Loading...

Simba SC, TFF ni kizaa zaa

WAKATI uongozi wa Simba ukilitaka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kutothubutu kuwapokonya pointi tatu walizopewa na Kamati ya Saa 72 ya Usimamizi wa Ligi Kuu, wamelitaka shirikisho hilo kulishirikisha Jeshi la Polisi na Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA) ili kuhakiki taarifa za kamisaa wa mechi.

Akizungumza jana kwenye makao makuu ya klabu ya Simba, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano, Haji Manara, alisema kwa TFF kuhusisha mamlaka hizo za serikali, wanaamini klabu yao itatendewa haki kabla hali haijawa tofauti na ilivyo sasa wakati Ligi Kuu Tanzania Bara ikikaribia ukingoni. 

Manara alisema Simba imeshangazwa na kitendo cha TFF kuitisha kikao cha Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji wakati barua ya Kagera Sugar iliomba kufanyika kwa marejeo ya rufaa iliyokatwa na Wekundu wa Msimbazi.

"Hiki ni kiroja cha mwaka, Kagera iliomba hukumu iliyotolewa na Kamati ya Saa 72 ipitiwe upya, lakini badala ya chombo kile kile kukaa, tunaona kamati nyingine inaitishwa, kwenye marejeo huwezi kuleta ushahidi mpya, hii haipo kokote pale duniani, msimamo wetu Simba tunasema kile kikao (Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji) si halali, huku ni kuionea Simba kulikopitiliza," alilalamika Manara.

Alisema wanashangaa kuona shauri hili limechukua sura mpya baada ya mahasimu wao Yanga kutishia kwenda mahakamani wakati hakuna kikao kingine kilichowahi kufanyika mwaka 2006 Simba ilipopokonywa pointi kwa kumchezesha Mussa Hassan 'Mgosi' aliyekuwa na kadi tatu za njano sawa na Azam FC ilipopokonywa pointi kwa kumtumia beki wake, Erasto Nyoni msimu uliopita.

"Simba tunauhakika na ripoti ya kamisaa wa mchezo, tumepata taarifa kuwa suala hili wanataka kulipeleka katika kitengo cha makosa ya mtandaoni, waende lakini wakumbuke kamati hiyo hiyo imeshindwa kubaini hadi leo (jana) uamuzi kuhusu kesi ya mkataba wa Hassan Kessy tuliyoiwasilisha huu mwaka wa pili," Manara aliongeza.

Manara aliitaka pia serikali kuingilia kati namna baadhi ya viongozi wanavyoendesha soka kwa kuangalia 'mahaba' na klabu zao na kuacha kufuata kanuni na sheria zilizowekwa.

"Tunawapa hadi Jumatatu kiwe kimeeleweka, tunataka haki, sio itendeke, haki ionekane imetendeka," alisisitiza Manara.

Aliongeza kwa kuwataka TFF kuheshimu uamuzi uliotolewa na Kamati ya Saa 72 ambayo inaundwa na viongozi wa Bodi ya Ligi kwa sababu waliafiki kuipa Simba pointi tatu na mabao matatu kwa kuzingatia ripoti ya refa na kamisaa wa mchezo huo uliofanyika Januari 18 mwaka huu.

Source: Nipashe
Simba SC, TFF ni kizaa zaa Simba SC, TFF ni kizaa zaa Reviewed by Zero Degree on 4/20/2017 10:39:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.