Loading...

Mdee alivyowakoroga wabunge wa CCM Bungeni

WABUNGE watatu wa Chama Cha Mapinduzi na waziri walilazimika kusimama bungeni jana na kumkatisha Halima Mdee (Chadema) kuchangia mjadala wa bajeti baada Mbunge wa Kawe (Chadema) kuwatuhumu kusifia kile alichokiita ‘bajeti hewa' ya kilimo.

Mvutano huo uliibuka wakati Mdee alipokuwa akichangia mjadala bungeni mjini hapa kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka ujao wa fedha.

Katika mchango wake, mbunge huyo aliwataka wabunge aliowaita wapya kuwasaidia wananchi ambao asilimia 75 wanategemea kilimo badala ya kutoa pongezi kwa serikali kufuta tozo 108.


“Mnasema kuwa mmefuta tozo mbalimbali badala ya kutuambia mna mkakati gani wa kuwasaidia wananchi. Tungewekeza katika kilimo, ajenda isingekuwa kuondoa tozo,” alisema. 

Kutokana na kauli hiyo, Mbunge wa Mlalo, Rashid Shangazi (CCM), alisimama na kuomba kumpa taarifa mbunge huyo wa upinzani akieleza kuwa wabunge wote walioko bungeni ni wapya kwakuwa walichaguliwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 na kuapa mwaka huo huo.

Hata hivyo, Mdee hakuwa tayari kuipokea taarifa hiyo alipopewa ruhusa ya kuendelea kuchangia, lakini akawakoroga tena wabunge wa chama tawala kwa kusema kuwa yeye ni mbunge wa jimbo la mjini na analazimika kuyasema hayo kwa sababu wapigakura wake wanaathirika na mfumuko wa bei.

Alisema serikali imewaahidi Watanzania kuwa kilimo kitakuwa kwa asilimia 10, lakini ukuaji wa sekta hiyo umekuwa ukipungua mwaka hadi mwaka.

Alisema serikali katika mwaka wa fedha 2016/17, imetoa Sh. bilioni 3.3, sawa na asilimia 3.31 ya bajeti ya maendeleo Sh. bilioni 101 zilizoidhinishwa na Bunge kwa ajili ya sekta ya kilimo.

Baada ya kauli hiyo ya kuilaumu serikali kwa kutotekeleza ipasavyo bajeti, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Stela Manyanya, ambaye jana alikaimu nafasi ya Mnadhimu wa Serikali Bungeni, alisema malalamiko ya mbunge huyo hayana mashiko.

“Kama alivyosema, yeye ni mbunge wa mjini na wabunge wa vijijini wanatambua kero za wananchi wao… asiingilie uchangiaji wao,” alisema. 

Hata hivyo, Mdee ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Fedha na Mipango, alisema anachokisema ni kwa nia njema ya kuishauri serikali kwa manufaa ya taifa.

“Nimesoma bajeti ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji, fedha iliyotolewa ni Sh. bilioni nane tu na Tume ya Umwagiliaji ina wajibu wa kueneza miundombinu ya umwagiliaji nchini," alisema. 

Kauli hiyo ya Mdee ilimuibua Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Isack Kamwelwe, ambaye alisimama na kuomba kumpa taarifa mbunge huyo kuwa pamoja na serikali kutoa kiasi hicho kidogo cha fedha kwa ajili ya miradi ya umwagiliaji, wafadhili mbalimbali pia wametoa Sh. bilioni 43 kwa ajili ya miradi hiyo.

Alisema ujenzi wa miradi hiyo unaendelea katika maeneo mbalimbali nchini.

UVUMILIVU BUNGENI

Baada ya taarifa hiyo, Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), alisimama na kuomba mwongozo wa Kiti cha Spika, akitaka wabunge wawe wavumilivu wakati wabunge wenye mawazo tofauti na yao wanapochangia.

Alikosoa kitendo cha wabunge wa CCM na waziri kusimama bungeni kumkatisha Mdee kuzungumza kwa hoja ambazo alisema zinapaswa kujibiwa na mawaziri wakati wa kuhitimisha hoja husika katika mjadala huo na siyo wabunge.

Akijibu mwongozo huo, Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge, aliyeongoza kikao cha jana, alisema kanuni za Bunge zinaruhusu mbunge kupewa taarifa na wabunge wenzake huku akikiri kuwa yeye pia haupendi utaratibu huo.

Baada ya hapo, Mdee aliruhusiwa kuendelea kuchangia huku Kiti cha Spika kikiahidi kulinda muda wake, lakini Mbunge wa Newala, Kepteni Mstaafu George Mkuchika (CCM), akasimama na kutoa taarifa kuwa anachofahamu katika Bunge hilo hakuna mbunge wa mjini wala wa shamba bali wote ni sawa.

Kauli hiyo ya Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge (Mkuchika) iliibua maneno toka kwa baadhi ya wabunge waliozungumza bila idhini ya Kiti cha Spika.

Akiendelea kuchangia mjadala huo, Mdee alisema anawashauri wabunge wapya na wa zamani wakasome Ilani ya CCM ambayo hata yeye anaisoma.

Huku akiionyesha Ilani hiyo, Mdee alisema: "Mkasome Ilani yenu, haya ninayoshauri ni kwa mafanikio yenu na taifa. Mimi naisoma Ilani yenu pia,”alisema Mdee.

Alisema kuwa katika bajeti, serikali imekuwa ikitenga asilimia moja kwa ajili ya utafiti, lakini fedha hiyo haitoki.

Aliongeza kuwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, alisema jumla ya viwanda 234 vimejengwa, lakini ukweli ni kwamba vingi havijaanza bali vimesajiliwa na karibu robo tatu ya viwanda hivyo viko jijini Dar es Salaam.


“Tunasema kuwa hakuna viwanda bila malighafi lakini robo tatu viko Dar es Salaam. Ukienda kuangalia unaweza kucheka ufe mbavu, havina hadhi," alisema. 

“Huko mnapolima pamba, hamko katika mipango ya serikali, hakuna viwanda vilivyojengwa. Kama tungeweza kuweka miundombinu mizuri na pembejeo, tozo siyo 'issue' (siyo kitu). 

"Serikali ni moja lakini iweje leo ukisoma bajeti ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji na ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi hazioani?
Mdee alivyowakoroga wabunge wa CCM Bungeni Mdee alivyowakoroga wabunge wa CCM Bungeni Reviewed by Zero Degree on 5/21/2017 10:58:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.