Loading...

Hatimaye kamati ya saa 72 yatoa maamuzi kuhusiana na rufaa ya Simba kwa Kagera Sugar

Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi Tanzania, maarufu kama Kamati ya Saa 72 imeipa Simba SC pointi tatu na mabao matatu kutokana na rufaa waliyoikatia Kagera Sugar kwa kumtumia beki Mohammed Fakhi akiwa ana kadi tatu za njano katika mechi baina ya timu hizo Aprili 2, mwaka huu.

Katika mchezo huo ambao Kagera Sugar walishinda mabao 2-1 Uwanja wa Kaitaba, wanadaiwa kukiuka kanuni kwa kumchezesha Fakhi, beki wa zamani wa Simba badala ya mchezaji huyo kutumikia adhabu ya kadi tatu za njano alizopata mfululizo.



Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi, Ahmed Yahya amewaambia Waandishi wa Habari usiku wa April 13, 2017 kwamba Kamati ilibaini ni kweli Kagera Sugar walifanya kosa hilo la kikanuni na adhabu yake ni kupokonywa ushindi.

Kwa ushindi huo, Simba sasa inafikisha pointi 61 baada ya kucheza mechi 26, wakiendelea kuongoza Ligi Kuu Tanzania bara mbele ya mabingwa watetezi, Yanga wenye pointi 56 wakiwa wamecheza mechi 25.

Ikumbukwe Simba iliwasilisha malalamiko ikitaka ipewe ushindi wa pointi tatu na mabao matatu kutokana na Kagera Sugar kumchezesha Fakhi akiwa na kadi tatu za njano katika mechi yao namba 194 iliyofanyika Aprili 2, 2017 Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.

Katika kikao chake awali Ijumaa iliyopita, Kamati baada ya kupitia malalamiko hayo, iliahirisha shauri hilo hadi leo (April 13, 2017) kujipa muda wa kufuatilia baadhi ya vielelezo kuhusu malalamiko hayo.

“Malalamiko yaliletwa kwetu na timu ya Simba baada ya kufungwa na Kagera Sugar 2-1 kwenye uwanja wa Kaitaba, Simba walileta malalamiko kwamba kuna mchezaji mmoja wa Kagera Sugar Mohamed Fakhi alicheza mchezo huo wakati akiwa na kadi tatu za njano jambo ambalo ni kinyume na taratibu zetu kwa mujibu wa kanuni zetu za ligi,” alisema mwenyekiti wa kamati ya saa 72 wakati akitangaza uamuzi uliofikiwa na kamati yake.

“Tulikaa kikao cha kwanza siku ya tarehe 7 April, 2017 tukajadili, bahati mbaya siku hiyo hatukufanikiwa kufikia mwisho kwa sababu tulikuwa tunakosa baadhi ya taarifa ambazo zinaendana na maamuzi ambayo tungeweza kuyafanya kwa hiyo tulijipa muda hadi leo na tumefanikiwa kuzipata taarifa ambazo tulikuwa tunazitafuta na jioni hii tumefikia maamuzi.”

“Kutokana na nyaraka tulizonazo imethibitika kwamba, mchezaji huyu ambaye anaitwa Mohamed Fakhi alipata kadi ya njano kwenye mchezo kati ya Kagera Sugar na Mbeya City, akapata kadi nyingine ya njano kwenye mchezo kati ya Kagera Sugar na Majimaji na pia akapata kadi ya njano kwenye mchezo kati Kagera Sugar na African Lyon.”

“Baada ya kupata malalamiko haya, watu wa Kagera Sugar walikuja juu na kusema kwamba, mchezaji wao alipewa kadi kwenye mchezo kati ya Kagera Sugar na African Lyon na huo ndio utata uliotufanya tutafute ushahidi kuona kwamba hicho kitu kilitokea. Tumepata taarifa na kamati imeridhia kwamba hiki kitu kilitokea na kutokana na hilo, mchezaji huyo alikuwa nje ya sheria 37 (14) na adhabu yake ipo kwenye sheria yetu ambayo inasema kwamba (timu itakayotumia mchezaji ambaye ana kadi tatu za njano, basi itabatilishiwa matokeo na kunyang’anywa ushindi. Timu pinzani itapewa ushindi wa pointi na magoli matatu).”

Kwa hali hiyo, naomba nitangaze rasmi kwamba, kamati imefikia maamuzi hayo na taratibu zingine zitafuata kuhusiana na hilo.

Tumechukua muda mrefu kutoa maamuzi kwa sababu ya hali ilivyokuwa, kwamba upande wa pili walikuwa wanasema rekodi zao hazioneshi hivyo kwa hiyo ilibidi tutafute rekodi za ziada ndiyo maana tumechukua muda mrefu kutoa maamuzi ya suala hili. Vinginevyo tungetoa maamuzi siku ya tarehe 7 tulipopata malalamiko haya.
Hatimaye kamati ya saa 72 yatoa maamuzi kuhusiana na rufaa ya Simba kwa Kagera Sugar Hatimaye kamati ya saa 72 yatoa maamuzi kuhusiana na rufaa ya Simba kwa Kagera Sugar Reviewed by Zero Degree on 4/13/2017 11:34:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.