Loading...

Wanawake nchini Kenya watishia kutembea wakiwa uchi

WAKATI dunia ikiadhimisha Siku ya Wanawake leo, akina mama katika Kaunti ya Mombasa, wametishia kuandamana uchi iwapo Naibu Gavana, Hazel Katana, ataendelea kutoheshimiwa.

Wamesema Katana anakandamizwa na watu wasiojulikana walioko katika Serikali ya Kaunti ya Mombasa kwa vile ni mwanamke.
Zaidi ya kina mama 200 waliandamana juzi katika bustani ya Uhuru wakimtaka Rais Uhuru Kenyatta aingilie kati siasa za Mombasa.

“Katika kipindi hiki cha kuelekea Siku ya Kimataifa ya Wanawake, tutaandamana uchi wa mnyama, hatuwezi kukubali mama yetu aendelee kudharauliwa eti ameiba viti vilivyozeeka. Kama alikuwa anataka kuiba angeiba vitu vya maana,” alisema Asha Mwidani.

Walisema tangu mwenzao ajiengue kutoka Chama cha ODM na kwenda Jubilee ambako atawania kiti cha useneta, amekuwa akikumbwa na misukosuko na dharau kutoka kwa wafanyakazi wa kaunti kutokana na jinsia yake.

Wakibeba mabango yanayomtaja Katana, kina mama hao walisema wanasiasa wanawake wanapaswa kuheshimiwa na wanaume.
“Katana anapaswa kuheshimiwa kama viongozi wengine wa kiume. Kama gavana hayupo, Katana anapaswa kuchukua nafasi yake ya usimamizi wa shughuli za kaunti, lakini katika Serikali hii hilo ni ndoto,” alisema mama huyo mkazi wa Kingorani.

Alidai watu kadhaa katika kaunti hiyo ambao hakuwataja, walibeba viti kisha baadaye wanamlaumu Katana.

“Kiti anachokalia Katana ni moto sana, joto la siasa limejaa, siasa si uadui jamani. Tutatembea uchi mpaka kieleweke, iwe mara ya mwisho mama yetu kudhulumiwa,” aliongeza Fatuma Atemi.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa kaunti hiyo, Richard Chacha, alisema suala hilo linachunguzwa na vyombo vya usalama.
Wanawake nchini Kenya watishia kutembea wakiwa uchi Wanawake nchini Kenya watishia kutembea wakiwa uchi Reviewed by Zero Degree on 3/08/2017 12:23:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.