Loading...

Uteuzi wa Salma Kikwete kuwa mbunge wazua mjadala

Salma Kikwete
SIKU moja baada ya Rais Dk. John Magufuli kumteua mke wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Salma Kikwete kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mjadala mkali umeibuka kutokana na uteuzi wake.

Watu wa kada mbalimbali wakiwemo wasomi na wachambuzi wa masuala ya kisiasa, wameuchambua uteuzi huo kwa kuupinga na wengine kuupongeza.

Salma ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, akitokea Wilaya ya Lindi Mjini, amekuwa akitajwa kujitosa katika kinyang’anyiro cha ubunge Jimbo la Lindi Mjini, katika uchaguzi ujao.

Baadhi ya wachambuzi wanautazama uteuzi huo kama ni hatua ya kuimarisha uhusiano kati ya utawala wa Rais Mstaafu Jakaya Kikwete na utawala wake.

PROFESA MPANGALA

Akizungumzia uteuzi huo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ruaha (RUCO), Profesa Gaudence Mpangala, alisema ni kawaida katika mfumo wa kiutawala kwani kuna kulindana na kuendelezana.

“Mfumo wa kiutawala unajiendesha, watawala ni wale wale kama Magufuli, Kikwete na Mkapa bado wapo kwa hiyo kuna kulindana na kuendelezana,” alisema Profesa Mpangala.

Pia alisema azma ya Mama Salma kutaka ubunge ilianza siku nyingi tangu mumewe akiwa Rais, kwani alikuwa ananyemelea ubunge Lindi na wakati huo mtoto wake Ridhiwani akinyemelea Jimbo la Chalinze.

“Hizi ni siasa za kifamilia na zilijitokeza sana katika awamu ya nne. Ingawa Rais Dk. Magufuli aliliona hilo lakini amebanwa na Katiba kwa sababu alimwondoa Possi (Dk. Abdallah) kubalance jinsia,” alisema Prof. Mpangala.

BUTIKU

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku alisema alichokifanya Rais Dk. John Magufuli ni jambo jema na kwamba watu wasiunganishe uteuzi huo na Rais Mstaafu Jakaya Kikwete.

“Ni jambo jema, Rais (Magufuli) amefanya vizuri na watu wasimuunganishe na mumewe. Salma ana sifa zake binafsi na wala haihusiani na mume wake,” alisema Butiku.

BISIMBA

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Hellen Kijo Bisimba alisema uteuzi huo umemshusha daraja Salma Kikwete.

“Naona kama wamemshusha daraja huyu mama. Hiyo nafasi angepewa mwanamke mpya mwenye mawazo mapya na si kumpa mtu anayepaswa kupumzika.

“Kuchaguliwa kuwa mbunge ni kupoteza sifa, angepewa fursa ya kupumzika baada ya kazi kubwa aliyoifanya akiwa mke wa Rais,”alisema Dk. Bisimba.

RIDHIWANI

Mbunge wa Chalinze, Ridhiwan Kikwete aliweka katika ukurasa wake wa istagram na Facebook akisema mama yake (Salma) ni mwanamke wa shoka, kwani amewawezesha wasichana wengi kupata elimu.

Ridhiwani ambaye ni mtoto wa kwanza wa kiume wa Rais Mstaafu Kikwete, alisema mama yake amekuwa mtetezi wa haki za wanawake, hivyo anaamini atakwenda bungeni kuwezesha mapambano kuwa sheria rasmi.

“Umekuwa mtetezi wa haki za wanawake na usawa wa kijinsia, umewezesha wasichana kupata elimu. Wewe ni mwanamke wa shoka. Hongera sana kwa uteuzi. Imani sasa umepata sehemu ya kuwezesha mapambano kuwa sheria. Mungu akutangulie mama yangu. Hongera tena,” aliandika Ridhiwani.

KIBAMBA

Akizungumza na waandishi wa habari jana, mchambuzi wa masuala ya siasa, Deus Kibamba alisema uteuzi huo unadhihirisha wazi kwamba ni kuweka mahusiano baina ya awamu iliyopita na ya sasa.

“Nadhani ungewauliza wananchi wa kawaida wao ndio watazungumzia vizuri. Lakini kwa kifupi nadhani ni kuweka vizuri mahusiano ya awamu iliyopita na sasa lakini ni sahihi kikatiba.

“Kwa kifupi mama Salma ni mchapakazi, tulimwona akiwa pale WAMA aliendeleza harakati za wanawake vizuri,”alisema Kibamba.

DK. BANA

Naye Mhadhiri wa Siasa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Benson Bana, alisema haoni kama kuna ukakasi katika uteuzi huo kwa sababu hata katika nchi za nje wako wake wa marais walishawahi kuteuliwa kuwa mawaziri.

“Kila zama zina historia mimi sioni kama kuna tatizo na kuna mifano hai Rais Yoweri Museveni wa Uganda aliwahi kumteua mkewe Janeth kuwa waziri. Cha msingi aonyeshe uwezo katika kutumikia nafasi aliyoteuliwa,” alisema Dk. Bana.

Pia alisema Rais Dk. Magufuli ametumia vigezo stahiki kumteua kwa sababu amekuwa na harakati za kuwasaidia watoto wa kike nchini.

“Mama Salma akiwa Ikulu alianzisha taasisi ya WAMA (Wanawake na Maendeleo) ambayo ilijikita katika maendeleo ya watoto wa kike, ni jambo jema kwa nchi. Hivi karibuni pia alitunukiwa kuwa balozi mwema wa lugha ya Kiswahili na tusisahau ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa akiwakilisha Mkoa wa Lindi.

“Sidhani kama katika marais wengine waliopita kuna mke ambaye amewahi hata kuwa mjumbe wa NEC. Yeye ni raia wa Tanzania anayo haki ya kutumikia nafasi yoyote iwe ya kuchaguliwa au kuteuliwa,” alisema.

Hata hivyo mkazi wa Dar es Salaam, Nayera Bakalemwa, alishangazwa na uteuzi huo kwa madai kwamba haukutarajiwa na wengi katika karne hii kwa siasa za Tanzania.

“Zipo taarifa kwamba Regina Lowassa ambaye ni mke wa aliyekuwa mgombea urais wa Ukawa mwaka juzi, Edward Lowassa, alitaka kupewa ubunge wa viti maalumu lakini kwa busara na weledi alikataa uteuzi huo.

“Alikataa mamilioni ya mshahara wanayolipwa wabunge, alizikataa posho za vikao wanazolipwa wabunge, aliyakataa mamilioni ya fedha wanayopewa wabunge kama kiinua mgongo.
“Ni Watanzania wangapi hawana ajira na wana uwezo wa kumudu nafasi hii? Je, kwa cheo alichokuwa nacho kama ‘First lady’ hakikumtosha kiasi kwamba apewe nafasi nyingine?,” alihoji Bakalemwa.

JANET MUSEVEN

Juni mwaka jana Rais Yoweri Museveni wa Uganda, alimteua mkewe Janet kuwa Waziri wa Elimu na Michezo katika orodha mpya ya baraza la mawaziri alilotangaza.

Uteuzi huo uliwashangaza wachambuzi wa siasa ambao walisema Museveni ana ajenda ya kuweka familia yake katika siasa kwani tayari alimpandisha cheo mwanawe Muhoozi Kainerugaba na kuwa mkuu wa vikosi maalumu.

GRACA MACHEL

Mjane wa Rais wa Kwanza wa Msumbiji, Hayati Samora Machel (Graca), aliwahi kuwa mbunge na Waziri wa Elimu na Utamaduni akiwa mwanamke pekee wa kwanza kushika nafasi hiyo kubwa baada ya Msumbiji kupata uhuru wake mwaka 1975.

Licha ya hofu aliyokuwa nayo baada ya kuteuliwa, lakini kwa mafanikio makubwa alibadilisha hali ya elimu Msumbiji na kiwango cha watoto kwenda shule kiliongezeka mara dufu kutoka watoto 400,000 hadi 1,500,000.

Hata hivyo kifo cha mumewe kilikuwa ni pigo kubwa kwake na ilipofika mwaka 1989 alistaafu wadhifa wake wa uwaziri na kujishughulisha na shughuli za maendeleo ya jamii hasa watoto.

HILLARY CLINTON

Baada ya mumewe Bill Clinton kustaafu urais wa Marekani, Hillary alichaguliwa kuwa Seneta ambaye pia alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani ambapo mwaka jana alikuwa mwanamke wa kwanza kugombea urais nchini humo.

Seneta huyo wa zamani aliweka historia ya kuwa mwanamke wa kwanza kuteuliwa na chama kikubwa nchini humo cha Democrat kugombea urais ambapo alipambana na Rais wa sasa, Donald Trump wa Republican.

Uteuzi huo wa Salma ni wa kwanza katika historia ya Tanzania kwa kuwa mke wa kwanza wa Rais mstaafu kuteuliwa ubunge.

Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, alitajwa kuwa ni mmoja ya wana CCM watakaowania ubunge Jimbo la Lindi Mjini, lakini hakuweza kufanya hivyo licha ya kutakiwa na wana CCM wenzake.

Hata hivyo, mke huyo wa Rais mstaafu Kikwete anatajwa kuwa huenda akawania Jimbo la Lindi Mjini mwaka 2020.

Salma Kikwete anakuwa ni mbunge wa tisa wa kuteuliwa na Rais Magufuli katika nafasi zake 10 kwa mujibu wa Katiba ya nchi.

Hadi sasa wabunge walioteuliwa na Rais Magufuli ni Alhaji Abdallah Bulembo, Profesa Palamagamba Kabudi, Anne Malecela, Naibu Spika, Dk. Ackson Tulia, Waziri wa Mambo ya Nje, Dk. Augustino Mahiga, Profesa Makame Mbarawa (Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano), Profesa Joyce Ndalichako (Elimu)na Dk. Philip Mpango (Fedha na Mipango).

Source: Mtanzania
Uteuzi wa Salma Kikwete kuwa mbunge wazua mjadala Uteuzi wa Salma Kikwete kuwa mbunge wazua mjadala Reviewed by Zero Degree on 3/03/2017 10:54:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.