Loading...

Watanzania wawili wateuliwa kushika nyadhifa kwenye Sekretarieti ya EAC

MAWAZIRI wa Jumuiya ya Afrika Mashariki(EAC) wamechagua wafanyakazi 31 kutoka nchi za Afrika Mashariki wakiwemo Watanzania wawili kushika nyadhifa mbalimbali kwenye Sekretarieti ya Jumuiya hiyo.

Katika mkutano wa 35 wa Jumuiya hiyo uliofanyika Makao Makuu ya EAC Arusha, Tanzania kati ya Machi 30 na Aprili 4, mwaka huu pia walichaguliwa wafanyakazi watatu wa Bunge la Afrika Mashariki(EALA)na mmoja wa Mahakama ya Afrika (EACJ).

Jumuiya pia imeteua pia maofisa wanne kwa ajili ya Tume ya Bonde la Ziwa Victoria na kila ofisa mmoja atakwenda kwenye Tume ya Sayansi na Teknolojia ya Afrika Mashariki na Tume ya Utafiti wa Afya ya Afrika Mashariki.

Uteuzi huo wa sekretarieti ni sehemu ya hatua ya kukabiliana na upungufu wa wafanyakazi uliotokana na kuondoka kwa wafanyakazi 26 waliostaafu ama kwa mujibu wa sheria ya kufikisha miaka 60 au kumalizika muda wa mikataba yao.

Uteuzi huo ulifanyika baada ya kufanyika usaili ulioendeshwa na EAC Ad Hoc Service Commission ambayo huchukua makamishna kutoka Tume za Utumishi wa Umma za nchi wanachama. Miongoni mwa walioteuliwa ni Kenneth Bagamuhunda kama Mkurugenzi Mkuu wa Biashara na Forodha na anachukua nafasi iliyoachwa na Peter Kiguta aliyestaafu Desemba Mosi, mwaka jana.

Awali Bagamuhunda alikuwa Mkurugenzi wa Forodha wa sekretarieti. Kamugisha Kazaura ndiye Mkurugenzi mpya wa Miundombinu nafasi iliyoachwa na Philip Wambugu ambaye mkataba wake umekwisha muda tangu Februari Mosi, mwaka huu.

Mkurugenzi mpya wa Rasilimali watu na Utawala ni Ruth Simba akichukua nafasi iliyoachwa na Joseph Ochwada aliyeondoka katika Sekretarieti Machi 19, mwaka huu.

Simba alikuwa Ofisa Mkuu wa Rasilimali Watu. Kazaura na Simba ni watanzania. Wafanyakazi wa EAC ambao ni wataalamu huajiriwa kwa awamu ya miaka mitano, mbadala hufanyika mara moja chini ya kustaafu kwa mujibu wa umri ambao ni miaka 60. Taarifa ya Jumuiya hiyo ilisema uteuzi huo umeanza mara moja kuanzia Aprili 4, mwaka huu.
Watanzania wawili wateuliwa kushika nyadhifa kwenye Sekretarieti ya EAC Watanzania wawili wateuliwa kushika nyadhifa kwenye Sekretarieti ya EAC Reviewed by Zero Degree on 4/09/2017 06:24:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.