Loading...

Jeshi la polisi limekamata Malori 30 yakidaiwa kuvusha chakula nje ya nchi

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Kamishna Msaidizi, Hamisi Issah.
SAA chache baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kutangaza serikali kutaifisha mahindi yote na malori yatakayokamatwa yakivusha chakula kwa magendo kwenda nje ya nchi, Kikosi kazi maalumu cha makachero wa Jeshi la Polisi kimekamata malori makubwa 30 kwa tuhuma za kusafirisha chakula hicho.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Kamishna Msaidizi, Hamisi Issah, alisema wanayashikilia malori hayo baada ya kuyanasa katika operesheni ya kushtukiza iliyofanyika usiku wa manane jana.

Malori hayo ambayo mengine yanadaiwa kukutwa yakiwa yamefichwa kwenye mashambani aina ya Scania, Mitsubishi Fusso na Isuzu Forward maarufu kama ‘Tandam’.

“Usiku wa kuamkia leo baada ya tamko la Waziri Mkuu, tulihamia mpakani na kwenye mji wa Himo ambako tumeshakamata malori makubwa 30 na mengine tumeyakuta yakifaulisha mzigo (mahindi) kwenye magari madogo. Tunawashilikia na tumeanza kuwahoji,” alisema. 

Alisema tayari kikosi kazi maalumu cha makachero kimeanza kupita kwenye mageti ya forodha yaliyopo mipaka ya Holili na Tarakea, Wilaya ya Rombo, kuchunguza ni kina nani au maofisa gani wa polisi na wafanyakazi wa vituo vya forodha wanahusika kwenye mtandao huo.

“Ingawa hatua ya kwanza tuliyochukua ni kuzuia mzigo usitoke, jambo la pili linalofanyika ni kuchunguza maofisa wa polisi na askari ambao wako kwenye huu mtandao wa kuvusha mahindi, japokuwa pia hata maofisa wa forodha baadhi yao wanatuhumiwa na tunawachunguza,” alisema. 

Juzi, Waziri Mkuu alisema serikali ilikuwa imepokea maombi kutoka nchi za jirani za Somalia, Ethiopia, Sudani Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, zikitaka kupatiwa msaada wa chakula.

Wakati akizungumzia hali ya chakula nchini, baada ya Swala ya Idd na Baraza la Idd El Fitri, Waziri Mkuu aliwashukia Polisi akisema kuwa serikali inazo taarifa kwamba kuna maofisa wa jeshi hilo wanaohusika katika kupitisha malori hayo mipakani.

Majaliwa alisema: “Na tunazo taarifa, jeshi letu la Polisi wengine wanahusika katika kupitisha malori hayo. Kamanda wa Polisi mkoa ukigundua kama kuna afisa wa Polisi anaushiriki katika kuondoa mahindi nje, chukua hicho cheo chake, huyo hatutakii mema Watanzania.” 

Alimtaka Kamanda huyo (ACP-Hamisi Issah) kumfuata Mkuu wa Jeshi la Polisi Mstaafu, IGP Said Mwema ambaye kwa sasa anaishi Moshi ampe mbinu za kiintelijensia za kuwapata wanaokimbiza mahindi kwenda nje ya nchi, huku akimwagiza pia kuweka ulinzi kwenye mipaka yote ya mkoa wa Kilimanjaro.
Jeshi la polisi limekamata Malori 30 yakidaiwa kuvusha chakula nje ya nchi Jeshi la polisi limekamata Malori 30 yakidaiwa kuvusha chakula nje ya nchi Reviewed by Zero Degree on 6/28/2017 11:55:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.