Loading...

Bombadier ya 3 kuwasili nchini mwishoni mwa mwezi huu


NDEGE aina ya bombadier Q400 ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), inatarajiwa kuwasili mwishoni mwa mwezi huu na maandalizi ya kuipokea yameshaanza.

Kuwasili kwa ndege hiyo kutaifanya ATCL kuwa na ndege tatu za aina hiyo, baada ya zingine mbili kuwasili mwaka jana.

Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, Ladslaus Matindi, aliyasema hayo juzi wakati akizungumza na Nipashe kwa njia ya simu, na kueleza kwa sasa wanaandaa utaratibu wa kupokea ndege hiyo baada ya kuelezwa kila kitu kimekamilika.

Aidha, alisema Juni mwakani, ndege nyingine tatu aina ya B787 moja na CS300 mbili, zinatarajiwa kupokewa mwakani.

Katika hotuba ya bajeti ya mwaka 2017/18 ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Sh. bilioni 500 zimetengwa kwa ajili ya kukamilisha malipo ya ununuzi wa ndege tatu.

Kati yake mbili ni aina ya CS 300 na ndege kubwa moja ya masafa marefu aina ya Boeing 787 Dreamliner, na kwamba fedha hizo pia zitatumika kwa ajili ya kugharamia bima, mafunzo kwa marubani, wahandisi na wahudumu.

Pia, serikali imetenga Sh. bilioni 10 kwa ajili ya matengenezo ndege nne za Serikali.

Mwishoni mwa mwaka jana ndege zilianza safari za kwenda Mpanda, Katavi na kukiwa na mpango wa kupeleka kila mkoa lengo kuu ni kuunganisha mkoa huo wenye Hifadhi ya Taifa ya Katavi na mawasiliano ya anga, ili kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea hifadhi hiyo, hivyo kuongeza mapato zaidi.

Aidha, alisema ATCL iko mbioni kurudisha baadhi ya safari ambazo zilikuwapo awali za Arusha, Tabora na Mtwara, pamoja na kuongeza safari za Mbeya na
Kilimanjaro.

“Maandalizi ya safari za nje ya nchi yanaendelea mwaka huu sambamba na kuongeza idadi ya marubani na ndege. Tutautaarifu umma pindi maandalizi yakikamilika,” alibainisha.

Matindi alisema shirika hilo lina jumla ya ndege tatu, ambazo hufanya safari zake kwenye mikoa ya Mwanza, Kagera, Mbeya, Kigoma na Kilimanjaro/Zanzibar.

Aidha, alisema wataongeza safari za mikoa na idadi yake kwenye mabano kuwa ni Mwanza mara mbili kwa siku. Bukoba na Mbeya (tano) kwa wiki, Kigoma (nne), na Kilimanjaro/Zanzibar (tano) na hivi karibuni wameanza safari za Dodoma mara mbili kwa wiki.
Bombadier ya 3 kuwasili nchini mwishoni mwa mwezi huu Bombadier ya 3 kuwasili nchini mwishoni mwa mwezi huu Reviewed by Zero Degree on 6/18/2017 09:49:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.