Loading...

Tanesco inadaiwa Bilioni 4 na Mamlaka ya Mapato Tanzania [TRA]

KAMATI ya Nishati na Madini imesema Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) linadaiwa zaidi ya Sh bilioni nne na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa ajili ya kodi za kutolea mitambo ya gesi bandarini.

Kamati hiyo imesema katika fedha hizo, pia ni kwa ajili ya kuilipa Mamlaka ya Usimamizi Bandari Tanzania (TPA) kuhusu makato mbalimbali ya kutolea mitambo hiyo ya Mradi wa Kinyerezi II.

Mwenyekiti Kamati ya Nishati na Madini, Deo Ngalawa
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Deo Ngalawa alisema jana walipotembelea maendeleo ya Mradi wa Umeme Kituo cha Kinyerezi I na Kinyerezi II, Dar es Salaam.

Alisema wataishauri kwa kina Serikali kuona namna ya kuisaidia Tanesco kulipa deni hilo ili mradi uendelee.

“Tunaamini kuwa hizi zote ni taasisi za serikali tunaweza kukaa na kuishauri serikali ikiwezekana mizigo uitolewe kisha baadaye Tanesco iweze kulipa ili kuendelea kwa mradi huu,” alisema Ngalawa ambaye ni Mbunge wa Ludewa.

Alisema maeneo mengi ya mradi huo yanahitaji kuwekwa mitambo ambayo imezuiliwa kutoka kutokana na deni hilo, hivyo watazungumza na serikali kuona namna ya kutatua changamoto hiyo.

Ngalawa alisema lengo la ziara hiyo ni kujua upatikanaji umeme kisekta upoje ili usaidie kufanikisha mkakati huo wa serikali ya viwanda katika nchi.

Alisema katika Mradi wa Kinyerezi II, Serikali haidaiwi kwa kuwa imetoa asilimia 15 ya fedha inayotakiwa kwa ajili ya maendeleo ya miradi hiyo.

Alisema serikali imetenga bajeti ya Sh bilioni 110 kwa ajili ya masuala ya umeme na kwamba imeshalipa Sh bilioni 88 sawa na asilimia 80, suala lililohojiwa na Mbunge wa Bukoba Mjini, Wilfred Lwakatare aliyetaka kujua ni kiasi gani cha fedha ambacho Tanesco wamekipata kutoka serikalini.

Msaidizi wa Mkurugenzi Mtendaji Uwekezaji, Khalid James alikiri kuwepo kwa deni hilo na kueleza kuwa baadhi ya mitambo imeanza kutolewa bandarini na kupelekwa kituoni hapo.

Alisema fedha za kulipia vifaa hivyo zipo na wataendelea kulipa kwa ajili ya kuhakikisha wanaleta mitambo hiyo.

Source: Habari Leo
Tanesco inadaiwa Bilioni 4 na Mamlaka ya Mapato Tanzania [TRA] Tanesco inadaiwa Bilioni 4 na Mamlaka ya Mapato Tanzania [TRA] Reviewed by Zero Degree on 3/24/2017 03:06:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.