Loading...

Atupwa Jela miaka 4 baada ya kukutwa na hatia ya kufukua kaburi la albino Mbeya

Mahakama ya Wilaya ya Mbeya imewahukumu watu wawili kila mmoja kifungo cha miaka minne jela na kulipa faini ya Sh2.3 milioni baada ya kutiwa hatiani kwa kula njama na kufukua kaburi la marehemu aliyekuwa na ulemavu wa ngozi (albino).

Washtakiwa hao wakazi wa Mbalizi walifukua kaburi la Sister Sisara (38) aliyefariki dunia mwaka 2008 na kuzikwa katika Kijiji cha Mumba, Kata ya Ilembo wilayani Mbeya.

Hakimu Rashid Chaungu aliwataja washtakiwa hao kuwa ni Jonas John (28) na Hazore Ezekia (33).

Akitoa hukumu, Chaungu alisema Mahakama imeridhika na ushahidi wa upande wa mashtaka uliowasilisha mashahidi watano.

Alisema katika kosa la kwanza kila mshtakiwa atatumikia kifungo cha miaka miwili jela na kulipa faini ya Sh1 milioni.

“Katika shtaka la pili, kila mmoja atalipa faini ya Sh1 milioni na kutumikia kifungo cha miaka miwili jela. Kwa sababu ya maelezo ya mashahidi wa upande wa mashtaka mlisababisha usumbufu kwa familia, mtailipa Sh300,000 kila mmoja,” alisema Chaungu.

Awali, walipopewa fursa ya kujitetea kabla ya adhabu kutolewa, John alisema amelelewa katika mazingira ya uyatima na ana familia, hivyo aliomba asamehewe.

Ezekia alidai ni mgonjwa mwenye maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) na anatumia dawa za kufubaza makali ya virusi hivyo, na kuomba asamehewe.

Mwendesha mashtaka wa Serikali, Bernadetha Thomas aliiomba Mahakama kutoa adhabu kali kwa washtakiwa ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hizo.

Baada ya hukumu kutolewa, Mwenyekiti wa Chama cha Albino Tanzania (Tas), mikoa ya Songwe na Mbeya, Claud Mwakyoma aliiomba jamii ishirikiane na vyombo vya dola kuwafichua watu wenye imani potofu za kuamini kuwa viungo vya binadamu vinaleta utajiri badala yake wafanye kazi halali.

Bonventura Mwalongo ambaye ni mjumbe wa kamati ya kushughulikia changamoto za albino nchini, alisema chanzo cha matukio hayo ni ramli chonganishi zinazofanywa na baadhi ya waganga wa jadi.

Katibu wa Tas, William Simwali ambaye ni kaka wa marehemu Sisara, alisema Serikali inatakiwa kusimamia zuio la waganga wa jadi kujitangaza kwa kuweka mabango.
Atupwa Jela miaka 4 baada ya kukutwa na hatia ya kufukua kaburi la albino Mbeya Atupwa Jela miaka 4 baada ya kukutwa na hatia ya kufukua kaburi la albino Mbeya Reviewed by Zero Degree on 4/06/2017 11:04:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.