Loading...

Tundu Lissu [CHADEMA] 'anunua' kesi nzito

TUNDU Lissu ambaye ni mmoja wa wagombea urais wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), atawasilisha maombi Mahakama Kuu, ili aunganishwe kwenye kesi ya kupinga uchaguzi wa chama hicho, iliyofunguliwa juzi katika miji ya Dodoma na Dar es Salaam.


Mbali na Lissu, mgombea mwingine wa nafasi ya urais wa TLS, wakili Lawrence Masha atawasilisha ombi kama hilo.

Wakizungumza na waandishi wa habari jijini jana, mawakili hao walisema wametafakari na kuona wakiwa nje ya kesi hizo, maslahi yao hayatalindwa vyema.

Kamati ya uchaguzi ya TLS ilipitisha majina matano ya wagombea wa nafasi ya urais kwa ajili ya uchaguzi wa baadaye mwezi huu. Wengine ni Francis Mtola, Victoria Mandari na Godwin Mwapongo.

Kwa mujibu wa Lissu, walalamikiwa katika kesi hizo ni TLS na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), na kwamba kesi ya Dar es Salaam ilifunguliwa na Onesmo Mpinzile na ya Dodoma imefunguliwa na Godfrey Wasonga.


Mpenzile na Wasonga wameomba Mahakama Kuu kutoa amri ya kuzuia uchaguzi huo kufanyika, kwa mujibu wa Lissu, katika kesi ya Dodoma kwa madai kuwa kanuni za sheria ya TLS ya mwaka 1954 hazijasajiliwa.

“Tuna wasiwasi kuna njama dhidi ya TLS, tunahofu TLS na AG hawatajitetea bali watakubali mashtaka ili uchaguzi usifanyike na maslahi yetu yatavurugwa," alisema Lissu.

"Leo (jana) na Machi 13 tutapeleka maombi yetu masjala ya Mahakama Kuu za Dodoma na Dar es Salaam ili tuunganshwe kwenye kesi kama wadaiwa ili kusiwe na njama za uongozi uliopo kuendelea kuongoza au wanaotaka kuvuruga TLS wakafanikiwa.

"(Tutaomba) tuwe sehemu ya walalamikiwa ili masuala ya uchaguzi huu yasije yakaamuliwa nyuma ya migongo yetu au juu ya vichwa vyetu, tuwe na fursa kamili kuiambia mahakama kwanini maombi ya kuzia hayana mbele wala nyuma.”

Lissu ambaye ni Mwanasheri Mkuu wa Chama cha Maendeleo na Demokrasia (Chadema), alielezea kushangazwa na uamuzi wa mawakili hao kufungua kesi hiyo, licha ya Wasonga kuwa mmoja wa wagombea wa Baraza Kuu la TLS.

KUENDESHA TLS:

Lissu alisema mawakili hao wanapiga sheria zinazotumika kuendesha TLS kwamba kanuni zake hazikusainiwa na rais baada ya kutoka katika gazeti la serikali.

Lakini, alisema, matakwa ya kisheria hayalazimishi mawakili kufanya hivyo bali Baraza Kuu kupitisha kanuni hizo.

“Tunashindwa kuelewa mawakili wenzetu walisukumwa na dhamira gani kufungua kesi hiyo, kwa kuwa wamefanya hivyo wiki mbili baada ya muda wa kuchukua na kurejesha fomu kwisha,” alisema Lissu ambaye ni Mbunge wa Singida Mashariki.

“Majina yetu yameshapitishwa na kamati ya uteuzi hivyo hatuhitaji baraka za Dk. John Magufuli, Dk. Harrison Mwakyembe wala mtu yeyote.

"Baraka za kamati zimetosha na wiki ijayo (Machi 18) tunaenda kuwaomba wanachama ambao wao ndiyo waamuzi wa nani awe rais.

Wizara ya Sheria na Katiba ilisema mapema wiki hii kuwa haitokubali viongozi wa TLS kuwa na kofia mbili, ikiwamo uongozi wa kisiasa, ili kuepusha mgongano wa maslahi.

Taarifa ya Wizari wa Sheria na Katiba iliyotolewa katika akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Facebook, ilisema Waziri Dk. Harrison Mwakyembe alitoa msimamo huo mjini Dodoma.

Taarifa hiyo ilisema zaidi kuwa Waziri Mwakyembe alikuwa akizungumza na viongozi wa TLS wakiongozwa na rais wa sasa chama hicho, John Seka.

Taarifa hiyo ilionekana kuzuia uwezekano wa Lissu kuchaguliwa kuwa rais wa TLS kutokana na nyadhifa alizonazo Chadema.

Lakini akizungumza jana, Lissu alisema matakwa ya kisheria ya wagombea wa chama hicho ni wakili wa kujitegemea kuwa mwanachama kwa zaidi ya miaka 10, mwenye sifa zote, aliyelipa ada za uwakili, mlipa kodi za serikali na mwenye leseni ya biashara na siyo wadhifa wowote kwenye siasa.

Alisema amekuwa mwanachama wa TLS kwa zaidi ya miaka 10 na kuona ana sifa ya kugombea.

“Hakuna mgombea ndani ya TLS anayeulizwa itikadi zake bali sifa zilizopo kikatiba, na hakuna anayepimwa uwezo wake kuwa kuwa kiongozi wa kisiasa au nafasi nyinginezo.

"Matamshi yao yako nje ya kanuni, sheria ya mwaka 1954 na taratibu za chama chetu na sisi hatutakubali kuona ufinyangaji huu ukiendelea.”

Source: Nipashe
Tundu Lissu [CHADEMA] 'anunua' kesi nzito Tundu Lissu [CHADEMA] 'anunua' kesi nzito Reviewed by Zero Degree on 3/10/2017 01:54:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.