Loading...

Abiria wanaopanda bodaboda bila helmet sasa kulipa faini au kwenda jela


ABIRIA wanaopanda bodaboda bila kuvaa kofia ngumu (helmet) wameonywa kuwa wakibambwa wakiwa katika hali hiyo watakumbana na mkono wa sheria ikiwamo kutozwa faini au kushtakiwa mahakamani.

Onyo hilo limetolewa na Jeshi la Polisi nchini kupitia kikosi cha Usalama Barabarani huku abiria hao wakitakiwa kuwa makini wanapopanda vyombo hivyo na ikiwezekana wanunue kofia zao kuepukana na zahama hiyo.

Wakati likitoa onyo, jeshi hilo limesema kwa Dar es Salaam pekee kuanzia Juni 5 hadi 14, mwaka huu, limekamata bodaboda 2,477 kutokana na makosa mbalimbali, ikiwamo kupita kwenye taa nyekundu, kubeba zaidi ya abiria mmoja maarufu kama mshikaki, kutovaa kofia ngumu na ubovu wa bodaboda.

Kaimu Kamanda wa Kikosi hicho, Fortunatus Musilimu, alisema jana alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu takwimu za makosa mbalimbali ya barabarani, ukaguzi wa magari ya shule nchini na hatua zilizochukuliwa.

Alisema kati ya makosa hayo ambao hawakuvaa kofia ngumu ni 1,221, bodaboda mbovu 283, waliopita kwenye taa nyekundu 387 na waliobeba mishikaki walikuwa 291.

Alisema madereva 77 kati ya walioofanya makosa hayo waliwekwa rumande na kupelekwa mahakamani wakiwamo abiria 129 ambao hawakuvaa kofia ngumu.

“Waliokamatwa waliwekwa mahabusu na walipotoka walitozwa faini na wakitoka abiria na dereva, walikwenda kununua kofia ngumu na wanatuletea risiti tunaihakiki, ili abiria aondoke nayo kofia nyumbani kwake na siku nyingine akienda barabarani abebe kofia yake,” alisema Musilimu. 

UKAGUZI MAGARI YA SHULE

Musilimu alisema hadi jana jeshi hilo limeshakutana na wamiliki wa shule na kufanya vikao mara mbili, ili kujadili hali ya usalama wa magari wanayotumia kusafirisha wanafunzi kutoka na kwenda maeneo tofauti.

Alisema mikakati ambayo imewekwa na jeshi ni kuendelea kuweka alama za usalama barabarani katika maeneo tofauti, ili kuwasaidia watumiaji wa barabara hususan madereva na wachukue tahadhari kulingana na alama zinavyoelekeza.

Alisema ukaguzi wa magari 1,683 ambayo hutumika kusafirisha wanafunzi katika mikoa mbalimbali nchini ikiwamo Dodoma, Arusha, Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya na Kilimanjaro, magari 538 yalibainika mabovu.

Alisema ilibainika madereva ambao hawana leseni stahiki ni 268 na waliokuwa na leseni stahiki ni 1,365 huku magari yanayomilikiwa na shule ni 1,226 na yanayokodiwa ni 472.

“Watoto ni kundi maalumu katika jamii ambao wanalindwa na sheria ya mtoto kwamba wanahitaji kuwa salama mahali popote hata katika usafiri. Wazazi na walezi wafuatilie hali ya usafiri wanaoutumia watoto wao na si kulipa ada tu,” alisema Musilimu. 

Alionya kuwa magari ya shule ambayo yanajaza wanafunzi kuliko uwezo wa gari, yataendelea kukamatwa.
Abiria wanaopanda bodaboda bila helmet sasa kulipa faini au kwenda jela Abiria wanaopanda bodaboda bila helmet sasa kulipa faini au kwenda jela Reviewed by Zero Degree on 6/18/2017 09:41:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.