Loading...

Serikali yabaini udanganyifu uliofanywa na mawakala wa pembejeo

SERIKALI imebaini kwamba madai ya Sh bilioni 62 wanazodai mawakala waliosambaza pembejeo za ruzuku nchini yana udanganyifu mkubwa.

Serikali kupitia Hazina ilifikishiwa madai hayo na halmashauri kadhaa na kuyatilia shaka, hivyo ikaiagiza Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ifanye uhakiki kujiridhisha kama madeni hayo ni halali kabla ya kuwalipa.

Madeni hayo yalibainika baada ya Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), Mbunge wa Sumbawanga, Aeshi Hilaly kumuuliza Katibu wa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi lini wakala wa pembejeo za ruzuku itawalipa.

Akiieleza Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) inayoongozwa na Naghenjwa Kaboyoka, Katibu wa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Injinia Mathew Mtigumwe alisema Wizara imejiridhisha kwa kufanya uchunguzi na kubaini kwamba deni hilo la sh bilioni 62 lina udanganyifu.

Mtigumwe alisema katika uchunguzi wa awali katika mikoa 10 walibaini kuwa, asilimia 70 ya mawakala wa pembejeo, wamefanya udanganyifu wa zaidi ya Sh bilioni 14 na kazi haikufanyika na wengine hawakujitokeza kuhojiwa.

Akiahirisha Kikao cha Kamati baada ya kutangaziwa msiba wa Dk Macha, Mwenyekiti Kaboyoka aliwataka viongozi wa Wizara kufanya marekebisho ya mapendekezo yaliyotolewa na Mkaguzi na Mdhibiti wa Serikali (CAG) kuhusu upungufu uliojitokeza kwenye usambazaji wa pembejeo na kuipelekea Kamati marekebisho.

Katika hatua nyingine, Makamu wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), Hilaly alihoji Serikali ina mpango gani kuwalipa wakulima wa mikoa ya Rukwa na Katavi waliotumia mbegu zilizosambazwa na wakala na kuwasababishia hasara kwa kuwa hazikuota.

Mtigumwe alisema sheria za nchi pia zinawabana wazalishaji wa mbegu nchini, kutokana na kuwaruhusu wazalishaji wa nje ya nchi kuingiza mbegu nchini bila kodi.

Kaimu Mkurugenzi wa Utafiti na Maendeleo, Hussein Mansoor alisema wizara imejipanga kwa kuweka mipango ya kilimo awamu ya kwanza ambayo walishughulikia ujenzi wa maghala na skimu za umwagiliaji.
Serikali yabaini udanganyifu uliofanywa na mawakala wa pembejeo Serikali yabaini udanganyifu uliofanywa na mawakala wa pembejeo Reviewed by Zero Degree on 4/02/2017 02:53:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.