Loading...

Watumishi watatu mbaroni kwa tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka Mkoani Kigoma

POLISI mkoani Kigoma imewakamata na kuwahoji watumishi watatu wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji kwa tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka, ubadhirifu wa fedha za halmashauri hiyo na kughushi nyaraka kwa niaba ya kujipatia fedha isivyo halali.

Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kigoma, Obadia Jonas alisema jana kuwa watu hao watatu waliokamatwa ni miongozi mwa watumishi sita wa halmashauri hiyo wanaotuhumiwa kwa matumizi mabaya ya madaraka na kughushi nyaraka, na kujipatia fedha isivyo halali kiasi cha Sh milioni 50.9 za Mfuko wa Barabara.

Aliwataja watumishi waliokamatwa na kuhojiwa kuwa ni aliyekuwa Mhandisi wa Maji, Sultani Ndoliwa, Mhandisi wa Ujenzi, Boniface William na Mhandisi Msaidizi wa Manispaa hiyo, Wilfred Shimba ambao walikamatwa Jumamosi na kufikishwa Kituo Kikuu cha Polisi mjini Kigoma ambako walihojiwa na kuachiwa kwa dhamana.

Aidha, Kaimu Kamanda aliwataja watumishi ambao hawajapatikana na wanatafutwa kuwa ni aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Boniface Nyambele, aliyekuwa Mtunza Hazina wa manispaa, Michael Marco na aliyekuwa Mtunza fedha wa halmashauri hiyo, Christina Nyumaihunzi.

Jonas alisema pamoja na kwamba watumishi hao watatu hawajakamatwa, Polisi inaendelea kuwatafuta ili wahojiwa na taratibu nyingine za kisheria ziendelee.

Awali, akitoa taarifa ya kikao cha Kamati ya Maadili ya Halmashauri kwa wajumbe wa Baraza la Dharura la Madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji, Katibu Muhtasi wa baraza hilo, Mussa Ahmadi alidai watumishi hao wanatuhumiwa kwa ubadhirifu na matumizi yasiyo sahihi ya zaidi ya Sh bilioni 1.2 za miradi mbalimbali.

Alitaja maeneo ambayo ubadhirifu huo ulifanyika kuwa ni pamoja na kiasi cha Sh bilioni 1.1 za Mfuko wa Barabara ambazo matumizi yake na vielelezo vyake haviwiani, huku kiasi cha Sh milioni 91 zilizopelekwa hospitali teule ya Baptist zikionesha kutopokelewa hospitalini.

Aidha, taarifa hiyo ambayo inatokana na taarifa ya Mkaguzi wa Ndani inabainisha kuwa katika mlolongo huo kunaonesha kuwepo kwa matumizi yasiyo sahihi ya Sh milioni 83 za Mfuko wa Pamoja wa Afya, na Sh milioni 48 za retention za mradi wa maji zilizochukuliwa bila kuwepo kwa taarifa yoyote ya matumizi ya fedha hizo.

Katika taarifa hiyo imeelezwa kuwa kiasi cha Sh milioni 50 za Mfuko wa Barabara zilipaswa kuingizwa kwenye Mfuko wa Amana wa halmashauri zilichukuliwa fedha taslimu baada ya watumishi waliohusika kuchukua fedha hizo kutoka katika hundi iliyokuwa imefungwa.

Baada ya kuwasilishwa kwenye kikao cha Baraza la Madiwani kwa taarifa hiyo, wajumbe waliipitia na kuidhia kuchukuliwa hatua mbalimbali kwa watumishi waliohusika sambamba na kuridhia kuchukuliwa hatua ya kufikishwa kwenye vyombo vya sheria kwa watumishi walioonekana kufoji nyaraka.

Akifunga kikao cha Baraza la Madiwani la Manispaa ya Kigoma Ujiji, Meya wa manispaa hiyo, Hussein Ruhava alisema madiwani hawatavumilia kuona watumishi wakifanya ubadhirifu bila woga na kurudisha nyuma mipango ya maendeleo ya halmashauri hiyo.
Watumishi watatu mbaroni kwa tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka Mkoani Kigoma Watumishi watatu mbaroni kwa tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka  Mkoani Kigoma Reviewed by Zero Degree on 4/11/2017 04:15:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.