Loading...

Hatimaye Simba SC wamalizana na TRA

Hatimaye klabu ya Simba imetangaza kuwa tayari imelipa kodi iliyokuwa inadaiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) baada ya kuingiza nyasi bandia nchini ambazo zilikuwa zimeletwa kwa ajili ya kuwekwa katika uwanja wa Simba uliopo Bunju, Dar.

Simba imelipa Sh milioni 80 baada ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutaka kuzipiga mnada nyasi hizo kutokana na kukaa kwa muda mrefu bandarini bila kulipia kodi.

Nyasi hizo sasa zitatandikwa kwenye uwanja wao ulioko Bunju nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, ambao sasa utatumika kwa mazoezi na mashindano mbalimbali.

Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi, Richard Kayombo, jana alithibitisha kuwa Simba wamefanikiwa kulipa kiasi walichokuwa wanadaiwa.

Kayombo alisema viongozi wa klabu hiyo ya Simba walipewa siku 14 kuhakikisha wamelipa kiasi walichokuwa wakidaiwa kabla ya kuzipiga mnada.

“Awali tuliwapa siku 14 ambazo ziliisha jana, (juzi) lakini habari nzuri ni klabu hiyo kuweza kutimiza ahadi yake kwa kulipa deni tulilokuwa tunawadai kama ushuru,” alisema.

Alisema baada ya kulipa kiasi hicho taratibu nyingine zifuatwe pamoja na kuwaruhusu viongozi wa Simba kutoa nyasi hizo bandarini.

“Kikubwa wamelipa ila ni lini zitatoka kuna ‘process’ (taratibu) kadhaa ambazo zitafuatwa kabla ya kutoka rasmi ila jua tu tumemalizana na Simba kwa sasa.”

Katika taarifa ambayo imetolewa na Simba SC kupitia akaunti yake ya Instagram imesema tayari imelipa kodi na nyasi hizo kwa sasa zitapelekwa Bunju kwa ajili ya kuwekwa katika uwanja ambao itakuwa inautumia kufanya mazoezi.


Hatimaye Simba SC wamalizana na TRA Hatimaye Simba SC wamalizana na TRA Reviewed by Zero Degree on 4/06/2017 01:22:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.