Loading...

Standard Chartered, IPTL mahakamani kwa mara nyingine tena

MAHAKAMA Kuu Kitengo cha Biashara imezipa siku 21 benki mbili za Standard Chartered kuwasilisha hati zao kinzani kwenye maombi mawili yaliyowasilishwa mahakamani hapo na kampuni tatu za kitanzania kupinga malipo ya dola za Marekani 168, 800,063 (Sh bilioni 400) kwa benki hizo.

Amri hiyo ilitolewa na Msajili wa mahakama hiyo, Agustine Rwizile ambaye amezielekeza Standard Chartered Hong Kong Limited na Standard Chartered Malaysia Berhard hadi Aprili 24, mwaka huu ziwe zimeshawalisha hati zao kinzani kujibu hoja mbalimbali ikiwemo ya udanganyifu iliyodaiwa kufanywa na benki hizo ili kupata hukumu iliyowapendelea.

Kampuni zinazohusika kwenye shauri hilo ambazo zinapinga benki hizo kulipwa ni Independent Power Tanzania Limited (IPTL), Pan African Power Solutions Tanzania Ltd (PAP) na VIP Engineering and Marketing Limited (VIP).

Msajili ameamuru shauri hilo litajwe Mei 30, mwaka huu kwa maelekezo mengine ambayo kampuni hizo ya kizalendo nazo zitatakiwa kujibu hoja zitakazoletwa na benki hizo kabla ya Mei 8, mwaka huu.

Katika maombi ya kampuni hizo yaliyowasilishwa mahakamani hapo, kampuni hizo zinaomba mahakama kutengua amri iliyotolewa Februari 9, 2017, kusajili hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu ya Malkia Uingereza, Idara ya Mahakama ya Biashara, Novemba 16, 2016 juu ya malipo hayo.

Mawakili Joseph Makandege wa IPTL na PAP na Respicius Didace wa VIP wamewasilisha mahakamani hapo hati ya viapo kuunga mkono maombi hayo na kueleza kuwa hukumu hiyo ya kigeni ilipatikana kwa udanganyifu, hivyo utekelezaji wake itakuwa ni kinyume na Sera za Umma za Tanzania.

Wameeleza kuwa Benki ya Standard Chartered Hong Kong Limited walijifanya kama mdai wa IPTL na wenye haki na mkataba wa uuzaji wa umeme na hivyo kwa kupitia udanganyifu huo, walipata hukumu iliyotolewa na mahakama hiyo ya Uingereza.

Hukumu hiyo iliyotolewa na Jaji Julian Flaux baada ya kusikiliza upande mmoja inazinufaisha benki hizo mbili. Kampuni hizo zinaomba mahakama itamke kuwa hukumu ya kigeni iliyosajiliwa mbele ya Jaji Barke Sahel wa Mahakama Kuu ya Tanzania (Kitengo cha Biashara) haisajiliki na wala haitekelezeki nchini Tanzania.

Kwa mujibu wa mawakili hao, utekelezaji wa hukumu hiyo inalenga kufuta kesi mbalimbali zinazoendelea mahakamani hapa Tanzania, ikiwa ni pamoja na kesi namba 229 ya mwaka 2013 na kesi namba 60 ya mwaka 2014, ambayo waombaji wanahoji nafasi ya benki hiyo katika kufungua kesi huko Uingereza.

Wameeleza kuwa hukumu hiyo ya kigeni sio hukumu ambayo imesajiliwa kwa kuzingatia masharti ya sheria inayoshughulikia usajili wa hukumu za nje na kwamba hapakuwepo na uzingatiaji wa mambo yote ilivyotajwa katika sheria hiyo na katika Sheria ya Mwenendo wa masahauri ya madai.

Inaelezwa katika hati za viapo kwamba Mahakama ya Uingereza haikuwa na mamlaka juu ya kushugulikia mgogoro wa IPTL kwa vile mitambo hiyo ipo Tanzania na mambo mengine yanayohusu kampuni hiyo yapo hapa nchini.

Februari 9, mwaka huu, Jaji Sahel alitoa siku 21 kwa IPTL, PAP na VIP Engineering and Marketing Limited kuwasilisha kama wana pingamizi lolote juu ya kusajiliwa kwa hukumu hiyo.

Hukumu hiyo ilitolewa na Mahakama ya Uingereza kwa upande mmoja baada ya kapuni hizo tatu za Kitanzania kugoma kuwasilisha utetezi wao kwa vile walikuwa hawatambui mamlaka ya mahakama hiyo kushughulikia mgogoro wa IPTL.

Source: Habari Leo
Standard Chartered, IPTL mahakamani kwa mara nyingine tena Standard Chartered, IPTL mahakamani kwa mara nyingine tena Reviewed by Zero Degree on 4/06/2017 01:43:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.