Loading...

Ukata wasababisha aliyekuwa Mkurugenzi wa Ufundi Yanga, Hans van de Pluijm kutimuliwa kazi

IKIWA ni siku wiki moja tangu ilipopokea kipigo cha bao 2-1 kutoka kwa mahasimu wao, Simba, Uongozi wa Yanga umemfuta kazi Mkurugenzi wake wa Ufundi, Hans van de Pluijm.

Taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo zimeeleza uongozi umefikia hatua hiyo kutokana na hali mbaya ya fedha inayowakabili kwa sasa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Pluijm, alikili kupewa taarifa ya kufutwa kazi na uongozi wa klabu hiyo na kukabidhiwa barua yake.

“Leo (jana) nimeitwa na Katibu Mkuu wa klabu (Charles Mkwasa) akaniambia kutokana na hali mbaya ya kifedha ya klabu kwa sasa hawawezi kuendelea na mimi wamenipa barua yangu," alisema Pluijm.

Alisema pamoja na kufutwa kazi, ana madai yake ya msingi na atakaa na uongozi kuona namna ya kumlipa stahiki zake.

“Sina wasiwasi nao, nitakaa nao na kuzungumza namna ya kunilipa kile ninachostahili kulipwa," alisema Pluijm.

Pamoja na kukili kupewa barua hiyo, Pluijm amesikitika kwa kitendo kilichofanywa na uongozi wa klabu hiyo na kwa kushindwa kumshirikisha kwenye maamuzi hayo.

“Nimefanya kazi Yanga kwa muda mrefu sana, nimekuwa Yanga katika wakati mzuri, na hili lililotokea sasa kila mtu anajua, wangenishirikisha kwanza, binafsi nilikuwa tayari kuvumilia," aliongeza kusema Pluijm.

Alisema Yanga ipo moyoni mwake na siku yoyote yupo tayari kurejea nchini kuifundisha.

Kwa upande wake, Mkwasa, aliliambia gazeti hili jana kuwa uongozi wa klabu hiyo utatoa taarifa yake baada ya mchezo wao wa Jumapili dhidi ya Mtibwa Sugar.

"Kwa sasa tupo bize na maandalizi ya mchezo wetu wa Jumapili, klabu itatoa taarifa na maelezo yote mara baada ya mchezo wetu ujao, kwa sasa ni ngumu kuanza kulizungumzia hilo wakati tuna mchezo muhimu mbele yetu," alisema Mkwasa.

Yanga ilimhamishia Pluijm kwenye Ukurugenzi wa Ufundi Novemba mwaka jana baada ya kumleta Kocha Mzambia, George Lwandamina kuchukua nafasi ya Pluijm.

Pluijm amefundisha Yanga kwa awamu mbili tangu mwaka 2014 alipoanza kwa kufanya kazi kwa nusu msimu, akimpokea Mholanzi mwenzake, Ernie Brandts kabla ya kwenda Uarabuni.

Alikwenda Al Shoalah FC ya Saudi ya Arabia na nafasi yake ikachukuliwa na Mbrazil, Marcio Maximo ambaye naye alifanya kazi kwa nusu msimu kabla ya Pluijm kurejeshwa Januari mwaka jana.

Kabla ya kuhamishiwa kwenye Ukurugenzi wa Ufundi, Pluijm aliiongoza Yanga kucheza michezo 128, akishinda 80, sare 25 na kufungwa michezo 23.

Msimu uliopita Pluijm aliongoza Yanga kubeba mataji yote matatu, Ngao ya Jamii, Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Kombe la Azam Sports Federation (ASFC).

Pluijm pia aliiwezesha Yanga kufika hatua ya makundi ya michuano ya Afrika (Kombe la Shirikisho) kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1998 na mara ya pili kihistoria.
Ukata wasababisha aliyekuwa Mkurugenzi wa Ufundi Yanga, Hans van de Pluijm kutimuliwa kazi Ukata wasababisha aliyekuwa Mkurugenzi wa Ufundi Yanga, Hans van de Pluijm kutimuliwa kazi Reviewed by Zero Degree on 3/04/2017 12:29:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.