Loading...

Orijino Komedi bye bye!

Hatimaye kundi la vichekesho lililojipatia umaarufu mkubwa nchini la Orijino Komedi, limefikia mwisho kwa kusambaratika, huku chanzo kikidaiwa kuwa ni mmoja wa memba wake mwenye mbwembwe nyingi, Silvery Mujuni, maarufu kama Mpoki a.k.a Mwarabu wa Dubai.

Kwa mujibu wa chanzo kilicho karibu na kundi hilo ambalo halijarusha kazi zake hewani kwa muda mrefu sasa, limeingia katika hatua hiyo, baada ya mmoja wa memba wake, kukiuka makubaliano, kitu kilichosababisha wote waamue kufanya mambo kivyao.

Inadaiwa kuwa hapo awali, kulikuwa na maazimio ya kila mmoja kuleta kundini, makubaliano yoyote ya kazi kibiashara ili mapato yatakayopatikana, wagawane wote.

“Walijua kuwa kazi zao kama kundi ziliwavutia kampuni na mashirika, lakini wakafahamu pia kuwa wakati mwingine siyo rahisi kundi kuingia mikataba, kwamba wapo ambao wangeweza kuvutiwa na mmoja wao, hivyo ikitokea namna hiyo, basi aliyepata dili hilo, alilete kundini, ambako yeye atapewa asilimia kubwa, huku wenzake nao wakipata kidogokidogo,” kilisema chanzo hicho.

Chanzo hicho kikaongeza kuwa, utaratibu ukawa ni huo na kila kitu kikaonekana kwenda vizuri, hadi Mpoki alipokuja ‘kutibua’ baada ya kupata dili kutoka kampuni moja ya simu, lakini kwa mshangao wa wenzake, hakupeleka kundini makubaliano yake.

“Watu walishtukia tu tangazo linaruka hewani, alipoulizwa imekuaje, akawa haeleweki, ndipo wenzake nao wakaamua kila mmoja kufanya kivyake na hapo ndipo kutokuelewana kukatokea,” kilisema chanzo hicho.

Baada ya habari hizo kupatikana, Mpoki alitafutwa, ambaye kwa sasa ni mtangazaji katika Kituo cha Redio cha EFM, ambapo baada ya kuelezwa kuhusu tuhuma hizo, alihoji;

“Hayo maneno kakuambia nani? Pale kwenye kundi letu tupo wengi au wao ndiyo wamekuambia? Mimi siwezi kujibu hiyo kitu na huwezi kunilazimisha kujibu.”
Lucas Lazaro Mhuvile, anayefahamikazai di kama Joti, alitafutwa ambaye baada ya kuulizwa kuhusu kilichotokea kwenye kundi lao, mahojiano na mwandishi yalikuwa kama ifuatavyo;

Joti: Lazima uniambie kwanza ni nani aliyekuambia habari hizo.

Mwandishi: Lakini maadili ya kazi yetu hayaruhusu mimi kutaja chanzo changu, nadhani wewe ungejibu tu vile unavyojua juu ya jambo hilo.

Joti: Mimi siyo mwandishi, ninachotaka utuite mimi na yeye aliyekuambia hizi habari, tukae tuambizane vinginevyo siwezi kukujibu kwamba ni kweli au siyo kweli.

Mchekeshaji mwingine maarufu wa kundi hilo, Isaya Mwakilasa ‘Wakuvanga’ alitafutwa, ambaye baada ya kuelezwa kusudio la kupigiwa simu, alisema hivi; “Unataka nikupe habari hovyohovyo au unataka nikupe kitu kizuri uandike? (Mwandishi alipomweleza kuwa anahitaji kitu kizuri, akamwambia), basi nitafute wakati mwingine kwa sababu hivi sasa nipo katika kazi muhimu.”

Emmanuel Mgaya ‘Masanja Mkandamizaji’ hakupokea simu yake licha ya kupigiwa mara kadhaa na hata ujumbe mfupi wa simu hakujibu, kama ilivyokuwa kwa Mark Regan.

Hata hivyo, kiongozi wa kundi hilo, Sekioni David, maarufu kama Seki, alizungumza haya.

“Kundi bado lipo ila kwa sasa liko mapumzikoni. Unajua, shoo ya mwisho tulifanya Septemba 2015, baada ya pale tukaingia katika kampeni, ila kazi ni ngumu na pia tokea tumeanza, hatukuwahi kupumzika, watu wanatakiwa wapumzike ili wapate ubunifu mpya.

“Kifupi ni kuwa tupo likizo tangu ile 2015, nadhani tutaendelea mwishoni mwa mwaka huu, kwa hiyo mwakani kundi linarejea barabarani kama kawaida, hiyo habari kuwa tumesambaratika siyo kweli, hivi sasa watu wako mashambani wanashughulika na kilimo.”

Source: GPL
Orijino Komedi bye bye! Orijino Komedi bye bye! Reviewed by Zero Degree on 4/05/2017 01:43:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.