Loading...

Bajeti ya pili ya serikali ya awamu 5 kwa mwaka wa fedha 2017/2018.


Huku akikatishwa kila mara na wabunge waliokuwa wakimshangilia mfululizo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, alitangaza rasmi makadirio ya mapato na matumizi ya serikali kwa mwaka ujao wa fedha takribani Sh. trilioni 32 huku akitangaza hatua kadhaa zinazoonekana kuwa na lengo la kutoa nafuu ya maisha kwa wananchi wa kawaida.

Aidha, bajeti hiyo iliashiria pia kuwapo kwa matumaini makubwa ya kuongezeka kwa mapato yatokanayo na kodi, hiyo ikitokana na vyanzo mbalimbali vipya vilivyoainishwa na pia kuwapo kwa mabadiliko kadhaa ya sheria za kodi na ile ya Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa.

Miongoni mwa yale yaliyoelekea kuwakuna wabunge wengi na hivyo kumlazimu Spika John Ndugai alazimike kuwatuliza kila mara ili kumpa fursa Waziri Mpango aendelee kuwasilisha bajeti hiyo ni pamoja na hatua ya serikali ni pamoja na kupunguza kiwango cha ushuru wa mazao ya chakula na biashara;

kuondoa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) katika vyakula vya mifugo; kutoza VAT kwa kiwango cha asilimia sifuri kwenye usafirishaji wa bidhaa na mizigo nje ya nchi zinazopita nchini ili bandari zetu ziwe bora kwa usafirishaji bidhaa nje ya nchi na pia kusamehe VAT kwenye bidhaa za mtaji.

Maeneo mengine yenye kuashiria nafuu kubwa kwa wananchi wa kawaida na kuwalazimu wabunge kumshangilia mfululizo Dk. Mpango ni pamoja na kufutwa kodi, adhabu na riba kwa magari chakavu; kuwatambua rasmi wafanyabiashara wadogowadogo kama mamalishe na wauza mitumba ambao sasa watapewe vitambulisho vyao maalumu; kufuta ushuru wa mabango yanayoonyesha mahala huduma za kijamii zinapotolewa ikiwamo shule na hospitali na pia kufutwa kwa ushuru wa makanyagio kwenye minada ya mifugo nchini kote.

Eneo jingine lililowakuna zaidi wabunge ni lile la kufutwa kwa kodi ya magari maarufu kama ‘road licence’, ambazo sasa makusanyo yake yamehamishiwa kwenye mafuta kila yanaponunuliwa na wenye magari.

Aidha, katika bajeti hiyo, miongoni mwa watu wanaotarajiwa kubanwa ni watumiaji wa vilevi mbalimbali pamoja na wavutao sigara ambao kwa ujumla, bidhaa zao nyingi zimeongezwa kodi kwa viwango mbalimbali, na hasa zile zitokazo nje ya nchi.

Pia walioguswa zaidi ni pamoja na wachimbaji wadogo wa madini ambao sasa watalazimika kulipia kodi asilimia tano huku pia kukitolewa uamuzi wa kutoruhusu tena usafirishaji wa madini kwenda moja kwa moja nje ya nchi kwa kutoka kwenye migodi husika.

Wakati akihitimisha uwasilishaji wa bajeti yake hiyo, Waziri Mpango aliwataka Watanzania kuendelea kuiunga mkono Serikali katika jitihada zake za kuwaletea maendeleo.


“Kwakweli, hapajawahi kuwa na bajeti nzuri kama hii  kwa miaka mingi,” alisema Spika wa Bunge, Job Ndugai mara baada ya Dk. Mpango kumaliza kazi ya kuwasilisha bajeti hiyo na kuibua shangwe kubwa kutoka kwa wabunge.

BEI POA ZA VYAKULA, MAISHA NAFUU:

Miongoni mwa mambo yaliyokuwa yakisubiriwa kwa hamu na wananchi walio wengi ni pamoja na kuona ni kwa namna gani bajeti hiyo itasaidia udhibiti wa bei za vyakula, vikiwamo vya nafaka za unga, mchele na maharage.

Hata hivyo, pengine kwa kutambua hilo, Dk. Mpango alisema ushuru wa mazao ya vyakula umepunguzwa kutoka asilimia tano hadi mbili na pia asilimia tatu tu kwa mazao ya biashara.

Baadhi ya wabunge waliozungumza na waandishi wa habari jana walisema uamuzi huo wa Serikali utawezesha kuongeza fursa ya kukua kiuchumi kwa wakulima na pia kutopanda zaidi kwa bei za vyakula kwa sababu ya kupungua kwa mzigo wa gharama zitokanazo na ushuru huo kwa wafanyabiashara.

Kuhusu kuwatambua wafanyabiashara wadogo kama mama lishe na wauza mitumba, Dk. Mpango alisema jambo hilo litawawezesha kupata vitambulisho na mwishowe kupewa maeneo rasmi ya biashara.

Dk. Mpango alisema vilevile kuwa kuanzia Julai Mosi, kutakuwa na matumizi ya mashine za kodi za kielektroniki (EFD) kwa Wizara, Idara na taasisi zote za Serikali.

Pia itafunguliwa akaunti maalumu ya Escrow ili urahisisha marejesho ya ushuru wa ziada wa asilimia 17 unaolipwa na waagizaji sukari viwandani kurejeshwa kwa wakati.
Bajeti ya pili ya serikali ya awamu 5 kwa mwaka wa fedha 2017/2018. Bajeti ya pili ya serikali ya awamu 5 kwa mwaka wa fedha 2017/2018. Reviewed by Zero Degree on 6/09/2017 09:36:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.