hiyo na kwa kuanzia watahakikisha Mbeya City wanaondoka na kapu la mabao katika mchezo wa mwishoni mwa wiki hii utakaochezwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Katika kikao hicho wachezaji waliuahidi uongozi kwamba watapambana ndani ya uwanja na kuwapa mashabiki wao raha kama ile waliyowaonjesha dhidi ya Yanga, wakiamini kuwa wanao uwezo mkubwa wa kufanya jambo lolote na wakati wowote.

Siri nyingine kutoka Simba, zinadai kuwa, presha waliyonayo ni kuhusu michezo yao ya Kanda ya Ziwa dhidi ya Toto African pamoja na Mbao FC, itakayochezwa Uwanja wa CCM Kirumba, na ule dhidi ya Kagera Sugar utakaopigwa Uwanja wa Kambarage na sasa wamepanga mikakati ya kuhakikisha wanashinda.

Simba wanaamini kuwa, wakifanikiwa kushinda michezo hiyo mitatu, watakuwa wametangaza ubingwa, hivyo pamoja na kwamba wanataka kushinda michezo yao saba iliyobakia, lakini nguvu kubwa ni hiyo michezo mitatu ya Kanda ya Ziwa.

Wakati hayo yote yakiendelea, licha ya kwamba mashabiki wanawapa hamasa kubwa wachezaji wao kwa kuwashangilia, wapo baadhi ya vigogo wakubwa, wakiwamo wabunge wanaoshirikiana na uongozi wa Rais Evans Aveva, ambao wanapiga jeki kwa kutoa fedha zao kama motisha kila timu inapokuwa na mechi ya Ligi Kuu.

Vigogo hao, wakiongozwa na mfanyabiashara maarufu na mwanachama wa Klabu hiyo, Mohamed Dewji ‘Mo’, wamekuwa chachu kubwa ya mafanikio ya ushindi kutokana na kuchangia fedha kwa ajili ya kutoa hamasa kwa wachezaji, jambo ambalo linaongeza morali kwa kiasi kikubwa.

Jambo jingine ambalo limeonekana kuleta mafanikio msimu huu katika timu hiyo ni umoja ambao Rais Aveva ameonekana kuhaha kuunganisha baadhi ya makundi ambayo yalikuwa yamejitoa baada ya uongozi huo kuingia madarakani.

Umoja uliopo Simba kwa sasa unafanana na ule uliowahi kuwapo mwaka 2003, pale walipoungana na kufanikiwa kuivua ubingwa timu ya Zamaleck ya Misri kwenye michuano ya Klabu Bingwa Afrika enzi hizo.

Habari za uhakika ni kwamba wadau zaidi ya 200 sasa wameungana kwa ajili ya kuhamasisha timu kufanya vizuri katika ligi.

Kocha msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja, alisema baada ya kumaliza mchezo wao na Yanga walikaa na wachezaji wake na kuwaambia kuwa safari bado ni ndefu na wanatakiwa kupambana kuhakikisha wanatwaa ubingwa, pia amewataka wasahau kusherehekea ushindi dhidi ya Yanga, kwa vile mchezo huo ni kama mchezo mwingine, tofauti yake ule ni derby na sherehe tu na vilevile umeongeza heshima kwa timu yao.

Source: DIMBA
Siri ya Simba SC kuifunga Yanga yafichuka Siri ya Simba SC kuifunga Yanga yafichuka Reviewed by Zero Degree on 3/01/2017 10:50:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.